Kenya: Mahakama yafuta uteja


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version

WAKATI nchini Tanzania mjadala wa kupata katiba mpya unazidi kupamba moto, hasa baada ya kupitishwa kwa Sheria ya kuanzishwa kwa mchakato wa namna ya kukusanya maoni, kwa jirani zetu, Kenya wameanza kunusa matunda ya Katiba yao mpya iliyozinduliwa Agosti mwaka jana.

Lakini tusisahau kuwa Katiba ya Kenya ilipatikana kwa maumivu makubwa, baada ya takriban watu 1,500 kupoteza maisha kutokana na ghasia zilizoenea baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa Desemba 2007.

Hivyo katiba ya Kenya inayosemekana kuwa moja ya katiba bora kabisa barani Afrika, haikupatikana kirahisi. Hiyo inadhihirisha usemi wa Kiswahili kwamba ukitaka kuingia peponi, basi ni lazima ufe kwanza.

Isieleweke kuwa nashurutisha kwamba Tanzania tuuane kwanza ndipo katiba ya wananchi ipatikane. Ninachosema ni kwamba kama jirani zetu Kenya, na wanachama wenzetu katika Jumuia ya Afrika Mashariki, hatimaye wamepiga hatua kiasi hicho, kwa nini tusiwapiku?

Kwamba kila mshirika katika mchakato atimize wajibu wake sawasawa, kwa uadilifu na uzalendo hasa wa kitaifa, ili nasi tupate katiba iliyo bora kama ya Kenya. Hapa nasema kila mmoja akitia dhamira vizuri, hatua hii inawezekana kufikiwa bila ya umwagaji wa damu.

Hebu tuone hayo “matunda” yanayopatikana nchini Kenya kutokana na Katiba yao mpya. Linaloanza kujitokeza ingawa kwa polepole ni utawala wa sheria na uwajibikaji wa kiwango cha juu – na hasa katika ule mgawanyiko wa madaraka baina ya mihimili mitatu ya dola – Utawala (tuseme Rais na serikali yake), Bunge na Mahakama.

Kwa mara ya kwanza, Mhimili wa Utawala unaanza kutojisikia vyema dhidi ya hatua zinazochukuliwa na mhimili Mahakama. Kwa maneno mengine katiba mpya haitoi tena mwanya kwa Utawala (Rais) kupuuza maamuzi ya Mahakama au kuiyumbishayumbisha kwa maslahi yake.

Miezi kadha iliyopita (Mei 2011) kulikuwa na uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge, jimbo la Kamukunji, jijini Nairobi.

Siku mbili kabla ya uchaguzi huo, wakati kampeni za vyama zikiendelea na taifa likisubiri kwa shauku kubwa matokeo ya uchaguzi, kutokana na ushindani mkubwa baina ya vyama viwili vikuu – ODM na PNU, ghafla likaja tangazo kwamba uchaguzi umeahirishwa bila ya kutajwa lini ungefanyika tena.

Kutokana na ombi lililowasilishwa na Paul Mwangi, mwanasheria machachari wa Nairobi na ambaye alikuwa mmoja wa wagombea kwa tiketi ya chama kichanga cha National Vision Party (NVP), Mahakama Kuu chini ya Jaji Jeanne Gacheche, iliridhia ombi la kusitishwa uchaguzi kwa maelezo kuwa Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi haikumpa haki ya kuwasilisha fomu yake ya kuomba uteuzi wa kugombea.

Uamuzi huo uliwashtua wengi, hasa wafuasi wa ODM na PNU ambao wagombea wao wote walikuwa na nguvu ya kisiasa kushinda.

Vyama vya ODM na PNU vilianza kulaumiana kwamba vilisababisha yote hayo ili kupata muda zaidi wa kujipanga na kutarajia ushindi.

Jaji Gacheche alisema katika hukumu yake: “Mchakato wa uteuzi ulikiukwa, na hivyo Mahakama lazima itimize wajibu wake ili kuleta utawala wa sheria.”

Namna wanasiasa wa upande wa utawala walivyoipokea hukumu hiyo ilionyesha wazi kutoridhika, na kwamba hakika walikuwa wamesalitiwa. Walikumbuka mazoea ya miaka mingi ya mhimili Mahakama daima kuwa upande wao na kuweza kuuburuza watakavyo.

Uamuzi huo umeweka mtizamo mpya wa kusahaulika kwa enzi za kuielekeza mahakama.

Kwa kulinganisha tu, hapa Tanzania suala la mgombea kukataliwa uteuzi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa sababu mbalimbali limekuwa ni la kawaida na maamuzi ya mwisho ni ya NEC yenyewe hata kama uchaguzi uko siku ya pili yake. Lakini katiba mpya ya Kenya inatoa haki ya mgombea yeyote kusikilizwa na hata ikibidi uchaguzi kuahirishwa ili kuidhihirisha haki pasina kutafuta kisingizio.

Profesa Maria Nzomo, balozi aliyestaafu nchini Kenya, anasema wanasiasa wako nyuma sana kuikubali hali hiyo mpya inayojitokeza ya mhimili mahakama kujitegemea kimaamuzi kwa kuwa chombo hicho muhimu katika kusimamia haki, na hivyo kustawisha amani ya nchi, sasa kimeamua kusimama imara.

Kufuatana na mtazamo wa Prof Nzomo, inaonekana mhimili utawala hauna njia ya kuikabili hali hii. Angalia mfano mwingine ufuatao.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan anayetakiwa kukamatwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) ya The Hague, alitembelea Kenya wakati wa uzinduzi wa Katiba mpya ya Kenya, ingawa anakabiliwa na tatizo hilo.

Lakini sasa, Rais huyo akizuru tena Kenya anaweza kukamatwa kutokana na hukumu ya Mahakama ya Rufaa chini ya Jaji Nicholas Ombija kuhusu shauri lililopelekwa na wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu likitaka al-Bashir akamatwe iwapo ataingia Kenya. Uamuzi wa Jaji Ombija ulilenga kutia mkazo kwa ile hati ya kukamatwa ya ICC.

Hukumu hiyo imewatia kiwewe watawala. Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Moses Wetang’ula amesema ilitolewa kimakosa na hata kusema serikali iko tayari kuipuuza kwa kumualika al-Bashir aje tena Kenya.

Lakini, mwanasheria Paul Mwangi anasema kuja juu huko kwa serikali kunausaliti msimamo wake wenyewe – kwamba mahakama hazina uthubutu kutoa hukumu kama hii, au inaweza kuipuuza tu hukumu bila ya kutokea athari yoyote kwa serikali.

“Kutokana na hasira tu, serikali inaonekana kusahau kwamba ilikuwa ni makosa kumualika al-Bashir kwa sababu ilikiuka sheria za Kenya na zile za mikataba ya kimataifa ambazo Kenya iliafiki na kusaini,” alisema.

Ukweli ni kwamba baada ya miaka mingi ya kuburuzwa na kukandamizwa, mhimili Mahakama sasa umepata msimamo wake imara na hauhitaji tena uteja kwa serikali.

Hukumu ya majaji Gacheche na Ombija ni kati ya kesi nyingi tu hivi karibuni zinazoushangaza mhimili utawala nchini Kenya.

Hukumu hizo ni kati ya zile za majaji wenzao waliojitokeza katika kuiweka Idara ya Mahakama kuheshimiwa kulinganishwa na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita chini ya utawala wa KANU.

Majaji wengine waliopata kutoa hukumu zilizoudhi utawala wa Rais Kibaki ni Jaji Mohammed Warsame, Daniel Musinga na Mohamed Ibrahim.

Kabla ya Katiba mpya, Jaji Mkuu, majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ysa Rufaa, Mwendesha Mashitaka Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walikuwa wanateuliwa na Rais.

Hali hii iliiweka Idara ya Mahakama katika hali ngumu kuweza kutoa hukumu zinazoweza kuiudhi serikali.

Sasa Rais hana mamlaka tena ya uteuzi wa wakuu hao wa kusimamia haki. Mamlaka hayo yanadhibitiwa na Tume ya Idara ya Mahakama, ambayo huteuliwa na Bunge.

0
No votes yet