Jinsi ya kuua CHADEMA, rahisi


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 18 November 2009

Printer-friendly version

IWAPO wewe ni mwanachama wa chama cha siasa; umo katika upinzani na unataka kuua chama chako, huna sababu ya kutoka jasho. Ni rahisi sana; na ushahidi uliopo unaonyesha ni kazi nyepesi, au siyo kazi; ni mchezo tu.

Chukua fomu. Omba uongozi. Upate. Jikusanye na baadhi ya viongozi wenzako. Finyanga zimwi moja linaloitwa “ubaguzi.” Imba zimwi hilo usiku na mchana. Baada ya wiki kadhaa litakuwa zimwi kwelikweli.

Taarifa za kuwepo zimwi linaloitwa “ubaguzi,” zikienea; zikavuma kwa kasi; zikakua na kuota ndevu, zikikurudia basi utaamini na kusema, “Kumbe nilichokuwa nafikiri ndicho hicho wengine wameona.” Utaamini zimwi hilo; kumbe ni wewe ulilifinyanga.

Kaa chini ufinyange dada zimwi. Anaitwa “uonevu.” Sambaza taarifa juu ya dada huyu. Acha ziende mbali – kaskazini, magharibi na kusini. Acha zipate kasi na upepo uzirudishe mashariki – kule uliko; nawe utasema ulianza zamani kunusa dada uonevu; kumbe upo. Utaamini.

Na vyama vingi vimeshonwa kwa nyuzi nyepesi. Ni wanachama wachache sana waliomo wenye fikra za kupambana na kwa nia ya kuleta mabadiliko. Wachache. Hata wanaotaka mabadiliko katika utawala, hawapigani. Wengi wanadhani mabadiliko yatakuja tu kwa wao kuwa upinzani.

Wengi wametokana au walitokana na hotuba za viongozi wa awali au wa sasa. Ziliwavutia. Ziliwachochea. Ziliwapa ujasiri wa kufikiri na hata kutenda katika mazingira yao – pale walipo. Lakini viongozi wakimaliza kuhutubia, chama kimekwisha.

Kwa maana hiyo, chama kinakuwa kokoro. Nani asiyejua kokoro? Litupe ziwani au baharini. Muda wa kuopoa ukifika, vuta. Angalia kilichomo. Hakika kuna samaki. Hilo halina ubishi. Hata aina ya samaki ambao kuhutarajia kuvua; wamo.

Lakini kuna konokono pia. Vijiti. Mawe. Mafuvu ya viumbe waliofia majini. Majani. Mimea ya majini. Labda na nyoka na hata kobe wa majini. Kokoro hilo. Ndivyo lilivyo. Vyama vinapotupa kokoro la kisiasa, hata chama cha miaka mingi kama TANU/CCM, vinavua nyoka na magome ya konokono.

Huwezi kuepuka. Ukitaka kuepuka utabaki na “kachama kako ka mfukoni; ka kwako na mke wako au watani zako.” Hakakui. Hakapanuki. Kanajiviringisha kwenye mafiga kama mbwa asubiriye uzao wa harufu. Kujizungushazungusha.

Ukiweza kujua mapema kwamba kokoro lako limeleta kisicholiwa; na hii ni kazi kubwa ya kisayansi na ya muda mrefu na umakini usiotetereka; waweza kuweka mfumo wa kukabiliana na tabia za viumbe vilivyovuliwa lakini ambavyo hukuwa na nia ya kuvivua.

Ukishindwa kuwa na mkakati wa awali, tabia za viumbe ambavyo ulivua kwa makosa, kwa ushabiki au kwa kutojua au hata kwa uzembe; na ambavyo hukuwekea mpango maalum wa kuvinyambulisha pale vilipoingia kwenye uongozi; basi ujue huna chama.

Vyama ni vya watu. Siyo vya malaika. Watu wana tabia zao; nia zao na matarajio yao. Kwa malaika hatujui iwapo wanatumwa tu na kama wanafikisha ujumbe wanaopewa. Lakini kwa watu, tunakiri kutamani kusikokuwa na mipaka na hila.

Utukufu wa kisiasa unaumba miungu isiyopenda tena kusikiliza vilio vya wenye mahitaji; hata ya kawaida, badala ya kuumba wananchi na wanachama wenye neema. Na katika siasa, kama huna tamaa achana nayo. Huko ndiko makao makuu ya tamaa.

Katika siasa kuna tamaa ya kuona mambo yanabadilika. Tamaa ya kukosoa, kurekebisha, kusafisha au kuanza upya. Tamaa ni tofauti na uchu. Mahali ambako tamaa imechanganywa na uchu ndiko kuna “mapanga shasha.” Hujui kama kutakucha.

Hii siyo dini. Wala haya siyo mambo ya imani. Siasa siyo mchezo mchafu; bali kuna watu wachafu katika siasa; hata katika sayansi. Waliobuni jinsi ya kueneza ndui Vietnam, wakati wa vita kati ya nchi hiyo na Marekani; hata kama walitumiwa na wanasiasa, walikiuka maadili ya taaluma. Uchafu unaenezwa katika nyanja nyingi.

Sasa ukitaka kuua chama chako, ni rahisi sana. Waweza kutumia konokono. Waweza kutumia nyoka. Waweza kutumia samaki wa kale ambaye ameanza kuonekana kwenye pwani ya Tanga na Kilindini, Mombasa. Mawakala ni wengi. Hawana cha kupoteza.

Kinachohitajika ni kuwajaza pumzi hadi shingo zikafura. Wakishindwa kupumua; wakahema na katika hali hiyo waweza kuwapa ushauri kuwa ili kuhema vizuri au kuacha kuhema, unahitaji kufanya hili, hili na lile. Basi.

Watafanya utakacho. Weka orodha ya malalamiko. Watupie wenzako malalamiko hayo. Chungulia kwenye kokoro lako. Chota viumbe walioingia kwa bahati mbaya au kwa uzembe. Watupie wimbo wako wa manung’uniko, malalamiko na shutuma. Utagundua duniani kuna waimbaji wa vipaji ainaaina.

Wataimba. Watacheza. Vibwagizo wataweka, tena kwa mbwembwe na madoido. Ukitupa neno watalidaka. Watalifinyanga utakavyo wewe. Na wewe siyo chama. Hapo chama kitakaa kando. Wewe utakuwa wewe na waweza kusema “Mimi ni chama na chama ni mimi!”

Kwani haijawahi kutokea? Waulize wana-NCCR-Mageuzi. Pale mwenyekiti wao Augustine Mrema alipowaita viongozi kuwa ni nguruwe; “…siwezi kuachia nguruwe shamba? Na asitokee mtu akasema kuwa haya huletwa na CCM. Katika hili chama hicho kilichochoka kiachwe kando.

Mkorogo ambao wanachama wa CHADEMA wanakaribia kunywa, unaweza kuzidi ule ulionywewa na wanachama wa chama cha mageuzi. Ni sumu iliyoandaliwa rasmi kuleta maafa kabla ya uchaguzi wa 2010.

Panahitajika mtambuzi. Asimame mwaloni. Atambue samaki. Vurumai za sasa CHADEMA, hazina manufaa kwa chama hicho wala vyama vingine vya upinzani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: