Kama Jussa, kama Mohamedraza


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 04 April 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

ISMAIL Jussa Ladhu na Mohamedraza Hassan Dharamsi, ni wajumbe wapya wa Baraza la Wawakilishi, chombo mahsusi cha kutunga sheria kwa Zanzibar. Wanafanana.

Jussa, kiongozi mwandamizi katika Chama cha Wananchi (CUF) na mwakilishi mchaguliwa wa jimbo la Mji Mkongwe, amemtangulia Raza kuingia barazani.

Wakati Jussa aliingia kupitia uchaguzi mkuu wa 31 Oktoba 2010, Raza ameingia baada ya kula kiapo cha utii wiki tatu hivi tangu achaguliwe katika uchaguzi mdogo wa kujaza kiti kilichobaki wazi kufuatia kifo cha Mussa Khamis Silima, aliyekuwa mwakilishi.

Wajumbe hawa wamezalikana kutoka asili ya Kihindi, hata kama wanatoka sehemu (sectarian). Kizazi cha Jussa kimejichimbia Makunduchi, kusini mwa kisiwa cha Unguja, wakati cha Raza kimetoka Shakani, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Kwa maudhui ya hoja yangu, mfanano unaowaunganisha kifikra Jussa na Raza, unakuja pale ninapoangalia mshindo uliotokea baada ya kuingia barazani.

Pamoja na kujua ukakamavu alioonesha akiwa mwakilishi, nachukua mwanzo wa Jussa alipokuwa mbunge bunge lililokoma Oktoba 2010. Alitumikia ubunge kwa miezi minane baada ya kuingia kwa kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete tarehe 10 Februari mwaka huo.

Ilichukua muda mfupi sana Jussa kuchukiza wabunge wa CUF, wakiwemo wakongwe wa aina ya Hamad Rashid Mohamed ambaye ni dhahiri sasa amejiinamia kwa kuvuliwa uanachama na kubaki akisubiri hatima ya kesi yake Mahakama Kuu Dar es Salaam.

Jussa, baada ya kujulishwa haki zake za ubunge, na akiwa amelipwa angalau mshahara wa mwezi, aligundua kuwa wabunge waliomtangulia walidanganya chama.

Walidanganya kuhusu mapato waliyopaswa kuyasalimisha kwa chama kutokana na makubaliano ya kukipa chama hicho kiasi fulani cha mapato ya ubunge kwa ajili ya kuongeza mfuko wa fedha za chama.

Inafahamika Jussa alisalimisha kiasi “kikubwa” kuliko ilivyozoeleka. Mbunge wa siku chache kama yeye kujitokeza kama muadilifu kupita wale aliowakuta, kumemjengea imani zaidi huku akidhoofisha hadhi ya wabunge wenzake hao.

Si kutwa wachambuzi ndani ya CUF leo, wakiitaja kesi hiyo kama kitendo kilichochangia kumkosanisha Jussa na wabunge hao. Kivipi? Eti kwamba kwa kupeleka fedha zaidi yao kwa chama, amewaonesha si waadilifu.

Kwa kitendo hicho, ndipo hasa ninapomuweka kundi na Raza, mwakilishi aliyeanza kwa kutoa matamko ninayoona yanatishia hadhi za wawakilishi wenzake kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Raza ambaye anasema wazi kuwa wapo viongozi waandamizi katika chama hawakupenda aingie barazani, ametangaza rasmi kuwa atasalimisha mapato yake ya mshahara na maposho ya uwakilishi kwa wananchi wa jimbo la Uzini.

Mara tu alipomaliza kula kiapo Jumatano ya wiki iliyopita, mbele ya wawakilishi waliozoea wakiwemo wapya ambao waliingia barazani Novemba 2010, Raza alikimbilia vyombo vya habari.

Huku akisikilizwa na makumi ya wananchi wa jimbo analowakilisha, alisema ataweka hesabu vizuri za mapato yote atakayokuwa analipwa ya uwakilishi na yupo tayari kueleza kila baada ya muda namna yalivyotumika.

Tena alianza kueleza kuwa ameambiwa na ofisi ya Baraza la Wawakilishi mapato yake ya mwezi yanafikia Sh. milioni 4 na atakapofikia ukomo wa uwakilishi, Oktoba 2015, atarajie kulipwa hundi ya Sh. 64 milioni.

Mpaka atakapokoma utumishi wa uwakilishi Oktoba 2015, Raza atakuwa ametumika kwa miezi 44 na hivyo kupata mapato ya Sh. 192 milioni. Kwa kuchanganya na maposho, zaweza kufikia Sh. 250 milioni. Fedha hizi zitafanya mengi jimboni.

Amesema atakachofanya ni kwamba anavyohangaika kushughulikia kuondoa shida za wananachi jimboni, atakuwa akitumia kwa kuzingatia mapato hayo.

“Sijali kama nitalazimika kutoa matumizi ya ziada kwa ajili ya kufanikisha mahitaji ya wananchi. Ziada hii nimeshaahidi kuwa itatolewa na familia yangu, rafiki zangu na wahisani wangu. Kwa hili wananchi wa Uzini musiwe na wasiwasi kabisa,” ametamba.

Raza alikuwa anazungumzia namna alivyoanza kutekeleza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni ambapo alipita kila kijiji cha jimbo la Uzini na kujionea matatizo yanayosumbua wananchi.

Baadhi ya vijiji amekuta wananchi wanahitaji vituo vya afya – vipya kwa kuwa vilivyopo vimechoka na mwingine kujenga vipya pale vinapokosekana, maji safi, umeme, skuli bora, na kujenga njia za kuunganisha vijiji jimboni na nyingine zinazounganisha vijiji na vijiji vya majimbo jirani.

Jimbo la Uzini, lililopo Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, limepakana na majimbo ya Kitope, kwa kaskazini Magharibi; Chwaka kwa upande wa mashariki, Koani kwa kusini na Dole kwa upande wa Magharibi.

Kitu ambacho tayari kimeshtua wawakilishi pamoja na wabunge wa CCM, ikianzia na mbunge wa jimbo hilo, Muhammed Seif Khatib, ambaye ana vipindi vinne tangu 1995, ni kusabilia mapato yake kwa shughuli za maendeleo ya wanajimbo.

Raza tayari ametoa karibu Sh. 40 milioni kwa ajili ya kusaidia idara za maji na barabara kushughulikia matatizo yanayokwamisha kupatikana kwa huduma za maji safi na salama pamoja na kutengeneza njia za vijijini.

Raza ameonesha waandishi wa habari stakabadhi Na. 326999 ya 7 Machi 2012 inayothibitisha kupokelewa kwa Sh. 20 milioni na Idara ya Barabara zitakazotumika kushughulikia barabara za ndani ya jimbo.

Amemjulisha Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kuwa amelipa fedha hizo kwa madhumuni ya idara ya barabara kugharimia matengenezo ya barabara zilizokaguliwa rasmi katika jimbo hilo.

Raza amejulisha waandishi wa habari katika mkutano wake kuwa amelipa kiasi cha Sh. 12 milioni kwa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa ajili ya kugharamia mtandao wa maji safi kwa vijiji ambavyo havina huduma hiyo.

Kwa mwanzo huu wa utumishi wa uwakilishi wa wananchi, Raza ametandika jamvi la taswira halisi ya vile atakavyoumiza roho na fikra za waheshimiwa wenzake ndani ya CCM.

Waheshimiwa wa CCM majimboni watalazimika kujipanga upya kwani ninahakika watajikuta wakiulizwa “hivi mheshimiwa mwenzenu Raza anafanya vipi kuendeleza watu wa lile jimbo analowakilisha.”

Kwa mwanzo wake Raza, hapana shaka ndani ya miaka mitatu atakayotumikia wananchi wa Uzini, na iwapo hatakwamishwa na siasa chafu za ndani ya chama chake, jimbo la Uzini litakuwa na sura kunjufu kimaendeleo.

Hiyo italiondolea jimbo hili kubaki nyuma kama nilivyojadili makala zile za wakati wana CCM wamempa kura za maoni za kutosha kupiku makada vijana wa CCM.

Yale matumaini waliyoyawaza makada vijana wa CCM jimboni, kutaka mabadiliko mema, yatadhihirika muda si mrefu. Makada wa vijana hawa watapita mitaa ya jimbo wakiringa na kujivuna kuwa kama si msimamo wao, jimbo lingebaki kuendelea kutumiwa na wakubwa wa chama kama alama tu ya mapinduzi, huku likiachwa life kimaendeleo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: