Kampeni ya Zitto ilifadhiliwa na nani?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 08 September 2009

Printer-friendly version

MKUTANO Mkuu wa Uchaguzi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umemalizika kwa Freeman Mbowe kuendelea kukalia kiti cha mwenyekiti.

Kampeni zilizovumishwa kuwa mikoa 11 ilikuwa inampendelea Zitto Kabwe (kuwa mwenyekiti) na kwamba ingempigia Mbowe “kura za maruhani” – za kumkataa, zimethibitika kuwa tupu na zilizolenga kuangamiza CHADEMA.

Lakini inaanza kusikika mitaani, kwamba hesabu hiyo ya “wapigakura za kumkataa Mbowe,” ilikuwa ya Msafiri Mtemelwa, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CHADEMA na Afisa wa Habari, David Kafulila ndani ya chama hicho.

Vijana hao wawili, ambao walikuwa wabeba bango la Zitto, ndio wametajwa kuwa wachagizaji wakuu wa kilichoitwa “kura zote kwa Zitto,” huku wakitoa madai na takwimu zisizokuwa sahihi ili kurubuni wajumbe wa mkutano mkuu.

Sasa kwamba Mbowe ameshinda kwa zaidi ya asilimia 93 ya kura zote zilizopigwa, haina maana kwamba wajumbe wote wa mkutano mkuu wamesema “basi yaishe,” baada ya Zitto kukataliwa kugombea uenyekiti.

Badala yake, kura nyingi kiasi hicho ni uthibitisho wa mambo kadhaa: Kwanza, kwamba takwimu za akina Mtemelwa kuwa kulikuwa na upinzani mkubwa na mkali dhidi ya Mbowe, hazikuwa sahihi.

Pili, kwamba Mbowe hakuwa na mpinzani mzito katika uchaguzi huo. Hivyo wapigadebe wa Zitto walikuwa wakikuza uzito wa Zitto ili kukidhi haja ya mradi wao. Ushindi huu unaonyesha kuwa hata kama Zitto angegombea, angeshindwa vibaya.

Tatu, kwamba kulikuwa na nia ya kuimega CHADEMA katika makundi mawili, bila kujali kama kundi la Mbowe lingebaki kubwa, alimradi kumeingia mtafaruku na CHADEMA isingebaki ileile ya zamani.

Nne, Zitto anatoka jimbo (Kigoma Kaskazini) ambalo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeapa kurudisha. Hivyo mgawanyiko katika CHADEMA ungeleta moja au mawili miongoni mwa mambo haya matatu:

Kwanza, kudhoofisha CHADEMA katika jimbo na kutoa mwanya kwa CCM kushinda. Pili, kutafuta jinsi ya kumshawishi Zitto kuingia CCM kama ilivyokuwa kwa Amani Kabourou.

Tatu, kwa kuleta mtafaruku CHADEMA na kukuza ugomvi mdogomdogo juu ya ukabila, matumizi ya fedha na mgawanyo wa vyeo, hadhi na umaarufu wa Zitto vingeshuka na hata kuisha; hivyo kuaga siasa akingali kijana.

Hili ndilo jambo ambalo wengi wanajiuliza kama Zitto alikuwa analifahamu au alikuwa amezibwa macho na shikinizo, ubinafsi na mafao mengine ambayo hayajawekwa bayana.

Bali linaloendelea kushangaza wengi ni kwamba Mbowe amemteua Zitto kuendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama chake, akisema kama mwanasiasa yeyote mzoefu angesema, “Yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo.”

Kuna wanaosema hatua ya Mbowe kurudishia Zitto nafasi yake kunaweza kusitisha, kwa muda, zogo la kugombea madaraka. Lakini hili linapingwa na wanaosema kuwa kama Zitto alikuwa na lengo, basi lingali palepale.

Tangu kuanzishwa kwake, miaka 17 iliyopita, CHADEMA haijawahi kukumbana na zogo la kunyang’anyana madaraka kama hili la sasa. Hiki ni chama ambacho kimekuwa kikiitwa “Chama cha Masikilizano.”

Wenyeviti wote waliotangulia, Edwin Mtei na Bob Makani waliondoka madarakani bila mkikiki. Hata Mbowe hakugombea nafasi hiyo hadi pale Makani alipoamua kustaafu.

Zogo ndani ya CHADEMA lilianza pale Zitto alipochukua fomu kugombea uongozi. “Vijana wake” walifanya kazi ya kuzizungusha kutafuta saini za wadhamini.

Kinacholeta mwanga juu ya nia mbaya katika kinyang’anyiro hicho ni kwamba, kama walivyozoea katika CHADEMA, wadhamini hawakujali hata kuangalia nafasi inayogombewa.

Ingekuwa Zitto anatafuta nafasi ya mwenyekiti, wangekuwa wanajua, kupitia vikao vyao kuwa sasa wanataka kubadili mwenyekiti. Hawakujua. Hivyo baadhi wamekiri kutojua kuwa Zitto alikuwa anatafuta uenyekiti.

Kwa mfano, Bob Makani – mwenyekiti mstaafu na mmoja wa baraza la wazee, ambaye alisaini fomu kumdhamini, anakiri kuwa alijua Zitto anagombea nafasi ya mwenyekiti baada ya fomu zake kurejeshwa na Mtemelwa.

Naye Profesa Mwesiga Baregu, mjumbe mwingine wa Kamati ya Wazee na aliyesaini fomu kumdhamini Zitto, anatoa kauli ileile kama ya Makani.

Kauli za wazee hawa wawili zinalenga kusisitiza jambo moja ambalo ni la kitamaduni katika CHADEMA na hata vyama vingine vinavyokwenda kwa mikakati thabiti.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho ameeleza, “Nafasi ya mwenyekiti haigombewi hivihivi tu, kwa kuviziana, bila kwanza kufanya mashauriano ndani ya vikao vya juu na kuangalia mwelekeo na mustakabali wa chama kwa ujumla. Hili hata Zitto analijua.”

Anasema hata wazee waliosaini kumdhamini Zitto walikuwa na “uhakika kuwa hakukuwa na maandalizi kwa ajili ya mwenyekiti mpya.”

Inawezekana basi kuwa Zitto na Mtemelwa walijua mapungufu hayo katika taratibu za chama chao na kuamua kuyatumia.

Mlipuko wa “Zitto kumng’oa Mbowe,” uliobebwa kwa mvumo mkali na vyombo vya habari, ulifanya CHADEMA kuelekezewa macho na masikio ya Watanzania.

Ni vikao vya juu vya CHADEMA vilivyopokea ushauri wa Kamati ya Wazee na kumshauri Zitto kuondoa jina lake kwa hofu kwamba hatua ya kuendeleza matakwa yake, ingejeruhi chama, lakini pia na yeye binafsi kisiasa.

CHADEMA inasema Zitto alikubali kuondoa jina lake. Vyombo vya habari vinakariri taarifa kuwa Zitto “alilazimishwa.” Bali Zitto, katika kukubali uteuzi wake wa kuwa naibu katibu mkuu, amesema amekubali uteuzi na kwamba hataisaliti CHADEMA.

Kama kauli hiyo inatoka rohoni mwake, basi maadui wa CHADEMA matumbo moto. Je, akina Mtemelwa wako katika hali gani? Vipi wale ambao walishabikia chama chao kuvunjika au kuingiliwa na mgogoro ambao ungekivunja?

Miongoni mwa mambo ambayo yalichagiza mgogoro katika hatua ya awali, zilikuwa kauli za kumpongeza Zitto kwa kutaka kugombea uenyekiti.

Kulikuwa na Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Augustine Mrema. Alisema kujitokeza kwa mpinzani wa Mbowe ni “kukua kwa demokrasia ndani ya CHADEMA na upinzani kwa jumla.”

Hapa bila shaka kila mtu ataona kuwa shetani anampongeza Mwana wa Mungu! Wanaomfahamu Mrema na chama chake wanaweza kujiuliza: Mrema anajua demokrasia? Iko wapi katika chama chake? Ile ya kusema, “Mimi ni chama na chama ni mimi?”

Mrema aliyekuwa anaanza kujitwisha bango la Zitto ndiye alimfukuza Benedicto Mtungirehi katika chama chake baada Mtungirehi kujitosa kuwania uenyekiti wa TLP. Ni miezi michache tu iliyopita.

Kiongozi wa TLP anapata wapi ujasiri na hekima ya kutambua demokrasia? Mbona chama chake kinakwenda kuzimu kutokana na kuendeshwa kwa fikra zake binafsi (kama zipo)?

Naye Tambwe Hizza wa CCM alinukuliwa akisema kumzuia Zitto kugombea ni ishara kwamba hakuna demokrasia. Hata hivyo, CCM haina mfumo wa demokrasia wa kuigwa na vyama vya siasa vichanga.

Lakini aliyekuwa anatembeza fomu za Zitto kutafuta saini, naye hana historia nzuri sana. Mtemelwa ni mjuzi wa mitafaruku ya uongozi ndani ya chama cha NCCR- Mageuzi.

Ni katika migogoro hiyo Mtemelwa alijizolea jina la “Black Mamba,” kutokana na kuandaa makundi ya vurugu yaliyoshabikia Mrema wakati huo wakisambaratisha NCCR-Mageuzi kabla ya kukimbilia TLP.

Mrema alimtumia Mtemelwa kama “dodoki” na hatimaye kumtema. Ni hivi majuzi tu Mtemelwa aliacha kazi yake ya mkurugenzi wa uchaguzi na kuwa “meneja wa kampeni” wa mgombea mmoja, Zitto.

Bali maswali yangali mengi. Kubwa ni hili: Kampeni ya Zitto ilikuwa inafadhiliwa na nani? Hadi sasa hakuna taarifa rasmi juu ya vyanzo vya fedha na ujasiri wa kumega kiota imara cha upinzani Tanzania bara.

Baadhi ya vyombo vya habari viliwahi kuchapisha taarifa zinazodai kuwa kampeni za Zitto zilikuwa zikipangwa na kuratibiwa na baadhi ya viongozi kutoka Jumuiya ya Vijana ya CCM na kwamba
baadhi ya mikutano ya mikakati ilikuwa ikifanyika katika hoteli ya Tamali, Mwenge Dar es Salaam.

Wachunguzi wa mambo wanasema hali hiyo huenda ndiyo ilifanya Zitto atuhumu viongozi wake kuwa wana ukabila akisema wabunge wengi wa Viti Maalum mwaka 2005, walitoka mkoa wa Kilimanjaro.

Akiwa nchini Ujerumani alinukuliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW) akisema Mbowe amekuwa baba wa migogoro na kwamba yeye anataka kurudisha umoja katika chama.

Kama kwamba haitoshi, Zitto alisema kuwa tofauti kubwa iliyopo kati yake na Mbowe ni kuwa yeye ni “mjamaa” na Mbowe ni “bepari.” Alikusudia au hakujua kuwa yote haya yalikuwa yanaongeza ukubwa wa ufa ndani ya chama.

Leo Mbowe anasema, “Yameisha. Mchango wa kila mmoja unahitajika.” Je, hizo ndizo fikra za Zitto pia?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: