Kikwete atikisa Bunge


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version

USHABIKI wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa umewaponza.

Watalazimika kufanya kilekile walichokuwa wakipinga kwa kejeli, matusi na hata maapizo.

Leo hii, wataingia bungeni. Watasomewa Marekebisho ya Sheria ya Katiba ya mwaka 2011; watayajadili na kuyapitisha.

Hatua ya leo inafuatia Rais Jakaya Kikwete kukaza msuli kwamba mapendekezo ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) juu ya sheria hii yana mantiki na sharti yapitishwe.

Kwa wiki nzima sasa, wabunge wa CCM wamekuwa wakijiapiza kuwa hawatapitisha marekebisho ya sheria husika kwa kuwa waliipitisha kwa kejeli nyingi kwa upinzani huku wengine wakijiapiza “hatutakula matapishi yetu.”

“Ukweli ni kwamba wabunge CCM sasa wamenywea. Watafanya kama Rais anavyotaka,” ameeleza mbunge wa upinzani.

Vyanzo vya taarifa vya MwanaHALISI vinasema Rais Kikwete hakuonyesha kutetereka pale alipokutana na kamati ya wabunge watano mjini Dodoma juzi, Jumatatu.

Tangu wiki mbili zilizopita, rais alipokutana na viongozi wa CHADEMA na kukubaliana nao juu ya marekebisho muhimu katika sheria ya katiba, kumekuwa na fukuto ndani ya CCM kwamba rais amewadhalilisha “wabunge wake.”

Kutokana na msimamo huo wa rais, wabunge wamegawanyika katika makundi matatu.

Kundi la kwanza linataka muswada uchomolewe baadhi ya vifungu; kundi la pili linataka uondolewe kabisa na kundi la tatu linataka upitishwe pamoja na marekebisho yanayopendekezwa.

Muswada wa marekebisho ya katiba ulipitishwa Novemba mwaka jana, kwa  kasi, bila kujadiliwa kwa kina na bila kutoa fursa kwa wananchi kuuona katika lugha ya Kiswahili, kuusoma na kuutolea maoni.

Sauti za upinzani kwa baadhi ya vifungu zilizimwa kwa jazba, kejeli na hata matusi ya moja kwa moja kisiasa.

Baada ya muswada kupitishwa, baadhi ya wabunge, wakiwemo mawaziri, waliwezeshwa kwenda majimbo mbalimbali kueleza kile walichoita uzuri wa muswada uliopitishwa.

Lakini upepo umegeuka baada ya Rais  Kikwete, aliyesaini sheria hiyo kukubaliana na CHADEMA juu ya marekebisho muhimu.

Kurejeshwa kwa sheria bungeni hata kabla haijaanza kutumika, kumethibitisha umuhimu wa kusoma muswada ule kwa mara ya kwanza na kuacha nafasi kwa wananchi kujadili, kama CHADEMA na asasi nyingine za kidemokrasia zilivyokuwa zikipendekeza.

Vyanzo vya taarifa ndani ya Bunge, CCM na serikali vinasema wabunge wengi wa chama hicho hawajaweza kuusoma muswada huo.

“Karibu asilimia 50 ya wabunge wa CCM, hata muswada wenyewe hawajausoma. Ukiwauliza kwa nini wanapinga marekebisho haya, tueleze athari zake, hawana majibu,” ameeleza mmoja wa mawaziri serikalini.

Anasema, “Badala yake, utawasikia wakisema, ‘unajua rais ametudharau sisi na kuwasilikiza CHADEMA,’” anaeleza waziri huyo.

Katika mabadiliko ya sasa yaliyopewa jina la “Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, Na. 8 ya mwaka 2012,” serikali imeridhia vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyama vya kitaaluma na asasi za kidini, kuteua wajumbe wa kuingia kwenye Tume ya katiba.

Sasa serikali imekubali kufanya mabadiliko katika kifungu cha 6 (1) cha sheria hiyo kwa kuondoa mamlaka ya uteuzi moja kwa moja kwa rais.

Miongoni mwa mabadiliko ni yale ya kifungu cha 6 (1) cha sheria. Sasa kinasema rais atateua wajumbe kutoka miongoni mwa majina atakayopelekewa na vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na vyama vya kitaaluma, kuwa wajumbe wa Tume ya Katiba.

Serikali imekubali pia kuongeza kifungu cha 17 (10) kinachoruhusu watu binafsi, taasisi za kidini na vyama vya hiari, kutoa elimu ya uraia. Asasi hizo zitakuwa sasa zinaripoti kwa mkurugenzi wa halmashauri badala ya mkuu wa wilaya.

Wabunge wa CCM walikuwa waking’ang’ania kuwa mkuu wa wilaya ndiye awe msimamizi wa zoezi. Inatarajiwa wabunge wengi watajikita hapo katika mjadala wa leo.

“Ni kweli kwamba wabunge tayari wamegawanyika. Lakini hapa tulipofika, sharti marekebisho hayo yaje na kupitishwa kama yalivyo ili kulinda hadhi ya chama, serikali na rais,” ameeleza waziri.

Hasira kuu ya wabunge inatajwa kutokana na ikulu kukana kuidhinisha posho mpya za wabunge, huku baadhi ya wanasiasa wakitaka kutumia mgogoro huo kulipizia kisasi.

Kwa mfano, taarifa zinasema, Beatrice Shelukindo ambaye tayari amejitambulisha mapema kuwa ni kutoka kundi la Lowassa, ndiye aliyetoa hoja ya kupigakura ya kutokuwa na imani na Kikwete bungeni. Hajakana.

Lowassa, mmoja wa maswahiba wa zamani wa Kikwete tayari ameanza kumhusisha na  tuhuma za ufisadi katika uzalishaji umeme wa dharura chini ya mkataba wa kampuni tata ya Richmond/Dowans.

Lowassa aliuambia mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM mjini Dodoma, Novemba mwaka jana kuwa kila alichofanya, katika tuhuma za ufisadi kuhusu Richmond na Dowans, alikuwa ama akitumwa au akimweleza rais Kikwete.

Rais kikwete alikataa kujibu tuhuma hizo hadharani. Lakini wachunguzi wa mambo ya siasa nchini wanasema tuhuma hizo zililenga kumkwaruza Kikwete na kumwondolea ujasiri.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa wabunge wa CCM hawana ubavu wa kupambana na rais. Wengi wako hoi kifedha.

Taarifa zinasema wengi wao, tayari wamechukua mikopo ambayo imeguguna hata pensheni zao, miaka minne kabla ya mwisho wa uwakilishi wao.

“Katika mazingira haya hawawezi kuwa na hoja ya kumwondoa rais madarakani. Wanapwaya. Wamejiingiza kubaya,” ameeleza waziri huyo.

Mapungufu makubwa katika sheria hii yametokana na udhaifu wa Celina Kombani, waziri wa sheria na katiba na Jaji Fredrick Werema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Uchunguzi unaonyesha kwanza hawakuwa tayari kuona mabadiliko na hawakuwa tayari kutoa fursa ya kupata mawazo mapya kutoka nje ya duara lao.

“Waliongozwa na ushabiki wa lazima tushinde wapinzani. Ni tabia yao hiyo iliyoathiri fikra za wabunge wengi hata katika jambo hili muhimu kwa vizazi na vizazi,” ameeleza mbunge mmoja machachari wa CCM.

0
Your rating: None Average: 5 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: