Kikwete tumbo moto


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 29 December 2010

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

HOFU imetanda serikalini ya kuanikwa kwa taarifa za mazungumzo ya siri kati ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa serikali ya Marekani, MwanaHALISI limeelezwa.

Tayari mtandao wa WikiLeaks umevujisha mazungumzo ya siri kati aliyekuwa naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Jendayi Frazer na rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

MwanaHALISI limefahamishwa na vyanzo vyake ndani ya serikali kuwa Rais Kikwete aliwahi kukutana na Frazer mara kadhaa kati ya 2005 na 2010.

Katika mikutano hiyo, mtoa taarifa anasema, Rais Kikwete na Frazer walijadili mambo mengi yanayohusu Tanzania, Afrika na kimataifa.

Mkutano wa kwanza kati ya Kikwete na Frazer ulifanyika Jumatatu ya 17 Oktoba 2005, katika ofisi za wizara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimatifa, jijini Dar es Salaam. Alikuwa hajawa rais.

“Bila shaka Kikwete amekuwa akimweleza mengi Frazer. Haya mambo yakiibuka leo, yanaweza kubomoa hadhi yake,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya CCM ambaye aliwahi kuwa waziri.

Anasema, “Unaju ndugu yangu, mazungumzo ya rais na Frazer yalifanyika katika mazingira ya kuaminiana sana kama ulivyo utaratibu wa kidiplomasia; kwamba kinachozungumzwa kinabaki siri ya wazungumzaji au ya mataifa yao. Sasa, unaweza kuona mwenyewe hatari iliyopo.”

Mtoa taarifa anasema wakati Kikwete anakutana na waziri huyo wa Marekani, ndio kwanza alikuwa amepitishwa na chama chake kuwa mgombea urais.

Anasema, “Nakuhakikishia kwamba kuna uwezekano mkubwa wa rais kuahidi mambo mengi ili kujijengea mazingira mazuri ya kukubalika kwa taifa kubwa kama Marekani.”

Akiongea kwa kujiamini, mtoa taarifa huyo amesema, “Rais lazima atakuwa amezungumzia msimamo wa serikali yake kimataifa na jinsi atakavyoshughulikia mambo ya ndani ya nchi.”

Anasema, “Rais anaweza kuwa aliahidi jinsi ya kushughulikia waasi wa Burundi, uhusiano wake na mataifa mengine ya Afrika, Komandi kuu ya kijeshi ya Marekani barani Afrika (Africom) na hata ubinafsishaji wa mashirika ya umma, mikataba ya madini, uwekezaji na mapambano dhidi ya rushwa.”

Kabla na baada ya Kikwete kuingia madarakani, waliojiita “wana-mtandao” walijiapiza kuwa mgombea wao angerejesha nyumba za serikali zilizouzwa kiholela na angerejesha mikononi mwa wananchi mashirika ya umma yaliyobinafsishwa kinyume cha taratibu.

Wachunguzi wa mambo wanasema inawezekana Kikwete alikwenda mbali kueleza jinsi atakavyokuwa na serikali imara, akitaja atakuwa na nani; na nani hawezi kumteua na kwa nini.

Kwa mujibu wa mmoja wa maofisa waliohudhuria mazungumzo hayo, Rais Kikwete alimweleza Frazer jinsi serikali ilivyopania kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 unakuwa huru na wa haki.

Akijibu swali la naibu waziri huyo aliyetaka kujua nafasi ya CCM katika uchaguzi mkuu upande wa Zanzibar, Kikwete alisema, “Matokeo yatakuwa mazuri.”

Kuibuka kwa taarifa hizo kumekuja wiki moja baada ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Edward Hoseah, kunukuliwa akimtuhumu Rais Kikwete kukwamisha utendaji wake wa kazi.

Taarifa za Hoseah kumtuhumu Kikwete zilipatikana katika mtandao wa WikiLeaks ukimnukuu mwanadiplomasia wa Marekani, Purnel Delly, ambaye alikutana faragha na Hoseah mwaka 2007.

Hoseah ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe katika Kamati ya rais iliyopewa kazi ya kukusanya fedha zilizoibwa Benki Kuu ya Taifa (BoT), alinukuliwa na mtandao huo akisema, “Rais Kikwete hana dhamira ya kuwafikisha mahakamani walarushwa wakubwa nchini.”

Aliyekuwa waziri wa Utawala Bora, Sophia Simba aliuambia mkutano kati ya kamati ya wazee wa chama chake na wabunge, uliofanyika Novemba 2009 katika ukumbi wa zamani wa Bunge mjini Dodoma, kwamba ndani ya CCM hakuna aliyesafi.

Simba ambaye vyombo vya TAKUKURU na Idara ya Usalama wa Taifa vilikuwa chini yake, mbali na kueleza jinsi fedha zilizoibwa, alidai kuwa mmoja wa watuhumiwa wakuu wa wizi huo, Jeetu Patel alifadhili mbio za kusaka urais za John Malecela mwaka 2005.

Waziri huyo ambaye wakati huo ofisi zake zilikuwa ikulu, alikieleza kikao cha wabunge na wazee, “Hakuna mwenye ubavu wa kunyooshea kidole wengine.”

Alisema Jeetu alitoa kiasi cha Sh. 200 milioni na kumpa Malecela na kwamba kelele za Anne Kilango Malecela za kupiga vita ufisadi, zinatokana na kile alichoita, “Nongwa ya kuukosa u-first lady” – mke wa rais – iwapo Malecela angepata urais.

“Rais anayajua haya. Kuna uwezekano mkubwa kuwa tayari ameyamwaga kwa Marekani ili kujikwamua na shinikizo la wafadhili wanaomtaka kukamata watuhumiwa wa EPA,” anaeleza mbunge mmoja wa CCM kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Amesema iwapo haya yatatoka, kwanza yatamgombanisha rais na wenzake, lakini pia, yatashusha hadhi yake kitaifa na kimataifa.

Anasema, “Hebu fikiria kama rais mwenyewe atanukuliwa akiwataja kwa ubaya watangulizi wake. Au akiwasema marais wa nchi jirani ambao anakaa nao kila siku. Je, hapo kutakuwa na kuaminiana kweli,” anahoji.

“Au kama alimwambia Frazer kuwa haridhiki na mawaziri wake fulani au hana imani nao… unadhani nini kitatokea kwenye baraza la mawaziri? Watu si wanaweza kumuacha peke yake?” kiliuliza chanzo hicho.

Mkutano mwingine muhimu kati ya Kikwete na Frazer ulifanyika Jumatano 16 Aprili 2008, katika Hoteli ya Intercontinental, jijini New York, Marekani.

Vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, viliripoti kuwa ajenda kuu ya mkutano wao ilikuwa ni hali ya Zimbabwe na jinsi Umoja wa Afrika (AU) na Marekani zinavyoweza kusaidia kuhakikisha uchaguzi nchini humo unafanyika chini ya misingi ya amani na haki.

Hata hivyo, vyombo hivyo havikueleza chochote kuhusu mazungumzo ya faragha ya viongozi hao.

“Ngoja nikwambie kitu ndugu yangu. Taarifa inayotolewa kwa waandishi baada ya mazungumzo ni sehemu tu ya kile kilichozungumzwa.

“Kwa mfano, iwapo kuna pande zinapingana, taarifa ya maafikiano itakayotolewa kwa waandishi huwa haielezi kuhusu migongano au ugomvi uliotokea katika mchakato mzima wa kutafuta amani. Kwa hiyo, waandishi huwa mnapewa vitu vidogo sana,” mtoa habari wa gazeti hili ameeleza.

Inadaiwa kuwa rais Kikwete alikutana mara kadhaa na Frazer jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo walijadili mambo mbalimbali ya uongozi nchini na Afrika kwa jumla.

Kwa mujibu wa nafasi yake, Frazer alikuwa na kazi ya kushughulikia masuala ya Afrika na alikuwa akipeleka makao ya wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, taarifa zote za mazungumzo yake na viongozi wa Afrika.

Kikwete anachukuliwa kuwa kiongozi kipenzi cha Marekani katika ukanda wa Mashariki mwa Afrika na Eneo la Maziwa Makuu; nafasi aliyopata akiwa mwenyekiti wa AU, miaka mitatu iliyopita.

Uhusiano huo wa karibu na utawala wa Marekani ulizua utata Septemba 2006, wakati habari zilipovuja kuwa akiwa jijini Washington, rais alikutana na aliyekuwa Rais wa Marekani, George W. Bush na kuongelea hali tete ya kisiasa Kenya.

Hakuna taarifa iliyowahi kutolewa kuhusu walichozungumza, ingawa kuna uwezekano mazungumzo hayo yalirekodiwa na kuna hofu ya kuwekwa wazi na mtandao wa WikiLeaks.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: