JK anakosa ujasiri kuzungumzia ufisadi


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version

SINA uhakika iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaelewa kwa kina, athari kwa nchi itokanayo na ufisadi ambao umetanda ndani ya serikali yake – katika ngazi zote.

Ilani ya CCM (Ibara ya 189) imelipa suala hilo maneno 150 tu (ukurasa 229 hadi 230). Kwa upande wake Ilani ya CHADEMA imelipa suala hilo maneno 800 (ukurasa 61 hadi 65).

Ndiyo maana hata mgombea urais wa chama hicho, Jakaya Kikwete halizungumzii suala la ufisadi katika majukwaa ya kampeni zake, kwani chama hicho hakioni kama ni tatizo kubwa linalowakabili Watanzania.

Kama siyo tatizo, CCM wangeweka mambo sawa kwa kutamka kwamba ufisadi haupo bali hukuzwa tu na vyama vya upinzani na magazeti. Hapo angekuwa anaipatia nguvu hoja yake ya kutolizungumzia suala hilo.

Ukweli ni kwamba CCM yenyewe ni mhusika mkuu katika kutoa tahadhari ya athari katika mustakabali wa nchi inayotokana na kukithiri kwa ufisadi. Na tahadhari hiyo haijajikita mahala pengine popote isipokuwa katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2007.

Pamoja na mapungufu yake mengi tu, kama vile kutokuwa na tafsiri inayoeleweka ya neno “ufisadi” (corruption) au pia kupendekeza kwa adhabu ya faini mahala pa kifungo, sheria hiyo iliyoandaliwa na serikali ya CCM na kupitishwa na Bunge lenye wajumbe wengi kutoka chama hicho, imeweka wazi athari ya ufisadi nchini.

Sentensi ya kwanza katika utangulizi ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 inaanza hivi: “Wakati inatambulika kwamba ufisadi ni pingamizi kwa misingi ya demokrasia, utawala bora na haki za binadamu, na ni tishio kwa amani, utulivu na usalama…..”

Lakini viongozi wangapi wa juu ndani ya CCM wanaweza kuimba wimbo huo majukwaani, kwa sauti ya juu bila kigugumizi? Ni dhahiri hakuna. Narudia hakuna.

Kama wapo, basi hawa wanaogopa kukemewa nyuma ya mapazia au kupewa vitisho vya namna mbali mbali na kuambiwa kwamba wanakidhalilisha chama. Wiki iliyopita hali inayofanana na hiyo imemkumba Waziri mkuu wa zamani alipowataka wananchi wasiwachague viongozi wanaotoa rushwa ili washinde uchaguzi kwani hawataweza kujali matatizo yao wakishaingia madarakani.

Kwa ufupi CCM haipendi kuona viongozi wake wakuu wakizungumzia ufisadi kwa namna ambayo inakionyeshea kidole serikali ya chama hicho kwamba ndiye mtuhumiwa mkuu.

Na utamaduni huu haukuanza juzi au jana, au hata katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi. Ulianza katika kipindi cha utawala wa Awamu ya Pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi wakati bado upo mfumo wa demokrasia ya chama kimoja.

Mnamo mwanzoni mwa miaka ya 1990, aliyekuwa Mbunge (Viti maalum – Umoja wa Vijana wa CCM) Jenerali Ulimwengu alikwaruzana bungeni na aliyekuwa waziri mkuu, John Malecela pale mbunge huyo alipoishutumu serikali kwa kulea ufisadi bila ya wahusika kuchukuliwa hatua.

Ulimwengu, ambaye pia alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, alikuwa anawalenga wakuu wa mashirika ya umma waliofisidi mashirika yao na kuyafilisi huku wakijenga ‘makasri’ Mikocheni na sehemu nyingine bila ya serikali kuwachukulia hatua yoyote.

Malecela alikuja juu kwa kumwambia Ulimwengu kuwa kwa kuwa yeye (Ulimwengu) ni kiongozi wa serikali (mkuu wa wilaya) hakupaswa kuishutumu serikali kama alivyofanya.

Tukio hilo ndilo lililomfanya Ulimwengu kujiuzulu ukuu wa wilaya kwani aliona wadhifa huo unamzuia kusema kile kinachomkera.

Na miaka michache kabla ya hapo, aliyekuwa Waziri wa Biashara na Viwanda, Cleopa Msuya, akijibu swali bungeni alisema anayo orodha ya wakuu ya makampuni ya biashara ya mikoa (RTCs) waliohusika katika kuyatafuna makampuni hayo na kwamba alikuwa anaifanyia kazi orodha hiyo.

Siku chahche baadaye, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema alimuomba Msuya hiyo orodha ili awapeleke wahusika mahakamani. Msuya aligoma kumpa orodha akisema kwamba “haimhusu Mrema.”

Kwa wanaokumbuka historia vyema, watakubaliana nami kwamba Mrema ndiye alikuwa kiongozi wa kwanza serikalini kukumbana na kizingiti katika harakati za dhati za kupambana na ufisadi – kuanzia lile tukio la kukamatwa kwa fuko la dhahabu uwanja wa ndege wa Dar es Salaam kutoka kwa mtu mmoja aliyekuwa anasafiri kwenda nchi za Ghuba. Wakati huo kukutwa na dhahabu ilikuwa kosa kubwa la jinai.

Kuanzia hapo utamaduni umekuwa kulindana tu ndani ya chama hicho, hali ambayo ndiyo inaleta kigugumizi kwa wagombea wa chama hicho, hususan wa nafasi ya urais, Jakaya Kikwete kuzungumzia ufisadi katika majukwaa ya kampeni.

Hali lazima iwe iwe hivyo hasa ikizingatiwa namna yeye mwenyewe alivyoingia madarakani mwaka 2005, na namna alivyoshughulikia masuala ya ufisadi yaliyoibuka katika kipindi chake kama Richmond, EPA (hususan Kagoda).

Katika uchaguzi wa mwaka 1995, mgombea urais wa chama hicho Benjamin Mkapa alilizungumzia sana ufisadi katika kampeni zake. Tofauti na Kikwete, Mkapa aliweza kufanya hivyo kwa sababu yeye binafsi hakuwa na doa lolote la ufisadi wakati ule.

Katika kulizungumzia suala la ufisadi, imekuwa kawaida kwa viongozi wa CCM kutenganisha kansa hiyo na utawala wa chama hicho, kwamba ufisadi, kama upo ndani ya CCM, basi ni wa mtu mmoja mmoja.

Wanashikilia kwamba kusema CCM ni chama cha mafisadi siyo sahihi, kwani wanachama mmoja mmoja ndiyo mafisadi – na hawa wanashughulikiwa ipasavyo – na wanataja viongozi kadhaa ambao tayari wako mahakamani.

Lakini wanashindwa kukubali kwamba chama hicho kinalea mafisadi, na hivyo ufisadi kwa ujumla – kwani kuna baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi hasa ule wa kampuni ya Kagoda wanajulikana na hawajafikishwa mahakamani.

Hii ni kwa sababu fedha zilizotokana na ufisadi huo zilitumika katika kampeni za mwaka 2005 zilizomwingiza Kikwete madarakani. Mchakato wa mahakama ungeweza kuibua ukweli kuhusu hili.

Aidha tumeaona mashambulizi dhidi ya kada mmoja wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando, baada ya kuigusa CCM pabaya pale aliposema kwenye jukwaa la kampeni kwamba ushahidi anao wa kimaandishi wa kuonyesha kwamba fedha za Kagoda zilitumika katika kampeni za CCM za mwaka 2005. Pia aliwataja wahusika wa wizi huo.

Na hii ndiyo sababu kubwa na pekee inayomfanya Jakaya Kikwete kutolipa suala la ufisadi kipaumbele kinachostahili katika kampeni zinazoendelea—ndiyo maana alikataa kushiriki mdahalo uliopendekezwa baina ya wagombea wa urais.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: