John Mnyika: Nguzo muhimu Chadema


William Kapawaga's picture

Na William Kapawaga - Imechapwa 28 January 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana
John John Mnyika

ANAITWA John John Mnyika, lakini mwenyewe anapenda kuitwa (JJ). Ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa, katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika mahojiano na MwanaHALISI wiki hii, Mnyika (28), pamoja na mambo mengine, anasema kazi yake ni kutangaza sera za chama chake kimataifa.

Anasema, “Tunakwenda mikoani kutangaza Chadema, lakini tukiwa chama mbadala kinachosubiri kuingia madarakani, ni muhimu pia tukajiimarisha kimataifa.”

“Lengo ni kujitangaza kimataifa ili tunaposhika madaraka tayari ndani na nje wawe wametuelewa na kuelewa sera zetu,” anafafanua Mnyika taratibu.

Anasema Sera ya Nje ya sasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) haikidhi matakwa ya wananchi, hivyo lengo la chama chake ni kuwa na sera bora na mbadala.

Anasema tayari wameanza kupokea maoni kwa njia mbalimbali ikiwamo mtandao wa intaneti na barua. Anasema baadaye watapita kila mkoa na wilaya kuuliza wananchi, “nini wanataka kiwe katika sera ya mambo ya nje.”

Mnyika anasema sera ya nje ya CCM ni dhaifu na ndiyo ilisababisha serikali kushindwa kusimamia vizuri makampuni yaliyowekeza katika migodi.

Mnyika anasema pamoja na kutangaza sera za chama chao nje ya nchi, idara yake pia ina jukumu la kutafuta marafiki kutoka vyama mbalimbali duniani.

Anasema Chadema ina ushirikiano na vyama mbalimbali duniani ikiwamo Conservative cha Uingereza, Republican na Democratic vya Marekani, FDC cha Uganda na NPP cha Ghana.

Vilevile, Chadema ina mahusiano mazuri na vyama tawala vya Norway na Sweden. Chadema ni mwanachama pia wa muungano ujulikanao kama Democratic Union of Afrika (DUA). Mnyika ndiye mratibu wa umoja huo. Makao makuu ya Sektarieti ya DUA yapo Tanzania.

Juu ya matumizi ya fedha kutoka nchi za nje, Mnyika anasema siyo sahihi kwa vyama vya siasa kuendesha shughuli zao za kila siku kwa fedha kutoka nje.

“Chadema hakipokei fedha kutoka nje kwa ajili ya kujiendesha. Chama chetu kinaendeshwa kwa ruzuku ya serikali na michango ya wanachama,” amesisitiza.

Anasema, hata hivyo, kuwa wanachama na viongozi ndio wachangiaji wakuu wa chama na kwamba wabunge wa Chadema wamekuwa wanachanga fedha kila mwezi kutoka kwenye mishahara yao ili kuendesha chama.

“Fedha tunazopata kutoka nje, tunazitumia kwa mafunzo ya viongozi wa ngazi mbalimbali. Haziwezi kuendesha shughuli za kila siku za chama. Kwanza, ni kidogo, lakini pia siyo sera ya Chadema wala wale wanaozitoa,” anafafanua.

Mnyika ni kiongozi na mtumishi. Ni mbunifu pia. Alipokuwa mkurugenzi wa vijana, ni yeye aliyebuni mfuko wa kuchangia feha ili kuwezesha vijana wengi kuingia bungeni na kwamba ndio utasaidia katika uchaguzi wa 2010.

Kuhusu ushirikiano wa vyama vya upinzani, Mnyika anasema, “Ulivunjika wakati wa kampeni za ubunge na udiwani, wilayani Tarime, mkoani Mara. Na sasa hali ni mbaya zaidi kutokana na matamshi na matendo ya baadhi ya viongozi wa upinzani.”

Kwa mfano, anasema baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wamekuwa wakitoa kauli mbalimbali katika vyombo vya habari kushutumu uongozi wa Chadema.

Lakini pamoja na viongozi hao kutoa kauli hizo Mnyika anasema watajitahidi kuhakikisha ushirikiano uliopo ndani ya Bunge hauvunjiki. Kuvunjika kwa kambi ya upinzani bungeni kutaondoa wasemaji rasmi wa wizara (mawaziri vivuli) na baadhi ya Kamati za kudumu za Bunge.

Baadhi ya kamati hizo ni Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa iliyo chini ya Dk. Slaa na  Kamati ya Hesabu ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Zitto.

Kuhusu tuhuma kwamba baadhi ya viongozi wa Chadema wamekuwa wakipigia kelele ufisadi, lakini wakati huohuo wakihusishwa na baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi, Mnyika anasema, “hiyo ni sehemu ya mkakati wa CCM kutuchafua.”

“Wanaotutuhumu wanatumiwa na wapinzani wetu wa kisiasa. Hii ni kutokana na msimamo wetu wa kupiga vita ufisadi,” anasema.

Kwa mfano, anasema Ismail Jusa Radhu (Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF), amewatuhumu ufisadi mbunge wa Viti Maalum, Grace Kiweru, Zitto na Mkurugenzi wa Fedha Anthony Komu. Lakini siyo siri kwamba Radhu ni swahiba mkuu wa mtuhumiwa Rostam Aziz.

Mnyika anasema Chadema inaamini kuwa kauli za Radhu ni kauli za Rostam na siyo za CUF. “Hatukujibu tuhuma hizo. Tungejibu kama tuhuma zingetolewa na viongozi wakuu wa CUF.

Mnyika anasema kampeni za Chadema za kupambana na ufisadi zimeleta mafanikio makubwa na kuwa ndio chanzo au kichocheo kikuu cha wananchi na vyombo vya habari kuvalia njuga ufisadi nchini.

“Hakuna kulala. Tutakwenda nyumba kwa nyumba na kijiji kwa kijiji. Tunataka wote waliohusika na uporaji wa rasilimali za taifa, wanakamatwa na kufikishwa mahakamani,” anasema.

Anasema hatua ya serikali ya kushindwa kumfikisha mahakamani mmiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, iliyochota zaidi ya Sh. 40 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kunaitia doa serikali.

“Tunaamini kuwa kuna utatu usio mtakatifu kati ya  CCM, Kagoda na Rostam kutokana na kuhusishwa na mtandao wa uchotaji fedha katika BoT. Mpaka sasa, Chadema bado inaamini kwamba Kagoda ni mali ya Rostam na fedha zilizochotwa na Kagoda zilitumiwa na CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005,” anasema Mnyika.

Anatoa changamoto kwa CCM kwamba kama madai yake si ya kweli, ionyeshe ilipata wapi mabilioni ya shilingi yaliyomwagwa katika kofia, fulana, khanga, mabango ya matangazo na posho nono nchi mzima.

“Sisi katika mkutano wetu mkuu uliofanyika  Juni mwaka jana, tulitangaza kuwa tulitumia Sh.700 milioni. Tulitaja hadi waliotupa fedha hizo. Tukawataka CCM waseme wamepata wapi fedha za kampeni. Lakini mpaka sasa imeshindwa; hali inayopelekea tuamini kwamba walichota kutoka mfuko wa EPA,” anasema.

Hata hivyo, CCM kupitia Katibu wa Halmashauri Kuu (Itikadi na Uenezi), John Chiligati imekanusha chama chake kuhusika katika sakata la EPA.

Anasema Chadema ilichangiwa na wanachama na baadhi ya viongozi, lakini mchango mkubwa ulitolewa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo.

Anasema mbali ya kutoa fedha, viongozi hao pamoja na wengine wakiwamo wabunge wamekuwa wanatoa vitendea kazi yakiwamo magari.

Mnyika anasisitiza umuhimu wa vyama vya siasa nchini kuonyesha fedha zake za kampeni zinakotoka ili kuepusha nchi kuingia katika vurugu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: