Kikwete asaliti wabunge CCM


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 01 February 2012

Printer-friendly version

MSIMAMO wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu marekebisho ya sheria ya katiba sasa uko njiapanda, imefahamika jijini Dar es Salaam.

Kile walichopigania “kufa na kupona” hadi kuzusha shari bungeni, ndicho wanatakiwa kufuta na badala yake kuridhia mapendekezo ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Taarifa kutoka Dodoma zinasema, tayari serikali iko mbioni kuwasilisha bungeni marekebisho makubwa ya sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011, kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete amekubaliana na viongozi wa CHADEMA.

MwanaHALISI limeelezwa na vyanzo vyake ndani ya serikali kuwa, miongoni mwa mabadiliko ambayo serikali itawasilisha kwenye Mkutano wa Sita wa bunge ulioanza jana mjini Dodoma, kuhusu mswaada huo, ni uteuzi wa wajumbe wa tume ya kukusanya maoni.

Kupelekwa kwa mabadiliko hayo, miezi miwili baada ya sheria kupitishwa na kabla ya kuanza kutumika, kumetokana na hoja nzito zilizowasilishwa na ujumbe wa CHADEMA kwenye mkutano wake na Rais Kikwete, ikulu jijini Dar es Salaam, wiki mbili zilizopita.

Mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi wa CHADEMA, ulifuatia hatua ya wabunge wa chama hicho kutoka bungeni, 14 Novemba 2011, kupinga kile walichoita, “kuburuzwa na serikali katika mchakato wa katiba mpya.”

CHADEMA kilisema hatua ya rais kuteua wajumbe wa tume ya katiba, kutasababisha kupatikana kwa katiba ambayo haitakidhi matakwa ya wananchi kwa kuwa wajumbe wake watawajibika moja kwa moja kwa rais. Wabunge wa CCM walipinga hoja hiyo.

Habari kutoka Dodoma zinaeleza kuwa wabunge wa CCM walijulishwa kuwapo kwa mabadiliko katika mkutano wao Jumapili iliyopita. Hii ilikuwa siku moja kabla kamati za kitaalam za serikali na CHADEMA kukutana na kufikia makubaliano yaliyosababisha marekebisho yatakayowasilishwa.

Taarifa zinasema tayari baadhi ya wabunge wa CCM wameanza kulalamikia hatua ya serikali kuafikiana na CHADEMA kwa madai kuwa watatoa ujiko kwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Imeelezwa kuwa malalamiko ya wabunge hao, yametokana na hatua yao, wakati wa kuchangia mjadala wa sheria ya katiba Novemba mwaka jana, ya kuwazomea, kuwatukana na kuwabeza wabunge wa CHADEMA; wakiwatuhumu kutumiwa na mabeberu.

Vyanzo vya ndani ya mkutano vinasema baadhi ya wabunge wa CCM walilipwa na chama chao kiasi cha Sh. 1 milioni kuvamia majimbo ya upinzani ili kueleza wananchi kile walichoita “ubora wa sheria” ambayo hivi sasa inakwenda kufanyiwa marekebisho makubwa kabla ya kutumika.

“Katika hili, CHADEMA wameshinda. Hawa watu wametoka bungeni. Rais akaenda kuwashitaki kwa wazee wa Dar es Salaam. Lakini CHADEMA wakaomba kukutana na rais; wakakubaliwa. Wakajenga hoja zao na rais akawasikiliza. Leo hii, serikali inakubali mapendekezo yao…Hii inaonyesha kuwa walichokuwa wakikipigania kilikuwa sahihi,” ameeleza waziri mmoja katika serikali ya Rais Kikwete.

Katika mabadiliko ya sasa yaliyopewa jina la “Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, Na. 8 ya mwaka 2012,” serikali imeridhia vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyama vya kitaaluma na asasi za kidini, kuteua wajumbe wa kuingia kwenye kamati ya katiba.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati ya wataalamu wa serikali na CHADEMA, kilichofanyika juzi Jumatatu mjini Dodoma, sasa serikali imekubali kufanya mabadiliko katika kifungu cha 6 (1) cha sheria hiyo kwa kuondoa mamlaka ya uteuzi moja kwa moja kwa rais.

Kifungu cha 6 (1) cha sheria sasa kinasema rais atateua wajumbe kutoka miongoni mwa majina atakayopelekewa na vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na vyama vya kitaaluma, kuwa wajumbe wa Tume ya Katiba.

Aidha, serikali imekubali matakwa ya CHADEMA ya kuongeza kifungu cha 17 (10) kinachoruhusu watu binafsi, taasisi za kidini na vyama vya hiari, kutoa elimu ya uraia. Asasi hizo zitakuwa sasa zinaripoti kwa mkurugenzi wa halmashauri badala ya mkuu wa wilaya.

Vilevile, serikali imekubali kufutwa kwa kifungu cha 6 (5) (c) katika  muswada ambacho kilikuwa kinawaondolea sifa ya kuwa wajumbe wa tume, watu waliowahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa au ni mtuhumiwa katika shauri lililoko mahakamani linalohusu shitaka la kukosa uaminifu au maadili.

Kufutwa kwa kifungu hicho, kama ambavyo CHADEMA ilikuwa imesimamia katika hoja zake za awali, kumetoa mwanya kwa raia wa Jamhuri kushiriki, bila kizuizi chochote, katika mchakato wa katiba isipokuwa kama mtu huyo ni mbunge, mjumbe baraza la wawakilishi au mtumishi katika vyombo vya usalama.

Ibara nyingine ambayo inatarajiwa kufanyiwa marekebisho kwa mujibu wa makubaliano kati ya Rais Kikwete na CHADEMA, ni 6 (5) (a) ambako madiwani au viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote waliokuwa wamezuiwa kuwa wajumbe wa tume, sasa wanaruhusiwa.

Jingine ambalo CHADEMA walitaka kuingizwa katika marekebisho na ambacho kimekubaliwa na serikali, ni kuhusu kamati ya nidhamu ya tume ya katiba.

Habari zinasema awali sheria ya mabadiliko ya katiba ilikuwa kimya kuhusu kuwepo kamati ya nidhamu, lakini sasa kimeongezwa kifungu kinachoruhusu kuundwa kwake.

Kamati ya nidhamu, kwa mujibu wa mabadiliko hayo, itaongozwa na mtu mwenye hadhi ya jaji wa mahakama ya rufaa, akishirikiana na wajumbe wanne kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS).

Chini ya mabadiliko hayo, sheria inaelekeza kamati ya nidhamu kufanya uchunguzi mara moja, pale itakapopokea malalamiko au kubaini kuwapo kwa kasoro za uvunjifu wa uaminifu miongoni mwa wajumbe wa tume ya katiba.

Pale ambapo ushahidi utapatikana juu ya malalamiko dhidi ya mjumbe husika, basi ataondolewa kwenye nafasi yake.

“Hata katibu wa tume ya katiba ataweza kuondolewa kwa kutumia mamlaka ya nidhamu ya tume yenyewe, tofauti na ilivyokuwa kwenye muswada wa awali uliokuwa unatoa mamlaka hayo kwa rais,” ameeleza mmoja wa wajumbe wa kamati ya wataalamu ya serikali.

“Haya ndiyo maelekezo ambayo rais ametupa. Nasi kama serikali tumetekeleza kama rais alivyoelekeza,” ameeleza.

Jingine ambalo limeguswa katika marekebisho haya, ni kupunguzwa kwa adhabu kwa wale ambao watapatikana na hatia ya kutenda jinai inayotamkwa katika sheria hii. Awali adhabu iliyotajwa ilikuwa kifungo cha miaka mitatu hadi saba au faini ya kati ya Sh. 5 milioni na Sh. 15 milioni.

Mabadiliko ya sasa yatapunguza adhabu na kuwa faini ya kati ya Sh. 3 milioni na 5 milioni au kifungo cha kati ya mwaka mmoja na mitatu.

Mtoa taarifa wa gazeti hili anasema hatua ya Rais Kikwete kuridhia mapendekezo ya CHADEMA kulitokana na hoja thabiti zilizowasilishwa kwake na kamati ya wataalamu wa chama hicho.

“Nakuambia, wale jamaa walikuja mbele ya rais wakiwa na hoja nzito. Walichambua kila kifungu cha muswada na kueleza athari zake kwa taifa na rais aliwasilikiliza na kuwakubalia,” ameeleza mtoa taarifa ndani ya serikali ambaye alikuwapo kwenye mkutano kati rais na viongozi wa CHADEMA.

Kamati ya wataalam iliyojadili mapendekezo ambayo rais alikubaliana na CHADEMA ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Serikali (CPD) Casmir Kyuki kutoka CCM.

Kwa upande wa CHADEMA walikuwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo John Mnyika.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: