Huu si ulafi, ni ukichaa


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 02 May 2012

Printer-friendly version

NI laana? Jamaa wanaojiita Chama Cha Mungu ni kama vichaa! Wanavyotoa kauli, wanavyokula ovyo ni kama wendawazimu.

Hawasikii, hawajali na hawajui wanalofanya kwamba linashusha utu na heshima yao. Wanajiona ni timamu ila wengine mavuvuzela.

Wakati baadhi huugua ukichaa kwa kuvuta bangi au kutumia dawa za kulevya au kulogwa, hawa Chama Cha Mungu ni kutokana na ulevi wa madaraka.

Kichaa ni jasiri, ana uwezo wa kumkabili mtu yeyote wakati wowote bila woga akitaka kuomba kitu hasa chakula.

Kichaa akiwa na njaa ‘hupona’ kwa muda, ataonekana ‘mzima,’ atakuwa mpole, atatambua akinamama ndio wanaopika chakula na ndio wenye huruma. Anajua kina baba hawana huruma.

Basi atapita nyumba kwa nyumba, atajenga urafiki kwa muda akiomba chakula kwa upole. Atasifu umuhimu wa wanawake, atasaidia kazi kama vile kupasua kuni, kuchota maji na kubeba masufuria ili apewe chakula.

Lakini akishashiba wazimu humrudia na hapo anaweza kunyang’anya vitu. Atapita jalalani ataokota chochote na kula, japo ni nadra kuona kichaa ameugua magonjwa ya matumbo.

Ndiyo maana mtu yeyote akifanya jambo la kipuuzi utasikia, “Wee kichaa nini?” au “Acha wendawazimu!”

Hicho ndicho walichoiga Chama Cha Mungu. Wakiwa na njaa ya utawala hujenga urafiki na akinamama na kuwasifu hasa wa vijijini, lakini wakishapewa chakura huenda zao Dar es Salaam.

Hata vichaa hukimbilia maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu na mjini kwenye ulaji. Hivyo, siyo ajabu vichaa wengi kuonekana katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza au Mbeya na Chama Cha Mungu wamejazana huko, hurudi majimboni au vijijini walikozaliwa wanapotafuta chakura.

Kama walivyo vichaa, Chama Cha Mungu pia wanajua  akinamama ndio pekee bado wanawaonea huruma na kuwapa chakura.

Lakini wanachosahau akinamama hao ni kwamba hiyo huruma yao huwa ni shida kwa miaka mitano. Mfano mwaka 1995 jamaa ‘walipona kwa muda’ wakapewa chakura na waliposhiba wakaenda kunenepeana Dar es Salaam na kuanza kusambaza harufu ya utanda-wizi na ulafi.

Akinamama pamoja na shida walizopata kipindi chote waliingiwa tena huruma mwaka 2000 wakatoa chakura kwa jamaa hawa ambao walionyesha ukichaa kamili kwa kuchukua na kugawa kilafi mali alizotuachia Babu yetu Nyerere kuanzia viwanda hadi mkaa wa mawe.

Kichaa kilipanda zaidi mwaka 2005 ‘wakaingilia hata kibubu’ (BoT), wakachota nyekundu nyekundu tupu wakagawana. Wanaume jasiri walipoamua kuwakabili vichaa hao kuokoa mali, wakaambiwa Sh. 133 bilioni zimechotwa kwenye kibubu, wakagawana na kufichiana siri.

Mwaka 2010 tuliposikia vijana wanakwenda kuwaambia mama zao vijijini wasikubali tena kutoa chakura kwa wakora, tukaambiwa wamechelewa.

Tayari jamaa walikodi tai watatu kuwafuata akinamama wawape chakura. Ikawa kazi. Kule walipiga picha na akinamama  mchangani huku wamepakata watoto wao eti wanawapenda sana.

Vijana walipofika kuteta na mama zao wakaambiwa eti wamewahurumia vichaa! Wakati umefika wanawake wajiulize kuwa wataacha lini masihara ya kuhurumia wezi na walafi kuliko nafsi zao?

Kwa nini hawataki kuwahurumia watoto na wajukuu wao ambao elimu yao inaharibiwa, urithi wao unaporwa na waroho, walafi, wezi na vichaa?

Wanauza twiga, viwanja; wanakula rushwa ya madini, wanafisidi nchi kijasiri, wanajenga majumba ya kifahari.

Mwanamke gani hajui Chama Cha Mungu kinategemea chakura kutoka kwao? Nani hajui kuwa kwa miaka 15 vichaa wezi wamejenga urafiki nao? Nani hajui kuwa wezi wanalindwa na wezi? Vichaa hawa watatufilisi!

0658 383 979
0
No votes yet