Katiba inayohitajika, inayokidhi mahitaji ya wananchi


Njelu Kasaka's picture

Na Njelu Kasaka - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

RAIS Jakaya Kikwete ameonyesha njia. Ni kutokana na hatua yake ya kukubaliana na wanaotaka kuwapo kwa Katiba mpya. Amefanya hivyo, siku chache baada ya wasaidizi wake wawili – Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Frederick Werema na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani – kuonyesha wazi kuwa hawataki kuwapo kwa jambo hilo. 

Wala hakuna mashaka kwamba katiba ndiyo sheria mama katika nchi, na kwamba sheria nyingine zote lazima zitokane nayo. Sheria yoyote iliyotungwa ikipingana na kifungu chochote katika katiba, sheria hiyo itakuwa batili na lazima itenguke.

Katiba pia ni mwongozo na kanuni ambazo watu, huandaa na kuandika na kukubaliana kuzifuata na kuheshimu kwa madhumuni ya kufanikisha malengo ya pamoja. 

Kwa maana hiyo, katiba huandaliwa na watu wenyewe ambao wataongozwa na katiba yao. Kwa maelezo hayo, ni wazi kwamba katiba huandaliwa na wananchi wenyewe. 

Ni vigumu kupata katiba nzuri iwapo miongoni mwa waandaaji wa katiba yupo mwenye nguvu kuliko wengine wote ya kukataa jambo bila kuhojiwa. 

Vilevile, ni vigumu kupatikana katiba nzuri iwapo mmoja wapo ana uwezo wa kulazimisha jambo fulani likubaliwe kinyume cha matakwa ya wengine. Na ni vigumu mno kupata katiba nzuri kama mmoja kati ya waandaaji ana uwezo peke yake wa kuteua wajumbe wa kuandaa katiba hiyo.

Katiba nzuri haiandaliwi na wajumbe walioteuliwa na mamlaka moja, bali makundi yanayoshiriki yakishatambuliwa na kujulikana, huteua wawakilishi kwenye kongamano la kuandaa katiba.

Wajumbe wa kongamano au wawakilishi wa makundi huchagua mwenyekiti wao na mara nyingine hula viapo ili waweze kuifanya kazi yao kwa maslahi ya wengi.  Kamwe watawala hawajiandalii katiba wao wenyewe.

Baada ya kongamano kumaliza kazi yake, ndipo huitishwa Baraza au Bunge la Katiba ili kuidhinisha katiba mpya.

Kwa kuangalia mfano wa katiba ya Marekani ambayo inasemekana ndiyo ya zamani kabisa, kongamano la kuandaa katiba ya majimbo 13 yaliyoamua kuungana na kuwa nchi moja, liliitishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1786.  

Hata hivyo, kongamano hilo halikufanyika kwa vile akidi haikutimia.  Mwaka uliofuata 1787 kongamano liliitishwa tena, akidi ilitimia na majadiliano yakaendelea.

Kabla ya majadiliano kuanza, kongamano lilimchagua mwenyekiti wa kuendesha vikao, George Washngton kutoka jimbo la Virginia.  Hapakuwa na mamlaka ya kuteua mwenyekiti.

Kisha ikatengenezwa kanuni za kuendesha mkutano na kuzipitisha kama mwongozo rasmi. Kati ya kanuni hizo ni usiri wa vikao. Jingine, ni uamuzi kufikiwa kwa wingi wa kura za wajumbe. Kongamano la katiba liliendelea na vikao vyake kwa miezi minne na hatimaye wakakubaliana mambo ya msingi ya kuwemo ndani ya katiba.

Kwanza walikubaliana kuunda taifa moja lenye muundo wa shirikisho – serikali kuu na serikali za majimbo. Hapa walikubaliana kuzigeuza nchi moja moja zinazounda shirikisho kuwa majimbo.  

Mambo mengine mawili ya msingi yalikuwa kuunda serikali ya watu – kwamba serikali kuu itapata madaraka yake kutoka kwa watu inaowatawala.

Katika hili serikali kuu ilitengewa maeneo itakayokuwa na mamlaka nayo na serikali za majimbo zilianishwa maeneo yao.  Walifafanua kuwa suala ambalo halikutajwa katika mamlaka ya serikali kuu, litabaki ama mikononi mwa serikali za majimbo au mikononi mwa wananchi wenyewe. 

Pili, walikubaliana juu ya mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mitatu ya dola - Bunge, serikali na Mahakama.

Mambo yote ya kutunga sheria na kutoza kodi yaliwekwa mikononi mwa Bunge huku yale ya kuendesha serikali yaliwekwa katika utawala. Masuala ya yanayohusu haki na kutafsiri sheria, yalikabidhiwa mahakama. 

Ni mahakama pekee iliyopewa uwezo wa kutafsiri sheria na katiba yenyewe na hata kuamua pale inapozuka migogoro kati ya jimbo na jimbo. 

Katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba serikali kuu ina mamlaka na uwezo wa kufanya kazi popote katika shirikisho bila ya kuhitaji kibali cha serikali ya jimbo.

Kongamano lilikamilisha kazi Septemba 1778 baada ya kutoa ufafanuzi wa vipengele mbalimbali; na katiba mpya iliidhinishwa Julai 1788 baada ya majimbo 11 kati ya 13 kuikubali. Kabla ya katiba hiyo kuidhinishwa, rasimu yake ilipelekwa kwenye bunge la kila jimbo.

Kimsingi utungaji wa katiba ni mchakato unaochukua muda mrefu na si kazi ya kulipua; ni kazi ya kutunga katiba si kazi ya mamlaka moja. Ni kazi ya wote kupitia wawakilishi wao wanaowateua. 

Kazi ya kutengeneza katiba inahitaji uangalifu kwa vile inaamua mustakbali wa taifa. 

Jaji Werema anasema katiba kufanyiwa marekebisho ni jambo la kawaida. Anatoa mfano wa katiba ya Marekani iliyofanyiwa marekebisho mara kadhaa. Lakini kuna tofauti kubwa kati ya Marekani na Tanzania.

Wakati katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 imefanyiwa marekebisho 14 katika kipindi cha miaka 34 sawa na wastani wa rekebisho moja kila baada ya miaka 2.4, katiba ya Marekani imefanyiwa marekebisho 27 katika kipindi cha miaka 223. Hiyo ni sawa na wastani wa rekebisho moja kila baada ya miaka 8.3. 

Aidha, katiba ya Marekani ni katiba ya watu na mhimili wa utawala hauruhusiwi kufanya marekebisho kwenye katiba. Pale kunapojitokeza haja ya kurekebisha katiba, pendekezo la kufanya hivyo lazima litoke katika Seneti au Baraza la Wawakilishi na kuungwa mkono na theluthi mbili ya maseneta na theluthi mbili ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. 

Katika nchi kama Tanzania ambako taratibu za uchaguzi zimenyakuliwa na viongozi wa kisiasa ambao kwa sehemu kubwa huamua nani achaguliwe na nani asichaguliwe, kuna idadi kubwa tu ya wabunge ambao walipita kwa nguvu ya viongozi badala ya matakwa ya wananchi. 

Hivyo uhalali wa wabunge wa aina hiyo kuamua jambo kwa niaba ya wananchi ambao kimsingi hawakuwachagua, unakuwa wa kuhojika. 

Viongozi lazima wachaguliwe na wananchi kwa hiari yao ili wapate uhalali wa kuwawakilisha na kuwasemea katika majukwaa mbalimbali kitaifa.

Hata hivyo, umuhimu na uhalali wa Bunge kushughulikia jambo kama hili unabaki palepale. Kwa sasa wananchi wengi wanataka katiba mpya itakayotokana na matakwa yao. 

Swali ni kwamba watatumia njia gani ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kuandika katiba mpya? Uwakilishi wa wananchi katika mjadala wa katiba utachukua nalo ni sula pana.

Je, ni namna gani unaandaa katiba mpya yenye kuzingatia matakwa ya wananchi katika nchi ambamo rais ana madaraka makubwa na ambamo wananchi walio wengi wamefanywa kuamini kuwa kila linalofanywa na serikali, hufanywa kwa maslahi ya wananchi?

Muundo wa serikali ya Tanzania una changamoto nyingi linapokuja suala kama kuandika katiba mpya, katiba ya watu. Katika nchi zenye muundo wa shirikisho kama Marekani na hata iliyokuwa Ujerumani Magharibi, wajumbe wa kuandaa mapendekezo ya katiba, huteuliwa na majimbo.

Wakati Tanzania ni muungano wa nchi mbili – Tanganyika na Zanzibar - kisheria Zanzibar inaweza kuteua wajumbe kwenye mkutano wa katiba, Tanganyika kama nchi haipo na wala haina serikali.  Kilichopo ni Tanzania ambayo inajumuisha na Zanzibar.

Hivyo, chombo cha kuteua wajumbe kutoka Zanzibar kipo na mahali pa wajumbe kwenda kutoa taarifa ya majadiliano papo. Sasa ni chombo gani kitateua wajumbe kutoka Tanzania Bara ambamo Wazanzibari hawatakuwepo?  Wajumbe wakipatikana watatoa taarifa wapi na kupata maelekezo ya nani?

Ni chombo gani kitakachowaunganisha wananchi wa eneo lililokuwa zamani Tanganyika ili kupata wajumbe watakaokaa meza moja na wenzao wa Zanzibar kujadili katiba mpya ya Tanzania?

Wajumbe kwenye mkutano wa katiba kutoka Zanzibar watakuja katika mkutano wa katiba kama Wazanzibari na watakuwepo kwenye mkutano kuona katiba mpya inalinda maslahi ya Zanzibar.

Tanzania Bara mambo si mepesi.  Wananchi wengi wanataka serikali isijitungie katiba yenyewe, bali watu watunge katiba. Hapo ndipo litakapopatikana tatizo la upatikanaji wa wajumbe na chombo cha kupokea maoni na mapendekezo ya kutoka kwa wananchi. 

Kuna mawazo kuwa taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali, zishiriki katika kupendekeza ya katiba mpya. Ni vema. Lakini nani atazitambua taasisi hizo na kuzipa uhalali wa kisheria kushiriki katika mkutano wa kutunga katiba?

Ni rahisi kutaka katiba itokane na watu wenyewe, lakini njia ya kufikia matakwa hayo katika mazingira yaliyopo nchini, ni ngumu. Hata muundo wa Muungano, unaweza kuwa kikwazo kingine katika kuandika katiba tunayoitaka.

Muundo wa muungano uliwanyang’anya Watanganyika uwezo wa kuamua peke yao baadhi ya mambo yanayogusa maisha yao. Katiba ya Tanzania ni miongoni mwa masuala ya muungano yanayohitaji kuungwa mkono na Wazanzibari kabla ya kufanyika. Iwapo Wazanzibari wakikataa, katiba mpya inaweza kukwama. 

Kinacholeta faraja ni wananchi wa pande zote mbili wanakubali kuwa Muungano haujakaa sawa na wanaona si vema kuendelea na hali ilivyo. Wanahitaji mabadiliko ili kuondoa manung’uniko kwa pande zote mbili.

Wananchi wa pande zote mbili wanalalamika kuwa makubaliano ya Muungano yalifikiwa kiujanja ujanja bila kushirikisha wananchi.  Wazanzibari wanakwenda mbele zaidi kudai Zanzibar imemezwa na Tanganyika na wamenyang’anywa madaraka yote, na Muungano umeharibu uchumi wao. 

Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yaliyoleta serikali ya umoja wa kitaifa yamefanya hali kuwa ya kukanganya zaidi. 

Kwa mfano, wakati Tanzania Bara wanaiona kama ni sehemu ya Muungano inayojiondoa kwenye makubaliano hatua kwa hatua, Zanzibar wanaona ni haki yao kutenda wanakifanya sasa.

Kwa kuzingatia kwamba serikali haipaswi kujitungia katiba yenyewe, kwamba kuna ugumu wa kupata wajumbe au taasisi za kuwakilisha upande wa Tanganyika na kwa kuzingatia kwamba Muungano una changamoto zake katika zoezi hili, basi hatua ya kwanza katika harakati za kupata katiba mpya, ni kupeleka wazo hili bungeni. Lipelekwe kama hoja ya serikali au kama hoja binafsi ya mbunge.

Bunge lipitishe azimio au kutunga sheria ya kuruhusu mchakato wa kuandaa katiba mpya, liainishe taasisi za kuteua wajumbe wa kushiriki katika mkutano wa kujadili mapendekezo ya katiba mpya na liweke utaratibu wa jinsi ya ukusanyaji wa maoni utakavyofanyika. 

Kazi nyingine ya Bunge, ni kutaja chombo kitakachopokea maoni na mapendekezo na kuyajadili na liombwe kuweka utaratibu utakaofuatwa kuidhinisha katiba mpya.

Kwa kuzingatia hayo, ni dhahiri mchakato wa kuunda tume ya kukusanya maoni ungesubiri hadi bunge liweke utaratibu utakaotumika katika kuandika katiba mpya.

Kama tume itaundwa na kukusanya maoni toka kwa wananchi ni lazima ieleweke kuwa tume itawasilisha kazi yake kwa rais na rais baada ya kuchambua kilichomo ataawasilisha bungeni.

Tume haiwezi kuwasilisha taarifa yake kwa chombo kingine chochote nje ya mamlaka iliyoiunda. Wala rais hawezi kupeleka mapendekezo yake kwa chombo ambacho hakijapewa uwezo huo na Bunge.

Kwa wale wanaokubaliana na rais kuunda tume wajue wanabariki maoni kuwasilishwa kwa serikali, kuchambuliwa na viongozi wa serikali na kufikishwa bungeni chini ya usimamizi wa serikali. Matokeo ya mwisho siyo lazima yazingatie matakwa yote ya wananchi. 

Kwa upande unaotaka katiba itungwe na wananchi kwa kushirikisha makundi mbalimbali katika jamii na hatimaye kuidhinishwa na kongamano la katiba, hawana budi kulihusisha bunge tangu hatua za mwanzo.

Mwandishi wa makala hii, Njelu Kasaka aliwahi kuwa Mbunge wa Lupa, wilayani Chunya, mkoani Mbeya. Anapatikana kwa simu: 0787 005 871 na imeili: knjelu@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: