JK amenikosha, bado kiunzi kimoja


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

TANGU Rais Jakaya Kikwete alipotangaza Tume ya Katiba Ijumaa iliyopita yamesemwa maneno mengi. Wengi wamepongeza uteuzi huo, hasa baada ya kuona majina ya viongozi kadhaa wanaotambulika kuwa hawana makuu.

Mijadala mbalimbali niliyofuatilia, imebainisha kuwa majina ya akina Jaji Joseph Warioba, ambaye ni mwenyekiti wa tume, makamu wake, Jaji Augustino Ramadhani na wajumbe kama Dk. Salim Ahmed Salim, Joseph Butiku, Dk. Sengondo Mvungi, Profesa Mwesiga Baregu na wengine yanafaa kwa kazi hiyo.

Ukiacha suala la idadi ya wajumbe wa Tanzania Bara kuwa sawa na wale wa Zanzibar (15 kila upande), kwamba halijatazama ukubwa wa eneo wala idadi ya wakazi, sijasikia mjadala mwingine unaopinga uteuzi huu wa Kikwete.

Hata wale waonaosema wengi wa wajumbe hao ni waislamu, sioni hoja yao maana najua ingekuwa kazi kubwa kuwatafuta wakristo kutoka Zanzibar. Hivyo nami nashawishika kusema kuwa walau kwa hili, Rais wangu Kikwete amenikosha, japo bado kuna maeneo kadhaa ya kusimamia kuonesha kuwa kweli anayo nia isiyotetereka ya kuipatia Tanzania katiba mpya.

Nia hii ya Rais Kikwete ilianza kuonekana mapema mara tu baada ya uchaguzi mkuu wa 2010. Itakumbukwa kuwa suala hilo halikuwamo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010-2015, hoja hiyo ilikuwa ya wapinzani, na hasa CHADEMA waliosema bayana kuwa wangeanza mchakato wa kutafuta katiba mpya ndani ya siku 100.

Ndani ya kipindi hicho kilichotamkwa na mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, bila shaka Rais Kikwete aliona jinsi suala hilo linavyogusa umma wa Watanzania, na mahitaji ya katiba mpya, ndipo akatangaza kuanza mchakato huo bila kujali lilikuwamo kwenye ilani ya chama au la.

Wakati Rais Kikwete akitangaza hivyo, watendaji wake wakuu serikalini, akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, na Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani waliendelea kuwa wagumu.

Walieleza bayana kuwa hakukuwa na haja ya kuandikwa kwa katiba mpya, bali kinachotakiwa ni kufanyia marekebisho hii iliyopo, bila kujali kuwa inalalamikiwa.

Rais Kikwete aliruka kiunzi hicho cha mkorogano wa mawazo kati yake na watendaji wake. Yeye alizidi kusisitiza umuhimu wa katiba hiyo, japokuwa lugha yake haikuwa na tofauti sana na ya watendaji wake, na hasa kwa kutowachukulia hatua “kwa kupingana naye”.  

Ilipofika hatua ya kupitishwa muswada wa sheria ya marekebisho ya katiba, licha ya kupitishwa kwanza na Baraza la Mawaziri, ulionekana una kasoro nyingi na ikalazimu uondolewe bungeni  ufanyiwe marekebisho muhimu.

Pamoja na marekebisho yaliyofanyika, uliporejeshwa tena wakati wa Bunge la Bajeti,  bado ulikuwa na kasoro kadhaa ambazo zilisababisha wabunge wa CHADEMA na NCCR-Mageuzi kutoka bungeni kama ishara ya kuupinga.

Baada ya kutoka, wabunge hao waliamua kwenda kuonana na Rais Kikwete. Alikubali kukutana wajumbe wa chama hicho, vyama vingine na taasisi nyingine, kuhusiana na kasoro hizo. Hapa pia Rais Kikwete aliruka kiunzi kingine. Alikubali marekebisho kadhaa yafanyike kwenye sheria nje ya bunge. Marekebisho hayo yalirejeshwa bungeni baadaye ili “kubarikiwa” na wabunge.

Pamoja na kwamba marekebisho yaliyopendekezwa na CHADEMA hayakupita yote, lakini nia ya Rais Kikwete ya kulipatia taifa katiba mpya ilizidi kujidhihirisha, kinyume na matakwa ya baadhi ya wabunge wa chama chake.

Mlolongo wa matukio katika suala hilo unanishawishi nianze kuamini taarifa zilizozagaa, kuwa Rais Kikwete alikwishawaambia baadhi ya wasaidizi wake kuwa “mnisaidie ili niwaachie Watanzania katiba mpya”.

Yapo mawazo kuwa mawazo ya Rais Kikwete hayana tofauti na ya wasaidizi wake ambao hawaoni umuhimu wa katiba mpya, bali kuirekebisha iliyopo, lakini hatua yake ya kujitokeza mara kadhaa akiwa na mawazo tofauti na wao, ni ishara kuwa anataka kulipatia taifa kitu tofauti.

Hata uteuzi wa Tume ya Jaji Warioba, ni ishara kuwa Rais Kikwete ameendelea kuruka viunzi vya wapambe wasiotaka katiba mpya, hasa kwa kitendo chake cha kuwateua watu ambao makada wa CCM wanadhani ni wapinzani ndani ya chama.

Kinachotazamiwa sasa ni jinsi gani, wajumbe hao wa tume watatumia imani wanayopewa na Watanzania kukusanya maoni kwa haki, uhalisia, bila upendeleo wala ubaguzi na kutoa ripoti inayotazamiwa na wengi.

Ingawa hatujaelezwa hadidu za rejea watakazopewa wajumbe hao baada ya kuapishwa keshokutwa Ijumaa, matazamio ya wengi ni kugusa maeneo yote yanayolalamikiwa na umma. 

Baadhi ya maeneo yanayolalamikiwa ni mamlaka makubwa ya rais, tume ya uchaguzi kutokuwa huru, kero katika muundo wa muungano, na mengine mengi.

Hadidu za rejea zitakazotolewa na Rais Kikwete kitakuwa kipimo cha nia yake thabiti katika kutunga katiba mpya, au kuipachika viraka vipya ile ya sasa, ambayo tayari ina viraka vingi vilivyowekwa katika marekebisho 14.

Mbali na hadidu hizo, pia Rais Kikwete ndiye atapokea ripoti ya Jaji Warioba baada ya kipindi cha miezi 18 ya kukusanya maoni. Kwa nafasi hiyo, bila shaka rais atakuwa na nafasi ya kutia mkono wake, na hapo ndipo yalipolala mashaka ya watu wengi.

Pamoja na kwamba Rais Kikwete amejaribu kushawishi umma kuwa nia yake ya kutupatia katiba mpya ni ya kweli, na iko juu ya ile ya watendaji wake, mtihani pekee uliosalia ni aina ya hadidu za rejea atakazotoa, na jinsi atakavyofanyia kazi ripoti ya tume yake baada ya kuipokea.

Hatua hiyo ya mwisho, kabla ya ripoti kuwasilishwa  kwenye Bunge la Katiba na baadaye kupigiwa kura na wananchi, ndiyo inatarajiwa kuwa kiunzi cha mwisho cha Rais Kikwete.

Akiweza kuruka hapo, kwa maana ya kuendelea kukata kiu ya Watanzania ya kupata katiba mpya, atakuwa ametenda anachosema – kuwaachia  Watanzania kumbukumbu ya kudumu.

Pia, akiweza kuruka kiunzi hicho, mpira utakuwa umetoka mikononi mwake kwenda kwenye Bunge la Katiba.

Bunge hili litaundwa na wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi na wajumbe wengine 166 watakaoteuliwa na Rais kutoka taasisi zisizo za kiserikali, za dini na vyama vya siasa.

Pengine, nafasi ya rais inaweza pia kujitokeza katika kutangaza majina ya wajumbe wa Bunge la Katiba, na watendaji wake wakuu, yaani Katibu wa Bunge na msaidizi wake, lakini kama katika hatua za awali nia imekwishajionyesha kuwa njema, hatutarajii ibadilike ghafla katika hatua hii ya mwisho na kuharibu mchuzi aliopika mwenyewe.

0788 346175
0
No votes yet