Kikwete asiturudishe nyuma


editor's picture

Na editor - Imechapwa 19 May 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MWAKA 2006, nchi wahisani zilitishia kuipunguzia Tanzania misaada kwa maelezo kwamba ilikuwa haijafanya juhudi za kutosha katika kurekebisha sheria ya kukomesha rushwa.

Baada ya tishio hilo, serikali ilifanya harakaharaka kurekebisha sheria hiyo na kuunda chombo kipya kiitwacho Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) badala ya Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takuru).

Mwaka huohuo, mahakama kuu ilitangaza wazi takrima ni rushwa. Halafu, mwezi uliopita, kwa mbwembwe nyingi, Rais Jakaya Kikwete alitia saini Sheria ya Matumizi ya Gharama za Uchaguzi.

Baada ya tukio hilo, vyama vya siasa vilianza kupanga mikakati ya kupata fedha kwa ajili ya kugharamia uchaguzi na kutangaza wazi. Mathalani, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilizindua mkakati wa kukusanya Sh. 50 bilioni kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (SMS).

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilifanya uzinduzi kama huo mwaka jana.

Lakini, katika hali inayoonyesha serikali ya CCM inaangalia namna itakavyotumia mwanya kukwepa kubanwa na sheria iliyoridhiwa na wabunge na mahakama, rais amelirudisha nyuma taifa kwa kusema “takrima haikwepeki.”

Kitendo chake cha kudai hata Chadema au Chama cha Wananchi (CUF) au NCCR-Mageuzi navyo hutoa takrima wanapokutana na wazee, hakiwezi kuwa kigezo cha kukwepa utekelezaji wa sheria ya kupiga vitaaina zote za rushwa, ikiwemo takrima.

Hapa rais anathibitisha kushindwa au anataka kudhoofisha kampeni dhidi ya rushwa.

Kwa hivyo, yapasa ifahamike kwamba hata anapoandaliwa mikutano yake katika maeneo mbalimbali, wananchi waliohudhuria huwa wamepewa “kitochi?”

Rais anataka tuelewe kuwa wazee hawafiki kwenye mikutano kuwasikiliza wagombea mpaka kitochi? Na kwa hivyo tusichukulie kuwa hiyo ni rushwa?

Kama huo ndio mtazamo wa rais kuhusu takrima, si ina maana amewaambia Takukuru wasihangaike kuwafuatilia wagombea wanaotoa takrima kwa vile bila hivyo mikutano itadoda?

Kama hivyo ndivyo, serikali itakuwa na ubavu gani kuzuia takrima anayopewa wapigakura kwa njia ya kupewa usafiri; baiskeli, pikipiki, pesa kwa ajili ya nauli, chai na chakula? Maana bila hivyo si wazee hawatafika sehemu ya mkutano?

Rais anapothubutu kukiri hadharani kuwa ni vigumu kupambana na rushwa kupitia takrima, ajue pia kwamba vyombo vya dola havitaorodhesha takrima katika mikakati yao kuwa ni rushwa.

Tunasema hivi moja kwa moja kwa sababu siku hizi imekuwa mtindo vyombo vya dola kufanya kazi kwa kusikiliza zaidi maagizo ya wateuzi wao badala ya kuzingatia katiba na sheria zinavyosema.

Ndiyo maana sisi tunathubutu kusema, katika hili rais asiturudishe nyuma.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: