JK ‘alikwina’ kumaliza mgomo wa madaktari


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version

KWA wazoefu wa kutazama filamu, kauli ya “staring hauawi” ni ya kawaida sana. Wanaotajwa katika kauli hii ni wahusika wakuu katika filamu, sinema au tamthiliya ya aina yoyote.

Katika filamu za mapigano, ya ngumi au vita, wapo wahusika waliojijengea umaarufu mkubwa duniani, kama Van Damme, Arnold Schwarzenegger, Sylvester Stallone na Michael Dudkoff.

Katika filamu zao, waigizaji hawa si rahisi kuuawa, japo hucheza katika nafasi za hatari na za kutisha. Mara nyingi, hadi mwisho wa mchezo wahusika hawa hujitokeza kuokoa wenzao waliozidiwa na hatimaye huondoka washindi.

Washiriki wengine ambao si “staring” katika filamu huchakazwa kwa kipigo, hujeruhiwa na hata kuuawa, lakini huvumilia mateso yote haya, ili kulinda heshima ya mhusika mkuu – “staring”.

Yaliyojitokeza wiki iliyopita kwenye sakata la madaktari na mgomo wao yanafanana sana na nafasi ya waigizaji kwenye filamu au sinema.

Filamu hii imetuonesha picha mbalimbali. Maelezo yake ni mengi na marefu, na wakati mwingine yanayopingana na kuchanganya.

Wakati wa mgomo wa kwanza uliodumu kwa siku 17, tulielezwa sababu zake kwa upande mmoja, na maelezo ya serikali kwa upande mwingine. Tulisikia vitisho vya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na jinsi madaktari hao walivyokaidi amri yake.

Walishuhudia jinsi walivyopimana naye nguvu. Wakaendelea na mgomo licha ya Waziri Mkuu kuwataka warejee kazini. Naye hakuwatimua kama alivyodai, badala yake akatoa ahadi za kumaliza matatizo yao – kumbe yeye hakuwa staring.

Tuliona namna madaktari ‘walivyokomaa’ pale waliposhtuka kuwa ahadi walizopewa na serikali hazitekelezeki, hasa baada ya muda waliopewa kumalizika.

Pia, kwamba ‘wabaya’ wao bado walikuwa wamekalia ofisi zinazotakiwa kutekeleza mahitaji yao ya kuwatengea maslahi bora na kutengeneza mazingira mazuri ya wao kufanyakazi kwa ufanisi.

Mwanzoni, filamu hii ilidhaniwa ingekuwa fupi. Ikaja kuwa ndefu ajabu. Ilianza mwanzoni mwa mwaka pale madaktari wanafunzi waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) walipogoma kushinikiza serikali iwalipe posho zao zilizocheleweshwa kwa miezi miwili.

Baada ya sehemu hii ya filamu iliyoendeshwa na viongozi wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kuwatimua na kuwahamisha, Chama cha Madaktari (MAT) kiliingilia kati. Kiliitisha mkutano wa dharura wa Baraza Kuu na kujadili hoja kadhaa na kuipa serikali saa 72 kuwarejesha madaktari hao Muhimbili.

Ndipo Dk. Lucy Nkya, naibu waziri wa afya, alipojitokeza kwenye filamu hii. Ilikuwa 17 Januari 2012, akidhaniwa ndiye “staring”, akatoa tamko la kupuuza madai ya madaktari na chama chao.

Akatetea sababu za kuwatimua Muhimbili, kuwa ni kutokana na kuvunja mkataba na mwajiri wao. Pia akawatuhumu kwa “kujihusisha na harakati.”

Kauli ya Dk. Nkya, mwanachama mwenzao wa MAT kabla ya kumfungia Jumamosi iliyopita, iliwatibua nyongo madaktari. Walisema imedhalilisha taaluma yao na kutuma ujumbe wa watu watatu ukiongozwa na Makamu wa Rais wa MAT, Dk. Primus Saidia kumuita kiongozi huyo kwenye mkutano wao Januari 19.

Siku hiyo madaktari walikusanyika ukumbi wa mikutano wa Don Bosco kumsubiri “Staring” Dk. Nkya. Nusu saa kabla ya muda uliopangwa, daktari huyo alibadili eneo, akawataka wakutane Arnautoglu, Mnazi Mmoja. Madaktari waligoma.

Vyombo vya habari baadaye vilimkariri Dk. Nkya akivua jukumu hilo, badala yake kuwataka wawasilishe madai yao kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE). Madaktari hawakukubali. Wakaona yeye si “staring.” Hakijaeleweka.

Walituma ujumbe wa watu watatu ukiongozwa na Rais wa MAT, Dk. Namala Mkopi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu wakapeleka pendekezo la kutaka kukutana naye. Hawakufanikiwa.

Ilipofika 23 Januari, wakatangaza mgomo huku wakiapa hawatazungumza na viongozi wa wizara. Waliowasusia ni Waziri, Dk. Hadji Mponda, naibu, Dk. Nkya, Katibu Mkuu Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali (CMO), Dk. Deo Mtasiwa.

Pia walimtaka Waziri Mkuu kumshauri Rais kuwaondoa Waziri na Naibu wake katika wizara hiyo kutokana na kushindwa kuwajibika – wameshindwa kuwa “staring” wa filamu yao.

Badala ya madai hayo kusikilizwa, Pinda alitoa wito kwa madaktari wote kurejea kazini 30 Januari na kwamba atakayekaidi itakuwa amejifuta kazi.

Agizo hili nalo halikuzingatiwa. Mgomo uliendelea na hali ikawa mbaya zaidi. Ukasambaa nchi nzima na ukaungwa mkono na madaktari bingwa. Wauguzi wakaahidi watajiunga hali isipodhibitiwa.

Pinda akakumbuka kuwa yeye hajakatiliwa. Akajitokeza upya kukutana na madaktari Muhimbili. Mara hii mnyenyekevu. Aliacha nyuma vitisho. Akatangaza kutekeleza walau nusu ya mahitaji yao. Akawasimamisha kazi Nyoni na Dk. Mtasiwa.

Akasema suala la mawaziri linamhusu Rais Kikwete. Akatoa ahadi na muda wa kutekeleza mahitaji yao.

Hapo sehemu ya kwanza ya filamu ikawa imekoma. Madaktari wakarejea kazini na maisha yakaendelea kama kawaida.

Mpaka hapo, “staing” alikuwa bado ni Pinda, waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Februari 29, mwaka huu Rais Kiwete alihutubia Taifa na kueleza kufurahishwa na uamuzi wa madaktari kusitisha mgomo na akasihi wafanye subira wakati serikali inashughulikia madai yao (bila shaka na hili na kuwatimua Dk. Mponda na Dk Nkya lilikuwamo).

Kamati iliyoundwa kushughulikia madai hayo ilipoketi Machi 3, mwaka huu kufanya tathmini, madaktari walibaini “wamepigwa changa la macho.”

Mawaziri walikuwa bado wanadunda. Madaktari wakatoa saa 72 (siku 3) wawajibike wenyewe au wawajibishwe; si hivyo wangeanza sehemu ya pili ya filamu.

Pinda alisihi wasigome na akasema serikali haioni sababu ya kuwawajibisha mawaziri hao. Akasahau kuwa alishasema “hilo limo mikononi mwa Rais Kikwete.”

Akamtetea Dk. Mponda, "mwenyewe anayelalamikiwa ndiyo kwanza ana mwaka mmoja na nusu kazini na hata madai mengine hayajui kwa kuwa hakuwepo."

Kwa hatua hiyo, ilionekana kama serikali imeshindwa kuwamudu madaktari, ikaomba msaada wa mahakama kwa maombi yaliyosikilizwa kwa siri tena upande mmoja.

Mahakama iliamuru madaktari wasitisha mgomo na kutangaza kurejea kazini. Maombi ya serikali yaliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

Taarifa za amri hiyo zilianza kutangazwa na vyombo vya habari vya serikali, lakini madaktari waliendeleza mgomo kwa maelezo kuwa hawajapata amri ya Mahakama.

Ghafla ikaja taarifa kuwa madaktari wameitwa na Rais Kikwete. Hii ilikuwa njia mbadala ya kumaliza mgomo wao baada ya wateule wake kushindwa.

Rais Kikwete amejizolea sifa nyingi kwa kufanikiwa kushawishi madaktari kuacha mgomo. Wenyewe wanasema wanamheshimu kiongozi na wanaamini madai yao yatashughulikiwa kwa wakati.

Kwanini alichelewa kujitokeza? Ingekuwa mkoani Iringa, wenyeji wangeuliza, “Alikwiya.” Alikuwa wapi?

Wangeuliza hivyo kwa sababu wanashangaa ilikuaje asubiri hadi “vijana” wake waaibike kwa kuonekana wameshindwa kazi? Vipi asijitokeze mapema; angeepusha kuongeza idadi ya vifo vya wagonjwa waliokosa tiba.

Kwa nini alishindwa kujitokeza mapema hadi madaktari wakatangaza kutokuwa na imani na viongozi wa wizara inayowasimamia? Kifilamu, staring alichelewa hadi wapambanaji wenzake wakajeruhiwa na kudhoofishwa.

Huenda jibu lake ni fupi tu: Alisubiri awe wa mwisho… yaani “staring” ambaye kawaida hauawi, lakini huishinda michezo yote na “kuwaokoa” wenzake.

Swali moja limebaki: Je, ataweza kuwaokoa mawaziri wake, au atawaweka kiporo kwa muda ili kulinda heshima yake; aje kuwatosa baadaye? Tungoje sehemu nyingine ya filamu hii.

0
No votes yet