JK kweli rais wa CCM


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

NIMEWAHI kuandika katika safu hii kauli nzito ya kwanza aliyotoa Barack Obama baada ya kushinda urais nchini Marekani.

Alisema, “Mimi ni rais wa Wamarekani. Nitawasikiliza sana Wamarekani hasa tunapotofautiana.”

Obama alitoa kauli hiyo akijua kwamba anatofautiana nao kuhusu kusudio la kufunga gereza la Guantanamo, urejeshaji nyumbani majeshi kutoka Afghanstan na Iraq, mpango wa bima ya afya na hivi karibuni ukomo wa madeni.

Serikali yake ilipowasilisha kwenye Bunge la Congress mpango wa Bima ya Afya, Rais Obama alilazimika kuahirisha safari ili ashawishi wapinzani wake, na hivi karibuni katika suala la ukomo wa kukopa, aliwaalika viongozi wa Republicans wajadili kwa manufaa ya taifa.

Kwa kufanya hivyo, akatekeleza kwa vitendo kauli yake ya “nitawasikiliza Wamarekani hasa tunapotofautiana”.

Rais wa kwanza kualikwa katika Ikulu ya White House alikuwa Rais Jakaya Kikwete, na aliporejea nchini, alimsifu Obama kuwa rafiki wa kweli.

Nilidhani Rais Kikwete, katika ziara ile, atakuwa aliiga namna ya kuwa rais wa Watanzania badala ya kuwa rais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Maana tofauti na Obama, Kikwete anapuuza maoni, ushauri na hoja zinazotolewa na wapinzani wake kisiasa akiziona kama kelele za mlango ambazo hazimzuii yeye kupiga usingizi.

Ni kweli Kikwete anachapa usingizi, kwani pamoja na kupigiwa honi juu ya ukali wa maisha, wanafunzi kunyimwa mikopo, wito wa mafisadi kushtakiwa na hivi karibuni kuhusu taratibu za uundwaji wa sheria ya katiba mpya, ameamua kusikiliza mbinja na vitimbi vya CCM.

Aliposikiliza hoja za raia na asasi za kiraia kupitia redio, televisheni na magazeti, alisubiri wabunge wa CCM wapitishe muswada wa sheria asubuhi kwa kura kisha jioni akawaalika wazee wa CCM kwenye ukumbi wa PTA wamshangilie anavyowananga wakosoaji wake.

Muswada ulipitishwa kwa kura baada ya vijembe vikali bila kuzingatia hoja. Wenye busara kati ya wabunge wa CCM waliojikita kwenye hoja walikuwa wachache.

Katika safu hii wiki iliyopita niliandika kwamba, mtindo huu wa wengi wape huwa hauzingatii uzito wa hoja ila wingi wa kura kurahisisha mambo. JK amethibitisha hivyo.

Wiki mbili baadaye akakubali kukutana na CHADEMA, na baadaye CUF. Katika kikao na CHADEMA, alikubaliana na hoja za wanasiasa hao, akasema, “Hata mimi naona mnazo hoja za msingi, lakini nikigoma kutia saini, wenzangu kwenye chama hawatanielewa”.

Akawa katika mtanziko. Lakini wenzake anaowaogopa ni kina nani? Si wana CCM waliobatiza rushwa kuwa ni takrima? Si hawa wanaonyosheana vidole katika ufisadi kupitia kampuni ya Richmond?

Si ‘waliokunywa’ fedha za rada na sasa wanakingiwa kifua wasishtakiwe? Waliojiuzia nyumba za serikali kwa bei poa na walioingia madarakani kwa fedha za EPA?

Upinzani umesema bungeni wezi hao washtakiwe lakini hawasikilizwi na rais yuko kimya. Akiwashtaki wenzake kwenye chama hawatamwelewa.

Wenzake kwenye chama ndio wanasema wizi wa EPA ni fedha kwa ajili ya usalama wa taifa na wezi kupitia Meremeta, ni fedha kwa matumizi ya Jeshi la Wananchi. Rais anaafiki kweli ufisadi huu ni kwa faida ya taifa?

Rais amekaa kimya, hataki kushinikiza wezi na mafisadi washtakiwe, kwa hofu wenzake hawatamwelewa. Ndiyo maana, hata katika muswada huu, ameamua kusikiliza watu walewale, mfumo uleule uliomweka madarakani na mwangwi uleule.

Tujiulize, Rais Kikwete ataulinda mfumo huu usio na maslahi kwa nchi hadi lini?

0658 383 979, Jmwangul@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 2.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: