Kadhia ya Museveni


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Rais Yoweri Museveni

MATUKIO yanayoendelea kuikumba Uganda kwa muda sasa, yanatia simanzi. Wananchi wasio na hatia wanauawa, viongozi wa upinzani wanapigwa na kudhalilishwa. Kisa?

Wanaonekana kumpinga Rais Yoweri Museveni na serikali anayoiongoza. Museveni amekuwa rais wa Uganda tangu alipofanikisha mapinduzi mwaka 1986.

Picha za Rais wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC), Dk. Kizza Besigye, akivunjiwa kioo cha gari na kumwagiwa pilipili machoni na mwilini, zimeonyeshwa katika vyombo mbalimbali vya habari.

Mmoja wa maofisa usalama wa serikali ya Museveni, Gilbert Arinaitwe Bwana, alivunja kioo cha gari la Besigye kwa kutumia kitako cha bunduki na kumwaga pilipili machoni kwa kiongozi huyo lengo likiwa kumdhuru.

Na alipotoka nje ya gari lake, kipigo cha mbwa mwitu kilimkuta. Heshima ya Besigye kama binadamu na kiongozi haikuonekana. Kisaikolojia, Museveni alikuwa akituma ujumbe kwa wananchi kuwa kama anaweza kufanya vile kwa kiongozi, raia ajiulize anaweza kufanywa nini.

Kiongozi mwingine wa upinzani, Norbert Mao, wa Chama cha Democratic, amewekwa ndani kwa karibu wiki moja kwa hatua yake ya kutembea kwa miguu kwenda ofisini.

Wakati hayo yakiendelea, si viongozi wa serikali za Afrika Mashariki au vyama vya siasa vya upinzani vikiwemo vilivyo rafiki na wanasiasa wa upinzani wa Uganda waliokemea matendo hayo ya unyanyasaji na ukandamizaji haki za raia.

Kinachosumbua ni kuwa kinachomsukuma Museveni kunyanyasa raia ni madai yao ya kutaka serikali iingilie kati na kusaidia kushusha gharama za maisha kutokana na kupanda kwa kasi bei za bidhaa muhimu.

Kile kitendo cha raia kwenda kazini kwa miguu, ni moja ya hatua za kuthibitisha ugumu wa maisha kwani wamelenga kukwepa kulipa nauli kwa vile hawamudu.

Kama kweli kuna dhamira ya dhati ya kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki katika siku za mbele, tabia za aina hii za Museveni zikemewe.

Machi mwaka jana, nilipata nafasi ya kuzungumza na Dk. Besigye alipokuja nchini. Tulikutana hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, Dar es Salaam pamoja na viongozi wa upinzani wa Tanzania waliowakilisha vyama vyao.

Walijionyesha kama marafiki wa Besigye na wanaharakati wa kweli. Jambo la kushangaza ni hakuna yeyote aliyetoa tamko la kukemea matendo anayotendewa na Museveni.

Mtu unajiuliza iwapo hapa Tanzania kweli kuna vyama vya upinzani vinavyoundwa na wanaharakati wa kweli au kuna wanasiasa wa kufurahisha genge tu?

Nikiri mapema kuwa sitarajii, hata kwa dakika moja, kusikia viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakifanya lolote kukemea kinachofanywa na Museveni nchini kwake.

Ni kwa sababu viongozi wa vyama tawala barani Afrika wana tabia ya kuwa vipofu juu ya matendo maovu wanayotenda wenzao. Sababu ziko wazi – yule anayeishi katika nyumba ya vioo hawezi kurusha mawe kwa adui yake aliye nje.

Ndiyo maana nilitarajia viongozi wa vyama vya upinzani watakuwa wa kwanza kulaani mwenendo huu wa Museveni nchini Uganda na viongozi wengine wa aina yake katika ukanda huu. Hii itajenga vema dhana ya ujirani mwema na upinzani unaozingatia hali halisi ya Afrika Mashariki.

Zaidi ya hapo, kwa kufanya hivyo, ukurasa utakuwa umefunguliwa kwa wapinzani wa Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda kuwatetea wapinzani wa Tanzania ikitokea nao wamekumbwa na matatizo ya kunyanyaswa au kukandamizwa.

Na hapo ndipo viongozi wa serikali wataanza kuwa sikivu hata kutarajia wathubutu kuanza kuonyana mmoja anapotenda kosa. Huko ndiko kuvuana magamba.

Katika kanda ya Afrika Mashariki, Besigye na Raila Odinga wa Kenya; ndio wanasiasa wanaoonekana vinara wa upinzani. Pale mmoja wao anapoguswa halafu asiwepo mwanasiasa yeyote kukemea kwa sauti kali, inaashiria tatizo kubwa kisiasa. Haijengi picha ya mshikamano wa Afrika Mashariki.

Vitendo vya Museveni vinakatisha tamaa juhudi za kuunda shirikisho. Nani tena atataka kujiunga nalo wakati kuna kila dalili kwamba yu miongoni mwa wanasiasa wanaonyemelea kuliongoza?

Mtu anayeng’ang’ania madaraka kwa zaidi ya miaka 24. Mtu ambaye miaka mitano iliyopita alibadili Katiba ya nchi ili aruhusiwe kuwania urais hadi afe na kuondoa ukomo wa vipindi viwili vilivyowekwa na Katiba aliyoshiriki kuiunda.

Mtu asiye utu. Mtu anayeonyesha dalili za udikteta usiofahamika kwa wana Afrika Mashariki kwa maana ya kuushuhudia ukiwakandamiza. Nani atataka kujiunga na shirikisho la kisiasa analoliongoza? Hakuna.

Ni lazima vyama vya siasa, asasi za kijamii na serikali za Afrika Mashariki zijumuike na kumkemea rais Museveni badala ya kunyamaza na hivyo kumfanya ni kiongozi asiyeguswa.

Wanasaikolojia wanasema wanyama wote, akiwamo mwanadamu, wana kiwango cha mwisho cha uvumilivu. Inapotokea kiwango hicho kimepitwa, mwanadamu atafanya kile kilicho akilini mwake.

Akifikishwa hapo, haitakuwa rahisi kumrejesha katika hali yake ya kawaida au ile hali iliyokuwepo zamani katika jamii anayoishi.

Tunisia, Misri, Ivory Coast na Libya zilikuwa salama mwaka 1979 wakati Tanzania na Uganda zilipokuwa zikipigana vita zenyewe kwa zenyewe.

Wakati mauaji ya kimbari yakitokea nchini Rwanda mwaka 1994, hakukuwapo na wengine walioumia zaidi ya wananchi wa taifa hilo na sisi majirani zake wa Afrika Mashariki.

Afrika Mashariki isivumilie tena viongozi ambao aina zao za utawala na matendo yao yanachochea katika uchafuzi wa amani katika eneo letu hili.

Kikubwa ni lazima tuonyane wenyewe kwa wenyewe bila ya kuoneana aibu. Na kwanza tumkemee Museveni.

0718 81 48 75
0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)