Kikwete si busara kulea akina Sophia

WIKI iliyopita nilieleza sababu za kutoswa kwa baadhi ya mawaziri wa serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete kuwa ni pamoja na kushindwa kwao kuwajibika ipasavyo kwa majukumu waliyopewa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, nilimtaja kama miongoni mwa mawaziri hao ambao utendaji wao haujanufaisha taifa kimatarajio. Hawa wamebaki mzigo kwa wananchi wanaolipia gharama za kuendesha serikali.
Katika utawala unaojali kila nukta ya muda wake wa kukaa madarakani, ni hatari kuendelea kubeba mizigo kwa kulea viongozi wasioleta tija.
Ni hatari kwasababu unapowadia muda wa wananchi wa kupima kazi iliyofanywa na utawala, kinachoangaliwa ni utendaji wa ujumla, nini kilifanyika, maisha bora kwa kiwango gani yalifikiwa na wananchi.
Kwa hiyo yeyote ambaye ni kigezo cha kufikiwa kwa mafanikio makubwa ya pamoja hana sababu ya kulindwa kwa kubebwa. Anakuwa mzigo.
Nilikumbusha kwamba juhudi za wazi zilizofanywa na Rais, moja kuandaa semina elekezi hotelini Ngurdoto na pia kutembelea wizara moja moja akieleza watendaji na vinara wa wizara staili mpya ya utendaji kazi inayofaa katika awamu yake ya uongozi.
Haiwezekani kupima utendaji wa kiongozi kwa miaka mitano yote. Muda huo ni mwingi ambao ukiisha, athari zitakazokuwa zimeikumba wizara ya waziri mhusika aliyeshindwa kazi, zitakuwa kubwa isivyo mithilika.
Kwa maana hiyo, alitarajia kwamba kila mwaka angetathmini hatua zilizochukuliwa kulingana na matarajio. Kwa msimamo huo peke yake, viongozi kama Sophia wangebaki mzigo na kwa jumla, aibu kwa taifa.
Kuna maswali mengi yanaulizwa mitaani kwamba inawezekanaje kiongozi aliyeaminika na kukabidhiwa wadhifa mkubwa kama wa Sophia, lakini akashindwa kuthamini dhamana aliyopewa, anaendelea kulelewa wakati anaipaka serikali matope?
Huyu ndiye anasimamia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Idara ya Usalama wa Taifa (TIS), na muhimu zaidi anasimamia utawala bora. Ilitarajiwa uongozi wake uwe ndio kioo kwa viongozi wengine katika kuendesha mambo kwa kufuata sheria na haki.
Unapotafakari kwa mapana nafasi aliyojiweka Sophia, si tu alikuwa amemrahisishia kazi Rais Kikwete kwamba hafai kutekeleza wajibu wa waziri wa kusimamia utawala bora serikalini, bali pia alikuwa ametoa angalizo muhimu kwamba ni muhimu uteuzi ukafanywa baada ya uchambuzi makini.
Nikiunganisha tukio la Sophia kumwaga razi kwenye mkutano wa wabunge wa CCM na Kamati ya Mzee Ali Hassan Mwinyi na taarifa zilizofikia vyombo vya habari kuwa Rais aliporejea nchini akitokea ziarani nchini Misri, alipanga kufanya kikao cha baraza la mawaziri, ilionekana dhahiri alikerwa na hayo.
Kilichotarajiwa hapo ni kwamba rais Kikwete kwa kuchoshwa na tabia mbaya ya viongozi kama huyu Sophia, basi lazima angeamua kulitikisa baraza la mawaziri kwa mabadiliko hata madogo.
Rais alisoma magazeti na kutonywa na wasaidizi wake na ukweli ulidhihirika kuwa baadhi ya mawaziri, wakiongozwa na Sophia walipindukia kwa utovu wa adabu. Walijivua uadilifu na walifuta imani waliyokuwa nayo wananchi juu yao.
Kuna habari zilivuja kwamba Rais hakufurahishwa na ushangingi uliojitokeza kwenye kikao hicho, hasa ulioendeshwa na wasaidizi wake, akina Sophia. Hilo moja, ingawa hakufurahishwa na kutaka tabia hiyo ikome, watu walitarajia basi angechukua hatua dhidi ya walevi wa madaraka.
Hatua hizo ndizo zinasubiriwa hadi leo hii, na hadi ninapojadili hapa ningali naamini hizo ndio hatua za kuthibitisha kumbe kweli katika urais wake, rais Kikwete hana mbia yeyote labda Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein.
Kwa nini watu wanatamani kuona Sophia na wanaofanana naye wakitupwa nje ya baraza? Ni kwa kuwa hiyo itasaidia kuzindua wengine juu ya mwenendo mwema wanaotakiwa kustawisha katika ofisi za umma.
Wakumbuke kwamba yule anayeteuliwa amepewa dhamana ya kuongoza masuala ya umma. Uongozi una misingi yake na inapaswa kufuatwa kwa ajili ya kuleta tija na huduma nzuri kwa wananchi.
Sophia, kwa kipindi kisichozidi miezi sita amekuwa akijitumbukiza katika mambo ambayo kama kweli umakini ungekuwa unatawala serikalini, angekuwa amesahaulika kama waziri tena katika Ofisi ya Rais.
Ni huyu aliyepigana hadharani na mwanachama mwenzake na mbunge, Janeth Kahama, katika harakati zao za kuwania uenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM. Kisa? Hakuna msingi. Jiulize tena, hata sasa baada ya kuufikisha uwaziri kwenye ngazi ya chini kama alivyofanya, nini kimemtokea? Hakuna!
Mwisho, tujiulize kwa nini Rais ameamua kumwacha Sophia licha ya tafrani alizozusha na matope aliyoipaka serikali yake, jibu ni gumu zaidi kwa sababu mbali na kujaza tu nafasi aliyonayo, waziri huyo haonyeshi kama anajua anachokifanya kwenye ofisi ya umma.
Hata kama Sophia ataingia mwaka mpya bado ameshikilia wadhifa huo, na hata kama ataendeleza ushangingi kwa kutojali asemalo na kutowajibika kama waziri mweledi, jambo moja linabakia dhahiri; bila Rais kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya watu kama Sophia, basi ajue amebeba mzigo mkubwa na mzito utakaomgharimu.
Ajabu uzito huu unaomkabili Rais Kikwete unaendelea wakati anajua fika mwaka ujao ni mwaka wa uchaguzi na atapimwa kwa yale aliyotenda kama rais na yaliyotendeka kutokana na uongozi wake.
Si siha njema ya kisiasa kiongozi mkubwa kama rais anayehitaji kura za wananchi ili kuendelea kuongoza taifa, kujitwika mizigo ya kisiasa itakayompa ugumu katika safari yake ya kuomba tena ridhaa ya wananchi.
Rais ana mamlaka kamili na Sophia. Na kwa kweli kuachia tu hali tunayoamini haifai, atakuwa amewasilisha ujumbe mmoja mkubwa kwa umma: Kwamba yeye ni shujaa wa kulea uchafu. Inampasa afikiri zaidi maana Watanzania wana haki ya kusherehekea kuingia kwa mwaka mpya wa 2010 na matumaini.