Kanuni za FIFA zinaipa haki African Lyon


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) lilikumbwa na changamoto kubwa lilipoibuka sakata la Athumani Idd Chuji alipoamua katikati ya msimu kujitoa Simba na kuhamia klabu ya Yanga.

Mwisho wa sakata lile, TFF ilipata fundisho ikaamua kutengeneza mikataba ya mfano itumike kuwaongoza wachezaji juu ya haki zao za msingi, uhalali wao na sababu zinazoweza kumlazimisha kuomba uhamisho.

Baada ya TFF kulipatia ufumbuzi tatizo la uhamisho wa ndani wa wachezaji ikapiga usingizi. Haikujisumbua kuwa linaweza kuibuka sakata jingine kubwa kama hili la klabu ya African Lyon kulilia malipo ya fidia kwa mauzo ya mshambuliaji Mbwana Samatta.

Suala la uhamisho wenye utata wa Chuji ulipita mabega ya TFF kwa vile shirikisho hilo kwa msimu wa 2007 halikuwa limeingiza kwenye vitabu vyake kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuhusu Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji.

Suala la Chuji lilijadiliwa sana kwa kuzingatia ibara ya 5 na 6 zinazozungumzia usajili na baadaye ibara ya 13, 14, 15, 16 na 17 zinazozungumzia namna ya kuvunja mikataba na madhara yake.

Safari hii African Lyon inawarejesha wadau wote wa soka kwenye darasa la usajili. Klabu hiyo inadai kuwa mchezaji huyo ni mali yake na ndiyo inayostahili kukinga malipo ya Sh. 150m za usajili wake kwa klabu ya TP Mazembe ya DRC.

Maelezo yaliyotolewa wiki iliyopita na Katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah yanatupilia mbali malalamiko ya klabu hiyo. Samatta ni mali ya klabu ya Simba na ndiyo yenye uhalali wa kupewa fedha.

Kitu pekee, ambacho African Lyon inaweza kudai tena ikipewa nguvu na kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuhusu Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji ni kupewa malipo ya fidia kwa mafunzo na elimu kwa mchezaji huyo.

Nyongeza 4 ya kanuni kuhusu Malipo ya Fidia kwa Kulea Vipaji (Training Compensation) inaipa haki klabu yoyote aliyopitia Mbwana Samatta kabla ya kuwa profeshno kupewa fidia.

Ibara ya 1 inasema mafunzo na elimu kwa mchezaji hutolewa katika umri wa kati ya miaka 12 na 23. Malipo ya fidia yatatolewa kwa kuzingatia sheria kwa ujumla hadi umri wa miaka 23 kwa gharama zilizotumika kwa mchezaji, labda tu ikijulikana mchezaji aliacha mafunzo katika umri wa miaka 21.

Ibara ya 2 sehemu ya 1 inasema malipo ya fidia kwa mafunzo yatatolewa (a) kwa mchezaji atakayesajiliwa kwa mara ya kwanza kama profeshno; (b) mchezaji atakapohamishiwa kwenye nchi nyingine hivyo kucheza ligi chini ya shirikisho tofauti na shirikisho la klabu iliyompa mafunzo.

Hata hivyo, kupitia kifungu cha 2 FIFA inaonya kuwa malipo ya fidia kwa mafunzo hayatalipwa kwa (i) kwa klabu yake zamani iliyovunja naye mkataba bila sababu za msingi; (ii) mchezaji akihamishwa kwa kategoria 4; na (iii) kama mchezaji profeshno amerudi kuwa wa ridhaa.

Ibara inayoipa nguvu African Lyon ni ya 3 kutoka Nyongeza Na 435 kuhusu wajibu wa kulipa fidia ya mafunzo. Ibara hiyo inasema (1) mchezaji akisajiliwa tu kwa mara ya kwanza kama profeshno, klabu mpya iliyomsajili itawajibika kulipa fidia ya mafunzo katika muda wa siku 30 kwa kila klabu ambayo mchezaji huyo aliwahi kusajiliwa nayo (kwa kuzingatia historia ya uchezaji wake kwenye paspoti) pamoja na ile iliyochangia mafunzo kuanzia alipokuwa na umri wa miaka 12.

FIFA inasema kiwango cha malipo ya fidia ya mafunzo kitapigiwa hesabu kwa uwiano wa siku ambazo mchezaji amekaa na klabu. Mchezaji profeshno akiuzwa kwenye klabu nyingine profeshno klabu inayostahili fidia itakuwa iliyomfunza kwa mara ya kwanza.

Sehemu ya 3 inasema ikiwa klabu profeshno iliyomnunua itashindwa kuwasiliana na klabu zote zilizowahi kumlea; au ikiwa klabu hizo hazitajulikana katika muda wa miezi 18 tangu mchezaji aliposajiliwa kama profeshno, basi malipo ya fidia yatapelekwa kwenye shirikisho la soka la nchi ambako mchezaji huyo alifunzwa.

Malipo hayo ya fidia yatapaswa kutumika kuendeleza programu za vijana.

Kadhalika Nyongeza Na 5 inazungumzia malipo ya mshikamano. Ibara ya 1 inasema kadri mchezaji huyo atakavyokuwa anasajiliwa na klabu nyingine profeshno kutakuwa na asilimia fulani ya malipo ya mshikamano kwa klabu za zamani.

Kwa hiyo, madai yanayotolewa na baadhi ya wadau akiwemo mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage kuwa African Lyon haistahili kupewa mgawo eti kwa sababu hawakuandikishiana kupeana malipo ya fidia ya mafunzo si ya kikanuni.

Kanuni haizungumzii klabu kuandikishiana mikataba bali mchezaji akiuzwa na huko alikouzwa akaenda kucheza soka ya profeshano, hata klabu iliyompa mafunzo alipokuwa na umri wa miaka 12 (hapa kwetu ni Umitashumta au Umisseta) inastahili malipo ya fidia.

Ndiyo maana FIFA inasema ikiwa klabu zilizowahi kumpa mafunzo mchezaji husika zisipojulikana katika muda wa miezi 18, malipo hayo ya fidia yapelekwe kwenye shirikisho, na hapa TFF, na yatumike katika programu ya kuendeleza za vijana.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: