Kikwete amtema rasmi Lowassa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 June 2010

Printer-friendly version
Amwandaa Karume kumrithi 2015
Dk. Shein ‘kupewa’ urais Zanzibar
Lengo ni kumaliza makundi, fitina
Rais Jakaya Kikwete na Rais Amani Karume

RAIS Jakaya Kikwete na Rais Amani Abeid Karume watakabidhiana urais wa Jamhuri ya Muungano mwaka 2015, taarifa zimeeleza.

Taarifa zilizoenea Dar es Salaam na mjini Zanzibar zinasema mwaka huu, Rais Karume ndiye atateuliwa kuwa mgombea mwenza wa Kikwete ili kuhakikisha rais wa Muungano ajaye anatoka Zanzibar.

Kwa hatua hiyo, ndoto za Edward Lowassa, waziri mkuu aliyelazimshwa kujiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, za kujisafisha na kuwa rais baada ya Kikwete, zitakuwa zimezimwa.

Aidha, ndoto za Dk. Mohammed Gharib Billali kuwa rais wa Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu, zitakuwa zimeyeyuka pia, kwani anayeandaliwa kwa nafasi hiyo ni makamu wa rais wa sasa wa Muungano, Dk. Ali Mohammed Shein.

Taarifa zinasema kwa mpangilio huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakuwa kimeondokana na ushindani wa “niue-nikuue” na makundi ambayo yanakaribia kukisambaratisha.

“Kuna hili la Shein kupitishwa na hilo likimalizika, tunataka Rais Kikwete amteue Karume kuwa mgombea mwenza. Hapa kila kitu kitakuwa kimefikia tamati na umoja na mshikamano ndani ya chama utakuwa umeimarika,” ameeleza mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu katika serikali na CCM.

“Mkakati wa kumpitisha Dk. Shein umelenga pia kumuinua Karume. Huyu ndiye tunayetaka awe mgombea mwenza wa Kikwete, lengo likiwa kumjenga kwa ajili ya 2015,” kimeeleza chanzo cha taarifa.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, mkakati umewekwa kuhakikisha jina la Dk. Shein ndilo pekee linalofikishwa katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kwa ajili ya kupigiwa kura.

Kiongozi mmoja wa serikali aliye karibu na mpango wa kutaka Shein kuwa mgombea pekee, ameliambia MwanaHALISI kwamba tayari mikakati yote imekamilika.

“Mambo yote yanakwenda kama yalivyopangwa. Tunataka Dk. Shein ndiye pekee aingie katika kinyang’anyiro cha urais Zanzibar. Hili litasaidia kuondoa makundi na kumaliza fitina za kisiasa visiwani,” amesema akimnukuu kiongozi mmoja wa serikali na CCM.

Alisema kwamba ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa, “Mkakati unasukwa wa kuhakikisha jina la Dk. Shein ndilo linakuwa jina pekee linalofikishwa NEC kwa ajili ya kupigiwa kura.”

“Hili la Shein likimalizika, tunataka Rais Kikwete amteue Karume kuwa mgombea mwenza. Hapa kila kitu kitakuwa kimefikia tamati na umoja na mshikamano ndani ya chama utakuwa umeimarika,” alisema.

Habari zinasema lengo la kumuibua Karume kutoka Zanzibar na kumleta Bara ni kutaka kumrithisha urais wa Muungano, baada ya Kikwete kumaliza kipindi chake cha urais.

Habari zinasema mchakati huo utaepusha kile kinachoitwa, “misuguano ya urais 2015” kutoka kwa wanasiasa wa Bara.

Wanasiasa kadhaa, akiwamo Lowassa, waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye na waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, wanatajwa kutaka kumrithi Kikwete.

Mwingine anayetajwa na ambaye amekuwa akitajwa sana kuwa mwiba kwa kambi ya Lowassa na swahiba wake mkuu, Rostam Aziz, ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.

Urais wa 2015 ndio unaotajwa kuwa kiini cha msuguano ndani ya bunge na katika chama ambapo Lowassa na mshirika wake, Rostam wanatajwa kujenga ngome ya kuwatetea kwa gharama yoyete ile.

Katika mchakato huu, mwanasiasa mmoja mwanammke ambaye ametangaza kugombea ubunge katika jimbo moja la Kanda ya Ziwa Victoria, ndiye anatajwa kuandaliwa nafasi ya waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya siasa wanasema mkakati wa kumfanya Shein kuwa mgombea urais wa Zanzibar, utakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wapambe wa Dk. Billali.

Taarifa zinaeleza, miongoni mwa sababu zitakazotumika kumwengua Dk. Billali ni pamoja na uamuzi wake wa kugombea urais Zanzibar mwaka 2005 kupingana na rais aliyepo madarakani.

“Unajua yule bwana alikosa subira. Chama chetu kimeweka utaratibu wa rais aliyepo kuachiwa kumaliza vipindi vyake viwili kwa mujibu wa katiba. Lakini yeye katikati ya shughuli alikuja kuanua majanvi na kumwaga ubwabwa,” kimeeleza chanzo cha taarifa.

Amesema, mbali na tuhuma za kuchukua fomu kumpinga Karume, Dk. Billali anakabiliwa na tuhuma nyingine ya “kuhujumu chama” siku chache kabla ya uchaguzi kutokana na hatua yake ya kumtuhumu Karume kuendesha nchi kifamilia.

Vilevile Dk. Billali anadaiwa kubeba watu waliowahi kuonywa na Kamati Kuu (CC) kuvuruga chama; kuleta mpasuko katika chama na kumdhalilisha rais wa Jamhuri.

Wanaotajwa kubebwa na Dk. Billali na ambao waliwahi kuonywa na CC, ni pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), Zahoro Mohammed na mwanachama wa Zanzibar, Mohammed Hija.

Tayari Rais Kikwete amechukua fomu za kugombea urais wa Muungano na mjini Zanzibar, juzi Jumatatu, Dk. Shein alichukua fomu za kugombea urais ikiwa ni hatua moja katika kufanikisha mchakato unaoripotiwa.

Hadi Jumatatu ni Jakaya Kikwete pekee aliyekuwa amechukua fomu ya kugombea urais kupitia CCM kwa upande wa Tanzania Bara.

Mbali na Dk. Shein, waliochukua fomu kugombea urais Zanzibar ni pamoja na Billali, Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna, Naibu Waziri Afrika Mashariki Mohamed Abood, mdogo wake rais wa Zanzibar, Balozi Ali Karume na Kamishna wa wizara ya elimu na utamnadiuni, Hamza Bakari Mshindo.

Mohammed Seif Khatib, waziri katika ofisi ya waziri mkuu (Muungano), jana alitarajiwa kutoa msimamo wake iwapo atagombea urais Zanzibar.

Hata hivyo, mchakato huu wa kuandaa viongozi una dalili za kukumbana na upinzani mkali ndani ya vikao vya CCM kutokana na kuwepo mikakati ya awali kuwania uongozi miongoni mwa viongozi mbalimbali.

Kwa mchakato huu, wawaniaji urais waliokuwa wakitajwa, akina Lowassa, Sumaye, Mwandosya na Membe hawana upenyo labda kwa njia ya upinzani.

0
Your rating: None Average: 3.6 (15 votes)
Soma zaidi kuhusu: