Kauli kasumba


editor's picture

Na editor - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TUNAICHUKULIA kauli ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya Misenyi ya kujiapiza kuwa atapambana na watumishi wa halmashauri wasiounga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ni ya bahati mbaya.

Kusikia kauli hiyo mdomoni mwa kiongozi wa aina ya DC ni kitendo cha kusikitisha katika zama hizi ambazo nchi imekuwa chini ya mfumo wa vyama vingi.

Kwani ni lipi muhimu kwa mtumishi wa halmashauri: Kuwajibika kwa mwajiri wake au kujipendekeza kwa CCM?

Njia sahihi ni mtumishi kutumikia wananchi kuliko kushabikia chama kinachoongoza dola. Kwanza, sheria zenyewe za utumishi wa umma haziruhusu mtumishi aliyeko serikali, kujishirikisha katika ushabiki wa chama.

Mtumishi anaweza kuwa mwanachama wa chama cha siasa, lakini hapaswi kuingiza ushabiki kwenye utumishi wa umma.

Ndiyo maana pale inapotokea mtumishi wa umma ametamani kugombea uongozi wa kisiasa, akishateuliwa, kisheria, lazima achukuwe likizo.

Sasa DC Kanali Issa Njiku anatamba ndani ya kikao cha Baraza la Madiwani kuwa kwa vile ameteuliwa kuendelea kuongoza wilaya ya Misenyi, atawashughulikia watumishi wasiopenda CCM.

Tena, DC Njiku anashutumu watumishi wale aliosema wanaonyesha ushabiki wa wazi kwa vyama vya siasa vilivyo tofauti na CCM.

DC Njiku alikoleza kile kilichojionyesha kuwa ni kituko ambacho kilitokana na kauli ya kada mwingine wa CCM na Mbunge wa Nkenge, Asumpta Mshama.

Mshama amefurahia uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa kumteua tena Njiku na sababu ni moja tu – kanali huyo anawashutumu watumishi wasioamini CCM.

Viongozi wote wawili tunaona hawajitambui na kwa hicho wanachokiamini, basi wajue wamepotoka na hawastahili walipo.

Ukweli, wanashabikia siasa za maji taka, zilezile ambazo hata baadhi ya makada wenzao katika CCM, tayari wamezichoka na wengine wanazikimbia.

Isitoshe, wamejiendekeza mno kama vile Tanzania imethibitishiwa kuwa bila ya CCM, haitastawi; na watu wake hawatapiga hatua yoyote ya maendeleo.

Wakati tunawapa pole kwa kushindwa kuangalia alama za nyakati, kwa upande mwingine, tunawapa moyo watumishi wote wa umma wasioshabikia CCM kazini.

Wala hawana haki ya kushabikia chama chochote cha siasa wawapo kazini. Wakifanya hivyo, watakuwa wamejikubalisha kuvaa kasumba kuwa bila ya CCM imara, nchi itayumba.

Wakiwa kazini wanapaswa kutumia muda wa kazi kwa ajili ya kutumikia wananchi na siyo kuwatumikia viongozi wa vyama vya siasa wanavyovipenda.

0
No votes yet