JK na ‘wahalifu’ wenye majoho


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi

NILIWAHI kuhoji huko nyuma iwapo Rais Jakaya Kikwete ni mhalifu au ni rafiki wa wahalifu?

Ilikuwa pale alipowafanyia kampeni watuhumiwa wakuu wa ufisadi wakati serikali yake na chama chake walikuwa wanalalama juu ya kukithiri wa ufisadi nchini.

Alifanikiwa kuwapitisha wawili katika kinyanganyiro cha ubunge, lakini mmoja, Basil Mramba alisombwa na hasira za wananchi.

Hata walioshinda baada ya kufanyiwa kampeni na Rais Kikwete, wanadai kuwa ni jitihada zao wala si za rais. Hilo linahitaji mjadala wa pekee.

Juma lililopita Rais Kikwete alizusha tafrani tena pale alipowatuhumu viongozi wa dini kuwa nao siku za karibuni “wamevutiwa” na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Pamoja na kwamba baadhi ya vyombo vya habari viliongeza chumvi katika habari hiyo, lakini ni kweli hotuba ya rais mbele ya maaskofu wa Kanisa Katoliki huko Mbinga, ilibeba ujumbe wa kuwaambia Watanzania kuwa viongozi wa dini ni watuhumiwa wa biashara hii chafu.

Kilichofuata baada ya hapo ni malumbano ya piga nikupige. Jumuia ya Kikristo Tanzania (CCT) ilitoa tamko la haraka kumtaka Rais Kikwete awataje watuhumiwa hao. Alipewa saa 48 kuwa amewataja.

Ndani ya saa 48 hizo, ikulu kwa kupitia mwandishi wa Habari wa Rais, Premi Kibanga, ikatoa taarifa kusisitiza kuwa ni kweli wapo viongozi wa dini wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na kusisitiza kuwa si jukumu la rais kuwataja.

Taarifa ya ikulu ilitoa wito kwa viongozi hao, wanaojisikia kuwa wametuhumiwa na wanajua wanafanya biashara hiyo, basi wajitokeze wenyewe hadharani.

Siku moja baadaye, mkuu wa kitengo cha kuzuia dawa za kulevya, aitwaye Nzowa akamtaja mchungaji mmoja mwenye jina la Kinigeria lakini anayefanyia shughuli zake Biafra Kinondoni na akaahidi kuwataja wengine siku zijazo.

Haya mengine ni muhimu katika makala hii, ila napenda nijadili kidogo mwenendo wa serikali katika kushughulikia wahalifu wa makosa makubwa na ya hatari kama hili la dawa za kulevya.

Nakubaliana na rais na ikulu yake kuwa viongozi wa dini ni wanadamu, wenye udhaifu sawa tu na binadamu yeyote; hata  kutuhumiwa au hata kujihusisha na biashara ya namna hii.

Tumeshuhudia viongozi hawa na majoho, wakifanya mambo ya ajabu kuliko hata watu wasio na imani katika dini yoyote.

Kinacholeta ukakasi katika tamko la rais ni mambo makuu mawili: Tabia yake binafsi na ile ya serikali yake ya kucheka na wahalifu hatari. Pili, ni wakati gani mwafaka wa kuibua suala zito.

Kwa kuwa uhalifu hauchagui mtu, hakuna sababu ya rais wa nchi kuanza kubembeleza au kutumia vijembe katika kueleza ubaya wa dawa za kulevya katika taifa letu.

Kuwatuhumu viongozi wa dini bila kuchukua hatua ni hatari sana, kwani kama tunavyojua, viongozi hawa pia wana nguvu ya ushawishi katika jamii.

Ukiwatuhumu tu bila kuchukua hatua za wazi, kwanza unajenga fikra za ubaguzi kwamba kuna wahalifu wanaoheshimiwa na wengine wasioheshimiwa.

Pili, kama mkuu wa nchi unaleta fikra kwamba hata wewe unashiriki uhalifu huo; kwani unaujua uhalifu bali huushughulikii. 

Suala la muda mwafaka wa kuibua tuhuma, hili pia ni muhimu kuangaliwa kwa makini.

Wakati kama huu mwaka jana, serikali ya Rais Kikwete iliibuka na bajeti yenye mapendekezo ya kufuta misamaha ya kodi kwa mashirika ya dini.

Ilidaiwa wakati huo na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo kuwa, makanisa na viongozi wake wanakiuka masharti ya misamaha, hivyo kulikosesha kodi taifa.

Ulitolewa ufafanuzi kuwa makanisa kadhaa na viongozi wake wanaitumia misamaha ya kodi kufanya biashara na kujinufaisha binafsi.

Baada ya kelele nyingi za wadau na baadhi ya wabunge, kwa hekima kubwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikutana na viongozi wa dini na kujadili namna ya kurejesha misamaha hiyo sambamba na kushughulikia makanisa na viongozi wanaokiuka masharti ya misamaha hiyo.

Mpaka leo, Watanzania hawajaambiwa ni viongozi wangapi wa dini na mashirika yao, wamekamatwa au kufikishwa mahakamani kwa kosa la kutumia vibaya misamaha ya kodi.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa za Tanzania wanaamini ule ulikuwa ni mkwara wa serikali kuwanyamazisha viongozi wa dini ili wasitoe sauti yao kali wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka jana.

Misamaha ya kodi ilirejeshwa na serikali ikatoa ufafanuzi usiokidhi madai mazito yaliyokuwa yametolewa na waziri wa fedha.

Hivi sasa serikali inakabiliwa na changamoto nyingi kutoka kila upande. Ni kama mfumo mzima wa utawala umesimama na ni Mungu ajuaye nini kitatokea kesho na keshokutwa.

Kauli ya Rais Kikwete kuhusu viongozi wa dini kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya inaweza kuwa ililenga pia kunyamazisha baadhi ya sauti za viongozi wa dini.

Kwamba, kwa kuwa kuna viongozi wa dini wanaojihusisha na biashara hii, basi viongozi wa dini hawana uhalali tena wa kuisema na kuikosoa serikali yake.

Na kwa kuwa kuna tabia ya kubambikizana kesi katika mfumo wa dola yetu, yawezekana tuhuma zinazosemwa zikategenezwa ili ionekane kuwa ni kweli wapo viongozi wanaojihusiaha na biashara hii.

Watanzania mpaka leo hawajaambiwa matokeo ya tume iliyoundwa na Kamanda Said Mwema, kuchunguza tuhuma za kutaka kumbambikia dawa za kulevya, mtoto wa mfanyabiashara maarufu hapa nchini.

Kwa mazingira ya Tanzania, ukiona kimya, inawezekana “kisu kilifika kwenye mfupa.”

Hali ya kukata tamaa iliyoenea miongoni mwa wananchi wengi, haitokani na kukithiri kwa matatizo wala maovu katika jamii.

Kinachokatisha tamaa zaidi ni kuona viongozi wetu walioapa kutulinda tusipatwe na madhara ya uovu, wao wanacheka na uovu wenyewe.

Hata leo, hakuna dalili za viongozi wetu kumaliza kucheka hivi karibuni ili washughulikie kikamilifu matatizo yanayotukabili kama taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: