Kama tatizo ni Jumapili, Ijumaa je?


Halifa Shabani's picture

Na Halifa Shabani - Imechapwa 07 July 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

MAASKOFU wa madhehebu ya Kikristo nchini Tanzania wametumia jukwaa lao walilozindua hivi karibuni kuitaka serikali ipange siku nyingine ya uchaguzi badala ya Jumapili kama ilivyozoeleka.

Maaskofu hao wameitaka serikali kuangalia upya na kutafuta siku nyingine mbadala na kuiacha Jumapili kuwa huru kwa Wakristo kuabudu.

Kauli hiyo si ya kwanza. Kabla ya hapo maaskofu wa dhehebu moja la kikristo walishasema kuwa kuifanya Jumapili siku ya uchaguzi ni kuwataka Wakristo kuchagua kimojawapo kati ya ibada na kupiga kura.

Wapo wanaounga mkono kauli ya maaskofu ya kutaka Jumapili isiwe siku ya uchaguzi na wapo wanaoipinga. Bahati nzuri, tofauti ya maoni kuhusu suala hilo haijawagawa wananchi katika misingi ya imani zao za kidini. Miongoni mwa wanaopinga wamo Wakristo na miongoni mwa wanaounga mkono wamo wasio Wakristo.

Wapo pia ambao licha ya kuwapinga maaskofu hao, wanawashutumu kwa kukosa uvumilivu wa kidini katika nchi yenye mchanganyiko wa imani. Wanahoji; kwa nini waione Jumapili moja katika miaka mitano na wasione Ijumaa zaidi ya 250 katika muda huo ambazo ni za ibada kwa wengine lakini hufanyishwa kazi?

Kama mtu ataamua kufanya utafiti kidogo, atagundua kuwa kwa wengi suala la siku ya uchaguzi kuwa au kutokuwa Jumapili halina umuhimu. Hakuna uzuri wala ubaya wa kuifanya au kutoifanya siku ya Jumapili au siku yoyote kuwa ya uchaguzi.

Kauli za mwanzo za maaskofu hao zilikuwa kali na thabiti. Mfano ni pale askofu Peter Mwamasika aliposema kuwa ni vema tume ya uchaguzi ikaheshimu uhuru wa kuabudu na kuiacha siku ya Jumapili huru ili Wakristo wakusanyike katika nyumba za ibada.
Askofu huyo alihoji: “Hivi unaweza kupanga siku ya uchaguzi kuwa Ijumaa halafu utarajie kuwapata Waislamu wakishiriki kikamilifu? Hapana; utawagawa, wengine wakati huo watakuwa misikitini.

Kushindwa kuzingatia ukweli huo kumesababisha watu wajiulize: “Kama kweli wao wanatetea uhuru wa kuabudu na kutenganisha ibada na shughuli nyingine, ni kwa nini Jumapili moja katika miaka mitano iwashughulishe badala ya kushughulishwa na Ijumaa zaidi ya 250 katika muda huo ambazo ni za ibada kwa waislamu lakini hufanyishwa kazi?”

Hakuna Mkristo anayefanya ibada kutwa nzima siku ya Jumapili hivyo muda wa kupiga kura Jumapili hiyo moja katika miaka mitano anao. Kwa Waislamu, sala ya Ijumaa hufanyika wakati wa kazi na masomo.

Ni lazima mtu aache kimojawapo kati ya sala na kazi au sala na masomo. Kwa walioko mashuleni na vyuoni, inawezekana kabisa wakati huo wa sala ukawa pia ni wakati wa mtihani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: