Kila la kheri Wambura, Rage lakini...


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 07 April 2010

Printer-friendly versionSend to friend

ISMAIL Aden Rage aliingia klabu ya Simba akaichezea kidogo na baadaye akaiongoza halafu akaondoka akiwa hajaifanyia kitu cha maana. Hata leo hawezi kusimama hadharani akatamba kupata kuifanyia Simba cha maana.

Labda waliporejea kutoka mazoezini Brazil na kile alichodai kuwa ni mfumo wa uchezaji wa samba na diagonal. Hizo zilikuwa ghiliba tu.

Juzi tumemshuhudia Michael Richard Wambura akitangaza nia ya kuwania uenyekiti wa klabu hiyo iliyoanzishwa miaka 74 iliyopita. Je, anakuja na jipya gani? Kama mwanachama huyo si mpya basi hana jipya.

Wambura aliwahi kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa muda wa Simba katika kipindi ilipogubikwa na migogoro ya uongozi. Ilitarajiwa angetumia uwezo wake kurejesha hali ya amani lakini alishindwa kwa vile alishuka na tabia ya uongozi wa kubagua vyombo vya habari aliokuwa kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mlango alioutumia Wambura kuingia kwenye soka unatatanisha. Kwanza alikuwa katibu wa Chama cha Kriketi na kutokana na nafasi yake akawa mjumbe katika Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Waziri wa Elimu, Utamaduni na Michezo wakati huo, Prof Juma Kapuya alimteua Wambura kuwa katibu wa kamati ya kukarabati Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) iliyokuwa chini ya Zaynudin Adamjee.

Adamjee na Wambura wakaanza kutumia kamati hiyo kufanikisha malengo yao ya kuwa viongozi wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) mwaka 1997. Adamjee alikuja kujitoa baada ya kuwa mbunge lakini Wambura akaja kumwangusha Rage katika kinyang’anyiro cha ukatibu mkuu wa FAT enzi mwenyekiti akiwa Muhidin Ndolanga.

FAT ya Ndolanga chini ya makatibu wakuu wote watatu, Ally Hassan Mwanakatwe (1993-1996), Rage (1996-2000) na Wambura (2000-2004) ilijaa migogoro. Rage alikuja kuonja jela kwa makosa ya utendaji FAT japo baadaye aliokolewa na parole kabla ya kukata rufaa na kushinda.

Uongozi wa Ndolanga na Rage uliwahi kutupwa nje na serikali ikateuliwa kamati ya muda, lakini FIFA iliwasimamia wakarudi na hata uongozi wa Ndolanga na Wambura uliwahi kuondolewa kwa hasira za wajumbe ukaingia uongozi wa Yahya Mhata na Mwina Seif Kaduguda kama katibu.

Uchaguzi mkuu wa Desemba 2004 ndio uliondoa ghasia TFF. Wambura alijiimarisha kuwania nafasi ya urais, lakini pamoja na kampeni za usiku kucha na mwenyekiti wake waliangushwa na mchezaji wa zamani wa Yanga na Pan African na kocha msomi, Leodegar Tenga.

Tenga alishika hatamu kwanza akimteua Ashery Gesabile kuwa katibu mtendaji halafu baadaye Fredrick Mwakalebela. Rage alishinda nafasi ya makamu wa pili wa rais, lakini alipoteza alipofungwa.

Mlezi wa klabu ya Simba, Prof Philemon Sarungi alimteua Wambura kuwa mwenyekiti wa muda baada ya yeye kupewa jukumu hilo na mahakama. Historia ya uongozi wa Rage na Wambura ndiyo inapaswa kutazamwa kama wanaohitajika sasa kuiongoza klabu hiyo kubwa.

Mambo yako wazi. Rage aliyewahi kuwa katibu mkuu wa DRFA, sasa ni mwenyekiti wa soka mkoa wa Tabora. Tazama mkoa huo una mafanikio gani kisoka? Maana mtu hawezi kusema ataipa maendeleo Simba wakati maeneo aliyobahatika kuongoza hayana mafanikio.

Au katika kipindi kifupi cha uongozi wa Wambura, kulikuwa na
mikakati gani maridhawa iliyobuniwa kwa maslahi ya Simba. Kuna muujiza gani anaokuja nao leo?

Ametangaza mikakati 18 akisema Simba lazima inufaike na rasilimali zake. Akasema ili klabu inufaike ni lazima mfumo wa klabu ubadilike kutoka wa ridhaa na kuwa wa kulipwa hali itakayoifanya ijiendeshe kibiashara na ushindani.

Alisema mpango huo pia utawezesha klabu kununua hisa katika makampuni mbalimbali katika soko la mitaji na hisa la Dar es Salaam (DSE). Hizi ni ndoto nzuri.

Wambura alisema iwapo atapata ridhaa ya wanachama atahakikisha mfumo wa uendeshaji unakuwa wa kulipwa na wachezaji watakuwa na mikataba na klabu tofauti na ilivyo sasa. Lakini sera inaruhusu?

Pia Wambura ameweka mikakati ya kuimarisha kitengo cha uhasibu, masoko na habari kwa kuajiri wataalamu wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa kuitangaza klabu pamoja na kuanzishwa gazeti. Hapa anamaanisha magazeti mawili ya Msimbazi na Ngurumo za Simba si mali ya klabu.

Vema lakini hizi ndiyo siasa za miaka nenda rudi za wagombea, wakichaguliwa hukaa madarakani hadi kipindi chao kikiisha huiacha klabu ikiwa na hali mbaya kuliko walivyoikuta.

Hata uongozi wa sasa chini ya mwenyekiti Hassan Dalali na katibu mkuu Mwina Kaduguda uliahidi neema hiyo. Leo umepitisha miezi minne ukigoma kuandaa uchaguzi kwa visingizio mbalimbali.

Dalali na Kaduguda watajivunia kuifunga Yanga lakini jengo la klabu bado chafu, milango na vyoo vyake ovyo na si vyumba vyote vinavyotumika kikamilifu. Wamemaliza kipindi chao klabu ikiwa haina dira ya hata nini kifanyike mwakani.

Sitamzungumzia Mohamed Nanyali kwa sababu simjui. Lakini nadhani hawa ninaowafahamu – Rage na Wambura – hawajasahau kitu Simba na ikiwa kipo basi kila la kheri katika uchaguzi mkuu wa Mei 29, mwaka huu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: