Kila mwaka? Kama ndivyo, basi!


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi

SASA bia wanywe wao. Soda wanywe wao. Sigara wavute wao. Sisi basi. Ebo! Hivi hapa ndipo mahali pekee ambako serikali inaweza kupata fedha za bajeti?

Twende kwenye bia. Kama serikali inajali, kwanini isiteremshe bei ya bia. Ili watu wengi waweze kunywa au watu walewale waweze kunywa bia nyingi.

Ili kampuni ziweze kutengeneza bia nyingi. Ili kampuni zipate mapato makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili serikali iweze kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?

Twende kwenye soda. Kama serikali inajali, kwanini isiteremshe bei ya soda. Ili watu wengi waweze kunywa au watu walewale waweze kunywa soda nyingi.

Ili kampuni ziweze kutengeneza soda nyingi. Ili kampuni zipate mapato makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili serikali iweze kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?

Twende kwenye sigara. Kama serikali inajali, kwanini isiteremshe bei ya sigara. Ili watu wengi waweze kuvuta au watu walewale waweze kuvuta sigara nyingi.

Ili kampuni ziweze kutengeneza sigara nyingi. Ili kampuni zipate mapato makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili serikali iweze kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?

Sasa wanywaji hawana hamu tena! Ama serikali inywewe bia; inywe soda na ivute sigara. Au wavitumie wanaovitengeneza.

Huo hapo juu waweza kuonekana kama muweweseko wa wanywaji soda, bia na wavuta sigara; bila kujua uchumi wa uzalishaji na masoko. Lakini kwa viwango vyovyote vile, kuna mantiki.

Ukitokea mgomo wa “kunywa” na “kuvuta,” mwezi wa sita wa mwaka wowote ule, nchi ikiwa chini ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), bajeti haitasomwa kamwe. Haitakamilika.

Kila mwaka ni bia, soda na sigara; hadi wenye viwanda wakaonya kwamba mwaka huu wakipandishiwa kodi zaidi ya asilimia 10, hawataielewa serikali.

Kujaribu kuonyesha “ubunifu,” serikali imekuja na pendekezo la wanaotaka usajili wa magari kwa utambulisho wa taarifa za mtu binafsi – majina, labda na picha na chochote kile – kulipa Sh. 5 milioni kwa miaka mitatu.

Ni yaleyale ya bia, soda na sigara. Serikali inasema itakusanya Sh. 50 milioni katika miaka mitato; kwa kutoza Sh. 5 milioni kwa atakayetaka urembo.

Hii ina maana serikali imelenga watu 10 tu. Wakilipa milioni 50 kila mmoja, serikali itakuwa imeridhika. Masikini!

Kama serikali inahitaji fedha kwa njia hii, kwanini isitoze Sh. 200,000 kwa mwaka kwa gari kwa maelfu ya magari ya vijana wanaotaka mbwembwe? Itapata zaidi.

Ukiangalia orodha ya magari binafsi yaliyosajiliwa hadi sasa katika mfumo mpya, utaona yametoka AAA hadi CAG. Haya ni maelfu ya magari. Serikali haitaki wanaoyamiliki washiriki.

Kinachoonekana hapa ni kwamba, watunga bajeti wanataka watu wachache (10), na huenda mafisadi wachafu zaidi, wapate nafasi ya kujitambulisha kwa mbwembwe.

Kwamba wezi wakubwa, wenye mabilioni ya shilingi ya kusambaza; mabilioni waliyopora umma wa nchi hii; wapate nafasi ya kuwakoga wananchi na kuonyesha kwamba wao ni tofauti.

Kwamba mafisadi walioshindikana, sasa wapate nafasi ya kurudi upya katika umma, kwa kuutisha, kuushangaza, kuukoga na kuudhalilisha kwa fedha walizowaibia.

Lakini, hata kama kiwango kisingekuwa Sh. 5 milioni, au laki mbili; wazo lenyewe la mikogo, katikati ya umasikini unaoandama wananchi, hakika ni la kibwege sana.

Aliyetoa wazo hilo barazani na “wataalam” walioliunga mkono ili kupata Sh. 50 milioni, wamedhihirisha uchovu mchafu.

Hiki ni kiasi ambacho serikali inaweza kupata katika siku nne tu kutokana na faini kwa makosa ya barabarani katika jiji la Dar es Salaam peke yake!

Serikali yaweza kupata kiasi hiki katika wiki moja au siku saba, kwa kusimamia kwa makini, ukusanyaji kodi kwenye masoko.

Fedha zinazohitajika ili kukidhi mbwembwe za kifisadi, zinaweza kupatikana – tena mara kumi au ishirini au zaidi – kwa siku moja tu, kwa kufuta wilaya moja iliyoundwa kisiasa na isiyo na manufaa kiuchumi kwa wananchi.

Watunga bajeti hawaoni wezi wanaokwapua madini kweupe. Hawaoni mafisadi wenye kodi za wananchi kwenye akaunti zao Ulaya. Hawaoni mabomba yanayovujisha mabilioni ya shilingi kwa njia ya mishahara hewa.

Hawaoni! Hawaoni safari za ndani na nje za watawala zinazokausha hazina na madarasa ya Ngurdoto yanayokamua walipakodi. Hawaoni dege la serikali lilalo mafuta kama ibilisi. Hawaoni!

Si busara kupendekeza serikali isitoze kodi kwenye bia, soda na sigara. Bali hoja ni hii:

Kuna muda mwingi na mrefu wa kuandaa bajeti. Kuna vyanzo lukuki. Kitendo cha serikali kuonekana inakwanyiakwanyia – shika hili shika lile – dakika za mwisho na katika bidhaa zilezile, ni ushahidi watawala wanaishi kama wapitanjia.

Na mpitanjia hajengi.

0713 614872
0
No votes yet