Jussa, huwezi kuitetea CUF bila kuibua udini?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

KILA uchaguzi au aina yoyote ya ushindani inapomalizika na mshindi kutangazwa, tumezoea kusikia kauli tofauti zinazokinzana. Utasikia ama sababu za kweli au nyingine ambazo kwenye soka huita “visingizio” kutoka kwa walioshindwa.

Kwenye uchaguzi, anayetangazwa mshindi, hufurahia matokeo na kuelezea mipango yake ya baadaye. Lakini kama ushindi wake umegubikwa na tuhuma za “kuchakachua”, ndipo utasikia akitetea ushindi wake ili ukubalike kwa wapiga kura ambao “hawakumchagua”.

Ndivyo ilivyotokea katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Uzini uliomalizika hivi karibuni. Mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mohamedraza Hassanali Mohamedali (Raza) aliibuka na ushindi usiobishaniwa wa kura 5,377.

Aliyefuata ni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ali Mshimba Mbarouk aliyepata kuwa 281 na Salma Hussein Zarali wa Chama cha Wananchi (CUF) akifuatia kwa kura 223. Mgombea wa TADEA, Khamis Khatib Vuai alipata kura 14 na Rashid Yussuf Mchenga wa Chama cha Wakulima (AFP) akanyakua kura nane.

Sijasikia ubishi wowote dhidi ya ushindi wa Raza wala  wagombea wa TADEA na AFP; vivyo hivyo sijaona mjadala kuhusu ushindi na nafasi zao katika vyombo vya habari wala mitandao ya kijamii.

Kinachojadiliwa katika uchaguzi huo ni ushindi wa wagombea wa CHADEMA na CUF, na hasa kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Ismail Jussa kuhusu sababu za mgombea wa chama chake kushindwa.

Zanzibar imekuwa ngome ya vyama vya CUF na CCM. Hii ni kutokana na sababu za kihistoria, ambazo zimeshaelezwa sana na hakuna sababu ya kuzirejea. CUF imeikamata Pemba na maeneo machache Unguja na CCM inashika Unguja.

Vyama hivyo viwili, ndivyo zilivyotarajiwa kushika nafasi ya kwanza, na ya pili katika uchaguzi huo. Lakini mambo yakawa kinyume; CHADEMA ambacho hakikuwa mizizi huko, kikapenya na kushika nafasi ya pili.

Chama hicho kimefanikiwa kupenya na kujitambulisha Zanzibar kupitia Uzini, hatua ambayo ni ishara mbaya kwa CUF. Lakini Jussa kupitia ukurasa wake wa FaceBook, anasema hilo si jambo la ajabu.

“…Kumekuja analysis (uchambuzi) kuwa CHADEMA sasa inaipiku CUF kwa kushika nafasi ya pili, na wengine wakadiriki kusema kufukuzwa kwa Hamad Rashid kunakiathiri chama. ya Ubunge jimbo la Uzini ambapo CCM ilipata kura 6,651, CHADEMA 617 na CUF 524. Aliyekuwa mgombea wa CHADEMA kwa nafasi hiyo ni huyu Ali Mshimba Mbarouk ambaye amegombea Uwakilishi mara hii. Sasa kutoka kura 617 hadi 281 amepoteza mvuto kiasi gani? Isitoshe, CUF kwa kuzielewa siasa za Zanzibar hatukusumbuka kutumia fedha nyingi. Tumetumia milioni 7 tu wakati CHADEMA wamenambia wametumia milioni 60 (haidhuru mimi naamini wametumia zaidi kwa mambo tuliyoyaona kule). Sasa katika hali hiyo, kuna lipi jipya? Nani aliyepoteza? CUF inajua inachokifanya.

“Niwarejeshe kwenye matokeo ya 2010 kwa nafasi ya Ubunge (siyo Uwakilishi) jimbo la Uzini, CCM ilipata kura 6,651, CHADEMA 617 na CUF 524. Aliyekuwa mgombea wa CHADEMA kwa nafasi hiyo ni huyu Ali Mshimba Mbarouk ambaye amegombea Uwakilishi mara hii. Sasa kutoka kura 617 hadi 281 amepoteza mvuto kiasi gani?

“Isitoshe, CUF kwa kuzielewa siasa za Zanzibar hatukusumbuka kutumia fedha nyingi. Tumetumia Sh. 7 milioni tu wakati CHADEMA wameniambia wametumia Sh. 60 milioni (haidhuru mimi naamini wametumia zaidi kwa mambo tuliyoyaona kule). Sasa katika hali hiyo, kuna lipi jipya? Nani aliyepoteza? CUF inajua inachokifanya.”

Maelezo hayo ya Jussa, ingawa amelinganisha chaguzi mbili tofauti, Ubunge na Uwakilishi, zilizoshirikisha wagombea tofauti, isipokuwa Mshimba, walau hii ni hoja ya kisiasa, kuliko kauli yake nyingine aliyoitoa wiki iliyopita yenye harufu ya udini na ukabila.

Akieleza sababu za kushindwa kwa chama hicho wakati akihojiwa na Mlimani TV, Jussa alisema wapiga kura wengi wa Uzini ni wakristo na wana asili ya bara, hivyo CUF hawakupoteza muda wao kufanya kampeni ya nguvu.

Kauli hii haikufaa kutolewa na kiongozi wa chama chochote, na hasa CUF ambacho kimekuwa kinafanya jitihada kuondoka katika tope la udini, kilimotumbukizwa au kujitumbukiza kwa muda mrefu.

Watanzania wengi wanakumbuka kuwa wakati CUF ina nguvu bara na visiwani, kampeni za CCM dhidi yake zililenga kukidhoofisha. Zilikitaja cha kidini, cha waislamu. Watanzania walio wengi waliaminishwa hivyo.

Baada ya kuanza kushirikiana na CCM katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), madongo hayo dhidi yake yamepungua, lakini chama chenyewe hadi sasa kimeshindwa kujinasua katika mtego huo. Mbaya zaidi akina Jussa wanakitosa zaidi.

Hivi Jussa anataka kutuaminisha kuwa Raza wa CCM amechaguliwa Mwakilishi wa Uzini kwa sababu ya uislamu wake? Au kwamba Uzini walikuwa wanatafuta imamu, shekhe au kiongozi wa Jumuiaya ya Ismailia? Kama ndivyo, mbona wagombea wa vyama vyote walikuwa waislamu? Iweje uislamu wa Raza/CCM uwe bora kuliko wa wagombea wa CUF, CHADEMA, Tadea na AFP?

Au Jussa anataka kutonesha makovu ya udini ulioibuliwa na CCM na wapambe wake dhidi ya CHADEMA wakati wa uchaguzi mkuu 2010, kuwa ni chama cha wakristo?

Kwamba wakazi wa Uzini (wengi wakristo) ndio wamefanya mgombea wa CHADEMA kuwa wa pili badala ya CUF? Kama hilo ni sahihi, kwanini hawakuipa CHADEMA kiti cha kwanza cha uwakilishi badala ya CCM na vyama vingine?

Kwa kauli yake kwamba CUF imeshindwa Uzini kwa sababu kuna wabara wengi, ina maana waliochaguliwa kwa wingi—CCM akifuatiwa na CHADEMA, wanakubalika au wana asili ya bara kuliko CUF (yenye asili ya Zanzibar).

Jussa, wakati anatoa kauli hii alidhani itavigusa tu na kuviumiza vyama vingine na hasa CHADEMA, lakini bila shaka hakujua kuwa mshale aliorusha utageuka na kumfuata yeye na chama chake.

Tafsiri ya kina ya kauli yake inabainisha mambo matatu; mosi, CUF ambayo haikuungwa mkono hadi ikawa ya tatu katika uchaguzi wa Uzini ambako kuna ‘wakristo’ wengi, ni chama cha au kinaungwa mkono na waumini wa dini nyingine, ukiwamo uislamu na chenyewe hakikuona sababu ya kupiga kampeni za nguvu.

Pili, kwamba chama chake hakikubaliki Tanzania Bara. Kinyume na kauli za viongozi mbalimbali wa chama hicho, kuwa kina nguvu katika baadhi ya maeneo bara, yeye anasema wabara walioko Uzini wamesababisha CUF isipate ushindi wala kuambulia nafasi ya pili.

Tatu, viongozi wa chama hicho wanapishana kauli. Jussa anasema si mara ya kwanza CUF kushika nafasi ya tatu Uzini, baada ya CCM na CHADEMA, lakini juzi, mwenzake, Naibu Katibu Mkuu (Bara), Julius Mtatiro alisema chama hicho “kina kawaida” ya kutoshiriki uchaguzi wowote ambako kilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi uliotangulia.

Mtatiro alitoa kauli hiyo Ijumaa wakati anatangaza sababu za chama hicho kutoshiriki uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki, ambako CHADEMA kilishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2010.

Kauli za Jussa ambazo alikusudia zikisaidie chama hicho kuondokana na aibu ya kushindwa uchaguzi kwenye ngome yake, badala ya kukisaidia zinakizamisha zaidi kwenye tope kali la udini, ukabila, ambalo ni sumu kwa umoja wa Tanzania kama Jamhuri ya Muungano.

Tayari kauli hiyo imeanza kuwagawa wanachama wa CUF. Mmoja wao, Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Vijana wa Chama hicho Taifa, Omar Constantine anasema, “Kauli hiyo ya Jussa inathibitisha kwamba, mahali ambako kuna wananchi kutoka Tanzania Bara na Wakristo hakuna CUF. Huu ni ubaguzi mkubwa usioweza kuvumilika.”

Ni matarajio yangu kuwa Jussa atabaini udhaifu wa kauli yake na kuirekebisha ili siku za usoni yeye na viongozi wengine wa siasa waanze kuwa makini na hivyo kuliepushe taifa na kauli hatari za mgawanyiko.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: