Jaji mkuu ni sehemu ya serikali?


Isaac Kimweri's picture

Na Isaac Kimweri - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

SEMINA elekezi iliyoandaliwa kwa ajili ya watendaji serikalini wiki tatu zilizopita mjini Dodoma imeibua jambo zito.

Jambo hilo ni ushiriki wa mihimili mingine miwili ya dola Bunge na Mahakama katika semina hiyo ambayo ililenga mhimili wa tatu – watendaji wakuu serikalini.

Katika hali ya kawaida, mihimili hii haitakiwi kuingiliana katika utendaji wake wa kila siku.

Kwa bahati mbaya na kwa kweli kwa utashi wa kiitikadi, katiba ya Jamhuri imempa ruhusa rais kuteua wabunge kuwa mawaziri na hivyo kulifanya bunge kuwa sehemu ya serikali. Kelele nyingi zimepigwa juu ya kasoro hii na naamini kuwa katiba mpya itashughulikia kasoro hii ili mihimili hii itenganishwe.

Wengi tunaamini mahakama haipokei amri wala maelekezo kutoka serikali wala bunge. Ni matumaini ya wengi kuwa mihimili hii itaendelea kutenganishwa kwa ajili ya kuboresha utawala bora katika taifa letu.

Kilichoshangaza katika semina elekezi ile ni uwepo, siku ya ufunguzi, wa Jaji Mkuu Othman Chande. Baadaye nilidokezwa kuwa alikuwa mmoja wa watoa mada (mwezeshaji).

Uhusika wa Jaji mkuu katika semina elekezi ya viongozi wa serikali unatia shaka na kuna kila sababu ya kuhoji utaratibu huu mpya wa utendaji kazi wa serikali ya awamu ya nne.

Jamhuri yetu si ya muungano wa mihimili ya dola kiasi cha kumfanya Jaji Mkuu kuwa sehemu ya serikali. Ili kumwepusha na majaribu yanayoweza kutia dosari maamuzi yake na uendeshaji wa mhimili wa mahakama, Jaji mkuu anapaswa kuwa mbali na maelekezo ya serikali – asiyasikie wala kuhusika kama chombo cha kuyatoa kwa watendaji wa serikali.

Hii ni kwa sababu, baadhi ya watendaji wa serikali wanaweza kujikuta wakitenda kazi zao kwa kuongozwa na jinsi jaji mkuu alivyosema au kujikuta wanamtumia kama shahidi wao ili kuwatisha waathirika wa maamuzi yao.

Jaji mkuu, kama mwanadamu, ana utashi binafsi na vionjo vya kiitikadi. Unapomhusisha katika semina elekezi ya watendaji wa serikali, unachokoza vionjo vyake na matamshi yake kiitikadi yanayoweza kuamsha na kuingilia maamuzi yake ya baadaye anaporejea katika wajibu wake wa kazi zake.

Ikumbukwe kuwa serikali iliyo madarakani ina sera maalum na ilani yake ya uchaguzi ambayo ni tofauti na vyama vingine ambavyo havijazuiwa kuchukua madaraka ya nchi wakati jaji mkuu akiwa bado madarakani. Hali hiyo ikitokea, jaji mkuu huyo atapokea au kushiriki semina elekezi ngapi?

Jaji mkuu ni kiongozi mkuu wa mhimili wa mahakama lakini si kiranja mkuu mwenye wajibu wa kuhakikisha majaji na mahakimu wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maelekezo yake katika jukumu la utoaji haki.

Majaji na mahakimu wana uhuru kamili wa kuendesha na kutoa maamuzi juu ya kesi mbalimbali na kwa hiyo ili kuutunza uhuru huo, jaji mkuu anapaswa ajiepushe na mazingira yoyote yanayoweza kumfanya kuingilia uhuru wa majaji na mahakimu.

Uhuru walionao majaji na mahakimu, anao pia Jaji mkuu. Lakini kwa kitendo cha kuhusishwa katika maelekezo maalum ya serikali kwa watendaji wake, amejifanya kuwa mtendaji kama wao na hivyo kupokea maelekezo ya mkuu wa serikali. Athari za kitendo hiki zitaonekana hivi punde katika utendaji wake.

Nasema haya kwa sababu uhuru wa mahakama umekuwa ukilalamikiwa na wengi. Uteuzi wa Jaji mkuu na majaji unaoacha maswali mengi, pamoja na mbinyo wa bajeti ya mahakama unaosababisha mahakama iwe ombaomba kwa serikali, vinaufanya uhuru wa mhimili huu uwe wa kinadharia zaidi.

Kuna mambo mengi ya kuhoji. Mathalani wakati wakuu wa mihimili ya serikali na bunge wana uhuru wa kuteua au hata kuongoza michakato ya kuchagua watendaji fulani katika mihimili yao, mhimili wa mahakama, jaji mkuu anateuliwa na rais na anapokea pia majaji atakaowaongoza kutoka kwa rais.

Hata kama rais anaweza kumshirikisha wakati wa uteuzi, bado hana mamlaka itoshayo juu ya majaji wengine kwa sababu aliyemteua yeye, ndiye aliyewateua wao. Utaratibu huu unaufanya mhimili wa mahakama kuwa sehemu ya mhimili wa serikali.

Matokeo ya mchakato huu wa kisiasa unaolazimishwa kuingia mahakamani, haki za watu zinacheleweshwa na hivi sasa bila fedha au kujuana na mtu mkubwa katika mahakama zetu ni ndoto mtu kupata haki yake kwa wakati.

Madhambi yaliyozagaa katika vyombo vingine vya dola na ndani ya serikali, yamezagaa pia katika mhimili wa mahakama kiasi cha kutishia amani ya taifa letu.

Imani ya maskini katika mahakama zetu imetoweka na kwa hiyo badala ya jaji mkuu kuhudhuria semina elekezi za serikali angeendesha za kwake ili kutafuta suluhu ya matatizo ya ndani ya mahakama.

Baba wa Taifa aliwahi kusema wakati akiwahutubia majaji kuwa, uhuru wa mahakama ni dhana kwanza kabla haijawa vitendo. Dhana hii inatakiwa ionekane uhalisi wake katika mwenendo wa majaji wenyewe na jinsi wanavyohusiana na viongozi wa serikali.

Mwenendo na maisha binafsi ya majaji vinahitaji visiache maswali juu ya uhuru wao katika kutoa maamuzi ya haki kwa Watanzania. Hivi sasa kuna wakuu wa mikoa (RC) na wilaya (DC) wanadiriki kuandika barua za maelekezo kwa mahakimu au kutoa maelekezo kwa watendaji wa chini yao kisha kuwapa nakala mahakimu kana kwamba wanataka barua hizo zitumike kama ushahidi dhidi ya watakaokiuka maelekezo hayo na kufikishwa mahakamani.

Imetokea hadharani mahakimu kuagizwa na ma-DC na ma-RC kujificha ili kuwakwepa wanasiasa wa vyama vya upinzani ili kutosaini viapo vyao nyakati za uchaguzi. Siyo siri tena kuwa majaji kupitia jaji mkuu wanapokea maelekezo ya nini kifanyike katika kesi nyeti zinazogusa maslahi ya kisiasa ya chama fulani au wanasiasa fulani.

Tumeshuhudia mahakimu wakipokea maelekezo maalum kutoka kwa wakuu wao juu nini kifanyike katika kesi fulani zenye mvuto wa kipekee. Tumeshuhudia masharti ya dhamana za washtakiwa fulani zikifanywa kuwa ngumu ili kuwaridhisha wakubwa fulani.

Vitendo vya namna hii vinaiondolea mahakama heshima na hadhi yake mbele ya jamii. Hata kukithiri kwa rushwa katika chombo hiki nyeti ni dalili tosha kuwa hakina uhuru wowote juu ya maamuzi na uendeshaji wake.

Uhuru kamili wa mahakama ni tishio kwa watawala dhalimu kuliko ulivyo tishio kwa wahalifu wa kawaida wa sheria. Kwa mantiki hiyo, kuongezeka udhalimu katika utawala wa nchi ni dalili kuwa uhuru wa mahakama unapungua.

Uwiano huu wa ongezeko la udhalimu wa watawala na kupungua kwa uhuru wa mahakama, ndicho kiini cha mwaliko wa jaji mkuu Othman Chande katika semina elekezi ya watendaji wa serikali kule Dodoma.

Tujiulize, siku serikali hii ikishtakiwa kwa ubadhirifu wa fedha za umma kupitia semina elekezi, Jaji Mkuu atakuwa mshatkiwa au shahidi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: