Joel Bendera amedanganya Bunge

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limedanganywa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera.
Kusema kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lina mahusiano mazuri na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) hata kushirikiana katika matumizi ya fedha zinazotolewa na FIFA, hapo hakusema ukweli.
Bendera labda alijua anachokisema si sahihi au alipotoshwa na waliomuandalia jibu, lakini hata yanayoendelea sasa yanathibitisha uhusiano wa TFF na ZFA ni sawa na walivyo paka na panya.
Bendera ni mwanasoka mstaafu aliyewika ujanani hata kufanikiwa kuipeleka timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwenye michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980 iliyofanyika mjini Lagos, Nigeria.
Bendera ni mbunge wa Korogwe Mashariki, aliyeteuliwa Naibu Waziri wakati Rais Jakaya Kikwete akiunda serikali baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Alipojibu swali la Hafidh Ali Tahir (Dimani), naye mwanasoka mstaafu, mezani kwa Rais wa TFF, Leodgar Tenga, tayari ilikuwepo barua ya Rais wa ZFA, Ali Ferej Tamim, inayomwarifu uamuzi wa Zanzibar kusimamisha ushirikiano.
Ferej anasema uamuzi huo umetokana na ZFA kuchoka kudharauliwa na TFF.
Ferej anataka mawaziri wa michezo Zanzibar na Bara waingilie kati kwani maendeleo ya soka yanazorota Zanzibar huku TFF ikijitwalia mamlaka na kuamua kila kitu peke yao.
'ZFA inaziomba wizara husika na michezo kuliangalia suala hili kwa UZITO WAKE ili kila upande upate haki yake inayostahili badala ya upande upande mmoja kuhodhi kilicho chao na kisicho chao,' anasema katika barua ya 16 Mei, zaidi ya mwezi mmoja kabla ya Bendera kujibu swali bungeni.
Waziri wa Zanzibar, Ali Juma Shamhuna alipinga uamuzi wa ZFA lakini waziri mwenzake, George Mkuchika hakusema lolote. Ila ZFA haijafuta uamuzi huo na TFF haijasema lolote.
Miongoni mwa madai ya ZFA, ni Zanzibar kunyimwa sehemu ya dola 250,000 ambazo TFF inapewa kila mwaka na FIFA tangu 2004.
Pia ZFA inanyimwa sehemu ya dola 100,000 ambazo TFF inapewa kila mwaka na CAF kwa ajili ya maendeleo ya soka.
TFF imetumia fedha za FIFA kwa mradi wa GOAL ukihusisha ofisi za kisasa na jengo la ghorofa moja linalotumika hosteli ya wachezaji wa timu ya taifa ya vijana na imetengeneza uwanja wa Karume kufikia kiwango cha kisasa.
'Fedha zinazotoka FIFA dola 250,000 zigaiwe na Zanzibar hadi leo hata senti moja hamjaleta na hamtaki? CAF wanatoa dola 100,000 kwa Tanzania ZFA hawapati hata senti moja,' anasema Ferej.
ZFA pia inasema viongozi wa TFF wanakwepa kukutana na ZFA hata kwa vikao vilivyopangwa.
'Ikumbukwe TFF na ZFA iliunda Kamati ya watu 12 ili iwe inaangalia kero za soka ndani ya nchi lakini TFF imekataa kabisa kukutana kujadili masuala muhimu ya soka. Ukweli wa hayo ni pale ZFA walipoomba kikao mara mbili na TFF kutoa visingizio visivyofahamika.
'Kikao cha kwanza kiliombwa 30/3/2008 TFF mlisema mnajitayarisha na mkutano mkuu. ZFA waliomba tena kikao 14/4/2008 ikawa kila kitu kiko tayari TFF wakatoa taarifa kikao hicho hakipo bila ya sababu za msingi, hii tabia mbaya tena ya dharau isiyokubalika na muungwana yeyote anayejua anayo haki lakini ananyimwa.'
ZFA wanasema TFF peke yao huteua waamuzi na kupeleka majina yao CAF bila ya kushirikisha ZFA. Waamuzi hao ni wale wanaopangiwa mechi za kimataifa.
Madai mengine ni ya uteuzi wa viongozi wa kufuatana na Taifa Stars na wa kuhudhuria mikutano ya FIFA na CAF unaofanywa na TFF peke yao.
Naibu Waziri wa Michezo Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo, alipoongoza msafara wa Taifa Stars kwenda Burkina Faso kwa mechi ya mashindano, hakugharamiwa na TFF bali SMZ.
Ni Kombo aliyechangia kupatikana kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Burkina Faso na timu kualikwa kuingia Bungeni na kula na kufurahi pamoja na wabunge mjini Dodoma.
Mbunge wa Dimani aliuliza bungeni namna ZFA inavyonufaika na fedha za misaada inazopata TFF kutoka FIFA ambazo Zanzibar pia inastahili kunufaika.
Katika majibu, Bendera alisema yamekuwepo mashirikiano mazuri na fedha hizo zinapofika, TFF hupanga matumizi na ZFA.
Hayo yanatokea wakati mwanaharakati wa Zanzibar, Rashid Salum Adiy, amemwandikia Rais wa TFF barua ya kutaka maelezo ya kuridhisha ndani ya mwezi mmoja kuhusu madai kama hayo, si hivyo ataipeleka TFF mahakamani.
Adiy akitumia kampuni ya uwakili ya ALI. O. JUMA, BSO ya mwanasheria Ali Omar Juma, analalamikia TFF kujitwalia mamlaka ya kuiwakilisha ZFA bila ya kuishirikisha wakati ndiyo chama kinachowakilisha sehemu moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Asipopata majibu hayo kufikia 30 Julai, mawakili wake watafungua mashitaka Mahakama Kuu ya Zanzibar bila ya kutoa indhari yoyote.
ZFA ilikuwa na ushirikiano mzuri wakati wa FAT wakiandaa michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania iliyokuwa ikitoa bingwa wa kuwania bingwa wa Afrika na Kombe la Washindi.
Hali hiyo ilikuwepo tangu FAT ilipokuwa na akina Said El Maamry hadi walipoishia Mwenyekiti Muhidin Ndolanga na Katibu Mkuu, Ismail Aden Rage.