Iwapi tija ya madini kwa umma


Sophia Yamola's picture

Na Sophia Yamola - Imechapwa 06 July 2011

Printer-friendly version

SERIKALI inasema sekta ya madini inakua kwa kasi. Ripoti mbalimbali kipindi cha miaka mitano iliyopita, zinaonyesha sekta imeingiza mapato ya dola 4.7 bilioni.

Kabla ya 2000, haikuwa na mchango wa maana kwa pato la taifa kwani hakukuwa na uwekezaji mkubwa.

Shughuli za utafiti, utafutaji na uchimbaji wa madini zilianza kushamiri mwaka 1998 ilipotungwa sheria na wawekezaji kuhamasishwa kuja.

Hatua hiyo iliongeza shughuli za utafiti na utafutaji madini na leo – miaka 13 baadaye, ndiyo tuna makampuni yaliyomilikishwa migodi kama ya Bulyanhulu, Buzwagi, North Mara, Tulawaka, Geita, Nzega na Buhemba.

Kwa hivyo, uwekezaji mkubwa unaofuatana na teknolojia ya kisasa, unaendelea kwa madini zaidi kugunduliwa – mengi yakiwa ni dhahabu.

Sasa Tanzania inatajwa kama nchi ya nne barani Afrika kwa kuzalisha madini; na ya tatu – nyuma ya Afrika Kusini na Ghana – kwa uzalishaji wa dhahabu.

Kiwango cha uzalishaji dhahabu nchini kimekua katika kipindi hicho kutoka tani moja ya dhahabu kwa mwaka hadi tani 50 mwaka 2010.

Sekta ya madini ni moja ya sekta zinazopewa kipaumbele katika mipango ya serikali kwani mchango wake kiuchumi unafuatia sekta ya utalii.

Maana yake, sekta ya madini inakua kwa kasi zaidi ya sekta nyingine, ikitanguliwa na utalii ambayo kwa wastani huchangia asilimia 25 katika Pato la Taifa.

Hata hivyo, mchango wake wa asilimia 3.8 ungali mdogo mno kulinganisha na faida inayopatikana. Mapato zaidi yangeingia serikalini iwapo utunzaji wa takwimu na utoaji wa misamaha ya kodi kwa wawekezaji ingetazamwa upya.

Uwezo mdogo wa serikali kuitawala na kuiongoza sekta hii, kiwango kidogo cha hatua za uongezeaji thamani kwa madini ghafi na uharibifu wa mazingira, huchangia sana kuinyima serikali mapato.

Isitoshe, sekta hii haijatoa mchango stahili katika kukuza sekta nyinginezo kama ajira, viwanda na miundombinu. Pia haijasaidia kuongezea wenyeji uwezo wa kuhudumia machimbo yao.

Malipo ya mishahara yanayopimwa kwa kiwango cha dola, na marupurupu makubwa kwa wafanyakazi wa nje, ni hatua zinazoneemesha wageni zaidi kuliko wenyeji ambao ilitarajiwa wanufaike na maliasili iliyoko nchini kwao.

Lipo tatizo la serikali kutoa misamaha ya kodi hata isiyofikirika kwa makampuni ya kigeni ikiwemo ile ya kulipa tozo dogo la mrabaha la dola 30 kwa kila wakia moja yenye thamani ya dola 1,000.

Mwaka jana, 2010, serikali iliifanyia marekebisho makubwa sheria ya madini. Lakini, bado kiwango cha mrabaha cha asilimia 4 kilichowekwa kutoka asilimia 3.8 ni kidogo kulinganisha na thamani halisi ya maliasili inayovunwa na kupelekwa nje.

Takwimu zinaonyesha mauzo ya nje ya dhahabu peke yake yalichangia asilimia 40 ya mapato yote yaliyotokana na uuzaji wa mazao yaliyozalishwa nchini kwa mwaka wa fedha uliopita.

Wataalamu wa uchumi wanasema mazingira mazuri ya kijiolojia na hali tengamano kisiasa iliyopo nchini, zimesaidia ukuaji wa sekta hii.

Lakini, tatizo kubwa kwa sasa ni ukuaji wa sekta hii kutosaidia ustawi wa jamii zinazoishi ilipo migodi.

Pale wawekezaji wanapovuna utajiri na kuusafirisha nje kibiashara, wenyeji wanabaki na mashimo na mazingira yaliyochafuliwa.

Wapo wanaosema Tanzania inajitakia kukosa mapato stahili. Kwa mfano, iweje viongozi waridhike na hata kusaini mikataba ya uchimbaji madini isiyozingatia maslahi ya nchi?

Iweje waziri alazimike kwenda Ulaya kusaini mkataba wa kuruhusu kampuni ya kigeni kuchimba madini nchini?

Kile alichowahi kukisema Rais Jakaya Kikwete kuwa utaalamu mdogo miongoni mwa Watanzania katika mikataba ya kimataifa, huchangia mikataba ya namna hiyo, hakikubaliki.

Kauli hiyo, inabeza msimamo wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliyetambua umuhimu wa maliasili ya madini hata kuamua kutoruhusu makabaila kuingia.

Akikataa kuruhusu wageni kuchimba madini, Mwalimu alisema, “Maliasili za nchi yetu, kama madini, ni kwa ajili ya Watanzania wa leo, wa kesho na wa keshokutwa.”

Ndiyo maana alikataa hoja za kukaribisha wawekezaji, kuja kupora madini yetu.

Alitaka wachimbaji wadogo waendelee kuchimba madini kwa kuamini mavuno wakati ule yalitosheleza haja ya kuinua ustawi wao na uchumi wa nchi. Alichukia falsafa ya “hatutakuwepo watajiju” na aliamini kuchimba zaidi ingekuwa ulafi!

Laiti sekta hii ingesimamiwa vizuri, tija ingepatikana na kuchangia kupunguza umasikini. Tungeshuhudia maendeleo makubwa maeneo yanayozunguka migodi.

Miradi michache ya kijamii ambayo wawekezaji wanasifia kuigharamia kama hisani na siyo shuruti kimkataba, si endelevu na thamani yake kifedha haiendani na kiwango cha faida waipatayo.

Mfano mzuri ni Mwendakulima, kijiji cha wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga. Wananchi wanalalamika ahadi za wawekezaji wa mgodi wa Buzwagi, hazijatimizwa.

Waliahidiwa barabara nzuri, maji safi na salama, zahanati ya kisasa, ukamilishaji sekondari ya kijiji ikiwemo maabara ambayo walijenga jengo tu.

Halmashauri ambayo hulipwa dola 200,000 (zaidi ya Sh. 300 milioni) kila mwaka kwa ajili ya maendeleo ya watu, ndiyo iliyopaswa kuweka vifaa vya maabara. Haijatekeleza.

Badala yake, iliamuru wanakijiji wachangie ununuzi wa madawati. Kumbe, fedha hizo zinazotolewa na wawekezaji hazipelekwi moja kwa moja kwao, bali hujumuishwa na mapato ya wilaya na kupangwa mipango inayofikiria maeneo yote.

Mipango ya halmashauri si lazima iwe ndiyo vipaumbele vya eneo ulipo mgodi.

Tangu mwaka 1998 kampuni ya Resolute Co., Limited ya Australia ilipoanza kuchimba dhahabu mgodi wa Lusu chini ya mradi wa Golden Pride, wananchi wanaoishi maeneo yanayouzunguka, hawana cha kujivunia.

Miongoni mwao ni zaidi ya watu 1,000 waliokuwa wakinufaika na mgodi huo, wilayani Nzega, mkoani Tabora, kupitia uchimbaji mdogo.

Hawakulipwa fidia. Wajasiriamali wakiwemo mamia ya wanawake, waliokuwa wakitoa huduma ya biashara mbalimbali eneo la machimbo, siyo tu hawakulipwa kitu, bali hata mali zao zilizoteketezwa wakati wa uvunjaji makazi ya wachimbaji, hazikujaaliwa fidia yoyote.

Hakuna kiongozi aliyekuwa tayari wakati ule wala sasa kusikiliza kilio cha watu hao ingawa viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini walifika Lusu. Wote waliondoka kwa kuahidi kutafuta ufumbuzi. Hakuna aliyerudi kutimiza ahadi.

Wakati viongozi wakikwepa uwajibikaji, vijiji karibu vyote vinavyopakana na mgodi havina huduma ya maji safi. Lakini, lita zipatazo milioni moja huteketea kila mwezi kwa shughuli za mgodi.

Sasa baadhi ya mashimo ya uchimbaji yanafungwa, huku shimo jipya likisubiriwa kuanza uchimbaji. Hakuna taarifa muafaka za jambo hili. Wananchi hawajajulishwa; wala mali zao zikiwemo makazi, hazijatathminiwa. Nani anajali?

Somo: Tusikubali kuingiza mwekezaji mgodini bila kujua hatima ya wachimbaji wadogo; bila kujua manufaa watakayopata wananchi wa karibu na mgodi. Hawa wamilikishwe hisa na kuhakikishia wananchi miradi ya kijamii.

Vinginevyo, jitihada za uwekezaji katika sekta hii zitakuwa sawa na kupiga ngumi ukuta; na matamshi ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja hadi bungeni, yatamrudia.

sophiayamola@yahoo.com, 0715 221208
0
No votes yet