Kikwete aanguke mara ngapi tujue anaumwa?

IKO kwenye rekodi sasa kwamba Rais Jakaya Kikwete ameanguka zaidi ya mara tatu akiwa jukwaani. Kila alipoanguka zilitolewa sababu tofauti na tukio la awali.
Wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali ndio wanatoa sababu hizo huku wakitoa hofu wananchi kuwa afya ya rais haina mgogoro. Husema afya ya rais ni salama.
Tunashukuru kwa majibu hayo kwamba afya ya rais wetu haina mgogoro. Lakini CCM na serikali, wanataka Rais Kikwete aanguke mara ngapi hadharani ili wajue kwamba afya yake ina mgogoro?
Sote tutaamini hivyo kwamba afya ya rais wetu haina walakini, bali CCM na serikali wanataka Rais Kikwete aanguke mara ngapi hadharani ndipo wajue kuwa anaadhirika?
Maana kama kweli afya yake haina mgogoro ni dhahiri sasa anaadhirika mbele ya wananchi pale anapoanguka hadharani.
Desemba 17, 2005 ilikuwa siku muhimu ya CCM kuhitimisha kampeni zake kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Rais Kikwete alianguka jukwaani dakika chache tu tangu kuanza kuhutubia wananchi kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
Alinyanyuliwa na kukimbizwa moja kwa moja kupata matibabu.
Oktoba 4, 2009 rais alianguka alipokuwa anahutubia waaumini wa Kanisa la Afrika Inland Church (AIC) mjini Mwanza. Alipumzishwa kwa muda na akarudi jukwaani kuendelea na hotuba.
Safari hii tena, tukio kama hilo limetokea. Ni 21 Agosti mwaka huu kwenye viwanja vilevile vya Jangwani. Rais alianguka baada ya dakika 16 hivi kuanza kuhutubia wananchi katika uzinduzi wa kampeni za CCM.
Alipumzishwa kwa dakika 20 na kurudi jukwaani kuendelea na hotuba. Hata hivyo, hali ilipomzidia alilazimika kukatisha hotuba na hatimaye kuondoka na kukimbizwa kupumzika.
Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, akionyesha dhahiri kufadhaika, alisema, “Kaeni, kaeni, Mungu mkubwa.”
Wanafamilia wa rais walionyeshwa wakitokwa machozi na wanachama wa CCM wakaonyesha kukata tamaa.
Watu waliotazama tukio lile moja kwa moja kwenye televisheni, walijionea namna rais alivyokuwa hakujua kilichotokea kwani aliporudi alisikika akisema, “wamenivurugia…”, “karatasi ziko wapi….”
Alikuwa anachakura makaratasi ya hotuba yake aliyokuwa akiisoma. Bila ya shaka karatasi zilipanguka na akawa anajitahidi kuzipanga upya ili aendeleze hotuba yake.
Aliporudi jukwaani, wasaidizi wake walisimama karibu zaidi naye kuliko awali. Baada ya kuweka ‘mambo sawa’ alimudu kuzungumza kwa dakika tano tu, akaondoshwa.
Muda mfupi jioni ile, CCM kupitia kwa mwenyekiti wa kamati yake ya kampeni, Abdulrahman Kinana, ilitoa taarifa isemayo Rais Kikwete ni mzima kwani afya yake ipo salama. Isitoshe, Kinana alisema kesho yake (Jumapili) rais atakuwa Mwanza kuendelea na ratiba ya kampeni. Akiwa mjini Mwanza, mambo mengi ambayo Rais Kikwete angeyazungumza jukwaani, aliyamalizia Katibu wa CCM Mkoa, Rajabu Kundya.
Baada ya Rais Kikwete kupanda jukwaani alitumia dakika chache, akashuka. Lakini wakati umati wa watu unaondoka, alichukua kipaza sauti na kutoa ahadi nyingine ya ujenzi wa barabara aliyodai haimo kwenye ilani.
Tunajua kuwa kete ya ushindi wa CCM ni Rais Kikwete – ndivyo Katibu Mkuu Makamba alivyotumainisha wananchi – na tunajua pia CCM ina wafuasi wengi watakaompigia kura katika hali yoyote ya afya yake.
Lakini CCM na serikali wajue kwamba kwa kuanguka-anguka namna hiyo, Rais anaadhirika. Kitendo cha kiongozi mkuu wa nchi kuanguka-anguka jukwaani bila ya kutarajiwa tena mbele ya wapigakura, kunaelekeza Watanzania kufikiria mara mbili.
Kikwete amevunja rekodi hata ya aliyekuwa Rais wa Cuba, Fidel Castro ambaye katika kipindi cha miaka 45 ya utawala wake, alianguka mara mbili tu. Rais Kikwete ameshaanguka mara tatu hadharani ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.
Sababu za Castro kuanguka ilidaiwa ni umri mkubwa (miaka 78), lakini Kikwete ana umri wa 60 na sababu hazijulikani kwa uwazi.
Oktoba 21, 2004, Castro alianguka wakati anateremka jukwaa baada ya kufungua sherehe za mahafali. Alivunjika mguu wa kushoto na mkono.
Taarifa za kuanguka kwa Castro ziliripotiwa na kituo cha televisheni cha taifa hilo.
Ripoti ya uchunguzi ya madaktari wake ilionyesha kuwa alivunjika goti la kushoto na mkono wa kulia. Castro aliamuru taarifa za tukio hilo zitangazwe kwa wananchi.
Baadaye Rais Castro alizungumza na wananchi wapatao milioni 11.2 wa Cuba kupitia televisheni ya taifa akisema alidhani alivunjika goti “na labda mkono…lakini niko kamili”.
“Naweza kuendelea na kazi. Nitafanya kila liwezekanalo ili nipone haraka, lakini kama mnavyoniona ninaweza kuzungumza,” alisema.
Afya ya Rais Castro ilianza kuzua mjadala na ikasababisha wapinzani wake wa kisiasa wanaoishi Miami, nchini Marekani – raia wengi wa Cuba wanaishi Miami kama wakimbizi – kuishapulia serikali kwamba inaficha taarifa za rais.
Mjadala mkali ulianza mwaka 2001 kutokana na tukio lililosababisha maelfu ya watu kulia baada ya kumwona kamanda wa majeshi akikosa nguvu na kuanguka chini baada ya hotuba ndefu jukwaani. Tukio hilo lilitokea 23 Januari 2001.
Rais Castro aliondolewa na kupewa matibabu, lakini alirudi baadaye kuwahakikishia wananchi kwamba yu mzima wa afya. Kutokana na tukio hilo, mwenyewe alitamka kwamba atakabidhi madaraka kwa mdogo wake, Raul Castro, na ndivyo ilivyokuja kuwa.
Hali hii inanikumbusha tukio la iliyokuwa Umoja wa Kisoviet (USSR), enzi za Katibu Mkuu wa Chama cha Kisoshalisti cha Urusi, Konstantin Ustinovich Chernenko ambaye alichukua hatamu za uongozi baada ya Yuri Andropov kufariki dunia. Chernenko aliongoza Urusi miezi 13 tu kuanzia 13 Februari 1984 hadi 10 Machi 1985 alipofariki dunia akiwa na umri wa miaka 74. yeye pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Urusi.
Chernenko alichaguliwa huku umma ukiwa na hofu kubwa kuhusu afya yake. Haraka alisema anamhitaji Mikhail Gorbachev awe mrithi wake.
Baraza Kuu la USSR halikumuidhinisha Gorbachev kuwa namba mbili, lakini ndiye aliyefanya kazi muda wote.
Alipofariki dunia, akaidhinishwa kushika uongozi wa taifa hilo kubwa lililokuwa likiongoza kundi jingine la kiitikadi duniani dhidi ya Marekani.
Vipi Tanzania? Tunajifunza nini kutokana na matukio ya Castro na Chernenko? Ni kweli hatupaswi kujadili na kujua hali ya afya ya rais wetu? Hivi ni sahihi kwa umma kupewa majibu ya kisiasa katika hali inayomkabili Rais Kikwete?