Jussa: Zanzibar ni koloni la Tanzania?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 25 January 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

MWISHONI mwa wiki iliyopita viongozi waandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF) walikuwa kisiwani Pemba kuwaeleza wanachama wao na wananchi hatua zilizochukuliwa dhidi ya Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wenzake wa kuwapokonya uanachama wa chama hicho.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wengi, akiwapo kijana machachari na anayeibuka kwa kasi kubwa katika anga za siasa, Ismail Jussa Ladhu.

Huyu ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi jimbo la Mji Mkongwe ; Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar na Mkurugenzi wa Nje wa chama hicho. Kwa hakika ni mtu mzito kwa maelezo yoyote yale.

Kwa muda mrefu Jussa ameonekana kuwa nyota ya kizazi kipya katika siasa za Zanzibar,  akifananishwa na kundi kubwa la vijana waliojaa CHADEMA kwa sasa kama akina Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki), Godbless Lema (Mbunge wa Arusha Mjini), John Mnyika (Mbunge wa Ubungo), Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma Kaskazini), Halima Mdee (Mbunge wa Kawe) kutaja hao kwa uchache  tu.

Hili ni kundi la wanasiasa vijana wanaotaka kuona taifa hili likipiga hatua kutoka lilipo sasa ili kuwa na maendeleo zaidi.

Kila nikiwatazama wabunge hawa nawaona zaidi kama Watanzania. Wote wamezaliwa ndani ya Tanzania, si Tanganyika na Zanzibar zikiwa kila moja na lwake, chini ya mfumo unaotambua nchi moja kimataifa.

Nilijiaminisha ndani ya nafsi yangu kwamba huko tuendako ni lazima kizazi cha wanasiasa wa aina hii, wajielekeze kuizungumza zaidi Tanzania kuliko Tanganyika na Zanzibar.

Lakini Jussa akihutubia uwanja wa Gombani Pemba, alizungumza mengi, kubwa ni juu ya kilio chake kuwa harakati zinazofanywa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, za kutaka kuoongezewa eneo tengefu la bahari lenye urefu wa km 241.5 ni kuipora Zanzibar haki yake.

Jussa ameapa kwamba CUF itasimama kupigania haki ya Wazanzibari katika mapambano hayo ikiwa ni pamoja na kupigana hadi kufa ili eneo hilo lisiongezwe kwenye eneo la Tanzania.

Maombi ya Tanzania yamepelekwa Umoja wa Mataifa na timu ya wataalam ikiongozwa na Profesa Anna Tibaijuka. Jussa anapinga na anataka CUF, chama chake kipinge.

Nilitangulia kusema hapo juu kwamba nikiangalia aina ya wanasiasa wanaofanana na Jussa, nilijiaminisha kwamba hawafungwi na Utanganyika na Uzanzibari, lakini kumbe nilijidanganya sana.

Sikujua kwamba katika kundi hili la wanasiasa wapo vijana wanaojiangalia kwa upeo finyu sana wa hapo waliposimamia, na hawapati fursa ya kujitafakari na kuangalia mambo kidunia hivi na kutambua, kwa hakika changamoto zinazotukabilia kama taifa, haziwezi kuondoshwa ndani ya fikra za kujitengea himaya ama ya Uzanzibari – Unguja au Upemba, au Utananyika – uwe wa makabila makubwa au madogo.

Mwaka 1964, Julius Nyerere (Baba wa Taifa) na Abeid Karume, walitambua siasa za vikundi vidogo vidogo hivi  kuwa ni kikwazo kwa watu wao kupata maendeleo. Hili hata leo lina nguvu na litaendelea kupata nguvu.

Kwa bahati mbaya wale tulioamini kuwa vijana hawa wanaamini katika mwanga huu mpana wa kuyajua mambo kama Jussa, tulikosea; kumbe ndiyo kwanza wamefungwa katika siasa ambazo hazijafunguka sawasawa kujua kama kweli wanaamini katika Muungano au katika himaya ndogo ndogo.

Pamoja na kuamini katika himaya hizo ndogo ndogo, Jussa katika kauli yake ya kujiapiza kuwa CUF inaongoza mapambano ya kupinga Tanzania kuongezewa eneo hilo tengefu la bahari, anajikuta akifungua mlango mwingine wa ufahamu juu ya chama chake.

Kama CUF inapigania Zanzibar, sawa; je, Tanzania itapiganiwa na nani? CUF ni chama kilichoenea Tanzania nzima, kwa nini inajali mipaka ya Zanzibar tu ? Hata kama haitaki sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 inaharamisha vyama vya ukanda, majimbo au eneo moja ya nchi.

Kwa maana hiyo, hatua ya CUF kuibuka na kusema  itapinga Umoja wa Mataifa, Tanzania kuongezewa eneo tengefu la bahari ni sawa na kusema kwamba CUF inasimama badala ya Zanzibar lakini hatujui Tanzania inasimamiwa na nani katika hili.

Ndiyo maana nimesema Jussa bila kujua anaweza kuwa amegusa sehemu mpya ya ufahamu kwa watu kwa kutaka kuifungamanisha CUF na Zanzibar tu.

Ni dhahiri, kumekuwa na juhudi za kimakusudi za kutaka kuhalalisha kwamba Serikali ya Muungano wa Tanzania ni serikali ya Tanganyika. Kimantiki ndicho alichosema Jussa.

Lakini anajua wazi si kweli kwamba Tanganyika ni serikali ya Muungano wa Tanzania, si kisheria tu bali hata kwa matendo halisi na kimantiki tu.

Kwa hiyo, kama eneo tengefu la bahari likiongezwa wanufaikaji na eneo hili si Watanganyika tu kama ambavyo Jussa anataka watu waamini. Kwamba Wazanzibari hawatahusika na eneo hilo kwa kuwa tu limeombwa na Tanzania ni njia nyingine ya kujenga hoja nyepesi katika ukweli mpana wa mambo.

Kiongozi wa kitaifa wa ngazi ya Jussa, tena mwenye umri wa ujana kama yeye anapoamua kuingia katika siasa za maeneo kwa mambo ya kitaifa tena akikifungamanisha chama chake na hisia na siasa hizo, tatizo linakuwa kubwa zaidi.

Inawezekana kuna watu waanaamini kwamba Mungano ni kero kwao, wanaamini kuwa usalama na ustawi wao utahakikishwa zaidi katika siasa za kujigawa, siasa za vieneo, siasa za kutambuana kwa majina ya koo na kabila.

Wenye mawazo haya wanaweza kuamini wako sahihi sana, lakini wanasahau kuwa wanahubiri siasa za kupuuza hata ukubwa wa nyayo zao, wanapunguza uwezo wao wa kupanuka, wanapunguza uwezo wao wa kufika mbali na kupambana katika dunia hii ya utandawazi.

Nimalize kwa kumsihi Jussa awe makini na kauli za kutazama kila kitu katika sura ya Uzanzibari na Utanganyika. Mwanasiasa anayetaka kupambana hadi kufa kwa kitu ambacho kiko wazi basi huyo ana jambo lake, aghlabu si la kheri.

Jussa angejipa fursa ya kutafakari kwa mapana zaidi angejua kuwa Zanzibar haiwezi kwenda mbele ya Umoja wa Matifa kuomba iongozewe eneo tengefu la bahari kwa sababu mbele ya umoja huo, haipo, haina kiti, kama ina jambo lazima lipitie kwenye nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kama Jussa anaona vipi atangaze mgogoro kuwa Zanzibar imegeuzwa kuwa koloni ili aanze harakati za kudai uhuru.

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: