Kikwete ametelekeza wapambanaji


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi
Rais Jakaya Kikwete

KAMANDA Jakaya Kikwete amesalimu amri? Vita dhidi ya ufisadi imemwelemea? Mbona hatekelezi ahadi zake za kupambana na ufisadi? Turejee kauli zake.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mjini Dodoma mwishoni mwa mwaka jana, Rais Kikwete alisema, “…Ni lazima mafisadi washughulikiwe.”

Alitoa hata wito kwa wananchi wanaowafahamu watuhumiwa, “wasaidie kuwataja.” Alisema serikali anayoiongoza itapambana na kila atakayejihusisha na vitendo vya ufisadi, “hata kama mhusika ni mwanachama wa CCM.”

Kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Rais Kikwete alitoa kauli kama hiyo. Alisema, “kamwe serikali haitakuwa na urafiki na watuhumiwa wa ufisadi.”

Katika kilele cha siku ya wafanyakazi duniani, Mei mosi, zilizofanyika Mbeya, mwaka 2006, Kikwete aliwataka wafanyakazi washiriki katika vita hivi na kutaka wafanyakazi wataje wale wanaowatuhumu.

Mwaka 2007 Rais Kikwete aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari, Ikulu, Dar es Salaam, “Msinione natabasamu, lakini I am serious (niko makini).” Alisema pia kuwa hana ubia na yeyote katika urais wake ispokuwa Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye alikuwa mgombea mwenza wake.

Hakika, kuna msululu wa ahadi za rais juu ya mapambano dhidi ya ufisadi na kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Kuna wakati rais alitoa ahadi ya kupambana na waagizaji wakubwa wa madawa ya kulevya nchini. Alisema wote wanaoingiza madawa hayo, anawafahamu kwa majina.

Lakini bado mamia kwa maelfu ya vijana wameendelea kuteketea. Hakuna hata kigogo mmoja anayejihusisha na biashara hiyo aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani.

Kuna wanaodai kuwa watendaji serikalini wameshindwa kuwachukulia hatua waingizaji hawa, kutokana na hofu ya kauli ya rais kwamba “majina ya waingizaji ninayo.”

Kikwete aliwahi kusema pia kuwa anawafahamu watuhumiwa wa rushwa, tena kwa majina. Alitoa wito wajirekebishe, kabla hajawachukulia hatua.

Hata wafanyabiashara wanaoshirikiana na watumishi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), hatimaye kukwepa kodi, rais alisema anawafahamu.

Lakini mpaka sasa, hakuna kikubwa kilichofanyika, wala hawezi kutokea kiongozi na kudai kuwa hatua dhidi ya wahusika zimechukuliwa lakini hazijatangazwa.

Inaonekana hata wasaidizi wake wa karibu hawataki kumkumbusha rais ahadi ambazo hajatekeleza. Au wameng’amua kuwa kinachotamkwa na bosi wao, “sicho kinachotakiwa kutekelezwa na serikali?”

Wamemwacha Kikwete akitembea na “zigo la ahadi” kwa wananchi. Kasahau, kachoka kaemewa?

Wiki iliyopita, Kikwete aliongoza uzito mpya kwenye ahadi zake. Alitaka apatiwe orodha ya watuhumiwa wa ufisadi katika zabuni ya ujenzi wa barabara. Sasa kuna watakaosema kuwa kauli za Kikwete zimekuwa “mchezo wa karata tatu.”

Wachangaji karata wanajitahidi kuaminisha wachezaji kuwa watashinda, lakini wao wanajua kuwa hakuna ushindi. Matokeo yake ni kwamba wachezaji na wachezeshaji hawawezi kumaliza mchezo bila zogo.

Sasa zahama zinawaangukia wale ambao wamesimama na kuonyesha kuwa wanapambana na ufisadi. Kikwete hajaonyesha kusimama nao kwa dhati, kwa hiyo mara nyingine wanadhalilishwa hata mbele yake.

Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta, ambaye amekuwa thabiti na bila kuchekea ufisadi, hana tena mahusiano mazuri na viongozi serikalini na hata baadhi ya wabunge.

Tayari kuna taarifa za uhakika, kwamba amesukiwa zengwe katika jimbo lake la uchaguzi, Urambo Mashariki, ili kuhakikisha anashindwa kurudi bungeni.

Zipo pia taarifa kuwa Sitta aliwahi kushambuliwa hadharani na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamisi Mgeja mbele ya Kikwete katika moja ya vikao vya Halmashauri Kuu (NEC).

Mgeja alimkoromea Sitta kuwa msimamo wake wa kupambana na ufisadi unakipasua chama chao. Kikwete hakuchukua hatua ya kumkemea au kumpoza Mgeja. Alikaa kimya.

Kikwete ameshindwa mpaka sasa  kutekeleza maagizo ya Bunge ya kuwajibisha watumishi wa serikali waliotajwa kuhusika katika kashfa ya mkataba wa Richmond.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, ambaye ni moja wa waliotajwa, bado amekalia ofisi ya umma. Kichekesho ni kwamba kwa nafasi yake, Mwanyika anafanya kazi na wabunge walewale waliomtaka Kikwete amwajibishe!

Mwanyika bado anafanya kazi na Spika Sitta, ambaye yeye na Bunge lake, bado wanaamini kuwa Mwanyika amekosa uadilifu na ameshindwa kuwajibika ipasavyo.

Katika mazingira hayo, Kikwete anamweka Spika katika mazingira magumu ya kushambuliwa na kudhalilishwa.

Rais Kikwete ameshindwa pia kumwajibisha Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea. Yote hii bado ni dharau kwa Bunge na Spika wake.

Hatua ya Kikwete ya kushindwa kutekeleza maamuzi ya Bunge, inakipunguzia chombo hiki cha wananchi heshima na hata uhalali.

Kwa mpangilio huohuo, Rais Kikwete amekataa au ameshindwa hata kumuunga mkono mfanyabiashara, Reginald Mengi, ambaye hivi karibuni alithubutu kutaja hadharani orodha ya watuhumiwa watano wa ufisadi, akiwaita “mafisadi papa.”

Badala ya kupongezwa, sasa kuna taarifa za kumsakama Mengi kutoka dola lilelile analoongoza Kikwete. Mawaziri wawili wa Kikwete wametoa kauli za kumpinga Mengi na kutetea watuhumiwa kama vile wamekodishwa na wahusika.

Waziri wa Utawala Bora, Sophia Simba na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika wamempinga Mengi hadharani. Mkuchika na Sophia hawataki kusikia kauli ya Mengi.

Mwingine ambaye amekuwa akipambana na ufisadi, lakini Kikwete ameshindwa kumtetea, ni Nape Nnauye, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UV-CCM).

Ni Nape aliyesakamwa baada ya kushupalia mkataba wa Lowassa wa kitega uchumi cha UV-CCM.

Hata pale ambapo wajumbe wote wa Baraza la Wadhamini la UV-CCM, kukana mkataba wa Lowassa na baadaye Kamati Kuu (CC) kuridhika kwamba mkataba haukufuata taratibu, bado Kikwete ameshindwa kumlinda Nape.

Ni kimya cha Kikwete kilichowapa wapinzani wa Nape fursa ya kumsulubu hadi kumfukuza uanachama wake na Kikwete hajachukua hatua za haraka kulinda haki za Nape.

Kuna huyu Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Kyera na Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza Richmond.

Kikwete anajua kuwa uhusiano wa Mwakyembe na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile ni mbaya; jambo ambalo rais angeweza kurekebisha ili kulinda mashujaa wake. Mwakipesile alikuwa mbunge wa Kyela kabla ya Mwakyembe.

Orodha ya wanaosakamwa ni ndefu. Bali ukimya huu unaangamiza mashujaa ambao Kikwete angesimama nao na kukubalika mbele ya jamii. Kwa nini anataka kuwapoteza, ni swali analoweza kujibu yeye mwenyewe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: