Kilichomponza DC Henjewele


Igenga Mtatiro's picture

Na Igenga Mtatiro - Imechapwa 23 June 2012

Printer-friendly version

TUKIO la tarehe 16 Machi 2012 ambapo Mkuu wa wilaya ya Tarime, John Henjewele alimpiga dada yake Rose Henjelewe eneo la Mbezi Louis na kumjeruhi katika ugomvi wa kifamilia, lilipaswa kumzindua Rais Jakaya Kikwete juu ya mteule wake.

Kisa nyumba. Mkuu huyo wa wilaya akishirikiana na ndugu zake wawili, walitaka kumshawishi mama yao wauze nyumba, lakini Rose alipinga. Henjelewe aliamua kumdunda dada yake ambaye alikimbilia polisi kuripoti.

Kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela aliithibitishia MwanaHALISI kutokea tukio hilo na akamtaka DC Henjewele ajisalimishe haraka ili sheria ichukue mkondo wake.

Tuhuma hizo ziliripotiwa katika kituo cha polisi Kawe, jijini Dar es Salaam na kuandikishwa kwa taarifa Na. KW/RB/2442/2012 ya Machi 16, mwaka huu.

Baada ya kupiga chenga wiki kadhaa, hatimaye mkuu huyo wa wilaya alijisalimisha na kama kawaida ya polisi wa nchi hii “wakaua kesi” inayohusu kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wanahabari wamejitahidi kufuatilia kuona akifikishwa mahakamani lakini wapi.

Tarime wakajiuliza, kama hana uwezo wa kushawishi hata ndugu zake tu katika suala linalohusu nyumba yao,  anawezaje kuwasikiliza wananchi wenye malalamiko ya kuporwa mashamba au ardhi yao? Kesi haipo kortini lakini jalada la tuhuma dhidi ya Henjewele liko polisi.

Je, polisi wametumika kuua ‘soo’ ili Henjelewe ateuliwe tena kuwa DC Tarime? Kwa hiyo, habari za DC kupiga mtu ndiyo sifa zinazohitajika katika utawala huu?

Uthibitisho kuwa DC bondia mteule wa Rais Kikwete hahitajiki tena, madiwani wa wilaya ya Tarime, katika kikao cha Baraza la Madiwani, kisicho cha kawaida, waliamua kumjadili na kumkataa.

Siku hiyo, iliyokuwa maalum kwa ajili ya kujadili agenda moja tu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), baraza halikuimba wimbo wa taifa, sala ya Halmashauri wala kufunguliwa na Mwenyekiti, Amos Sagara.

Walichokifanya madiwani hao ni kujiandikisha katika kitabu cha mahudhurio na kuanza kujadili ajenda hiyo moja na kujiapiza lazima mkuu huyo ang’oke na kubadilishiwa kituo cha kazi. Katibu tawala msaidizi wa mkoa wa Mara, Joseph Makinga alimwakilisha mkuu wa mkoa huo, John Gabriel Tupa.

Msimamo huo ulitolewa na madiwani 39 waliohudhuria kati ya 41; 22 wa CCM, mmoja wa Chama cha Wananchi (CUF) na 16 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Sagara aliwaambia waandishi wa habari, baada ya mkutano huo, kwamba wameazimia kumkataa DC Henjewele kuendelea kuwa mkuu wa wilaya hiyo kutokana na sababu kadhaa.

Baada ya tamko hilo la madiwani juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika kufifisha au kuua hoja ya kumkataa DC.

Kwanza waliandaliwa vijana wafanye maandamano ya amani kupinga madai ya madiwani ya kutaka mkuu huyo wa wilaya ahamishwe lakini ilishindikana.

Pili, Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine aliwaita mwishoni mwa wiki iliyopita madiwani wote wa chama hicho ili kuwashawishi wafute madai yao na wawaachie vyama vya upinzani, lakini ikashindikana.

Hoja za madiwani kumkataa DC huyo ni hizi. Kwanza ni kwamba mkuu wa wilaya hiyo, ameshindwa kuondoa kizuizi kilichopo eneo la Nkende katika barabara iendayo Sirari baada ya kubainika kuwa kizuizi hicho kinatumika kwa maslahi binafsi ya wakubwa kupitia polisi.

Katika taarifa, ambayo wanataka ifikishwe kwa Waziri mkuu, Mizengo Pinda, Sagara alisema ingawa kizuizi hicho kimewekwa kwa malengo mazuri ya kudhibiti magendo na wanaokwepa kulipa kodi katika Mamlaka ya Mapato (TRA) na wanaoendesha uhalifu mbalimbali, askari waliopo eneo hilo ndio  wanahusika kukusanya pesa na kutia mifukoni mwao.

Pili, Sagara alisema DC huyo ameshindwa kuhakikisha usalama wa wananchi katika wilaya nzima kutokana na kuongezeka kwa mauaji ya watu na wengine wakivamiwa na kuporwa wakati vyombo vya ulinzi na usalama vinamzunguka.

Baadhi ya matukio ya mauaji ni ya watu watano na wengine watatu kujeruhiwa na polisi katika eneo la Nyabirama katika mgodi wa dhahabu North Mara tarehe 16 Mei 2011. Polisi waliohusika na mauaji hayo hawakushughulikiwa.

Tukio jingine ni la kuuawa kwa kijana Joseph Mwikabe Mtatiro (20) wa kijiji cha Kwisarara kata ya Bumera 7 Mei 2012. Kijana huyo alipigwa risasi begani  na mlinzi wa kampuni ya Barrick inayochimba madini ya dhahabu katika mgodi wa North Mara.

Tatu, analalamikiwa kwa kushindwa kwake au kuacha kushughulikia mgogoro wa ardhi ulioibuka kati ya kijiji cha Nyamohonda kata ya Susuni na kijiji cha Ikoma kilichoko kata ya Ikoma wilayani Rorya ambacho wakazi wake wameingilia na kupora ardhi ya Nyamohonda.

Katika mgogoro huo, uliosababisha uharibifu wa mali, watu 31 wa kijiji cha Ikoma akiwemo diwani Laurent Adriano (CCM) walikamatwa na polisi.

Vilevile analalamikiwa kwa kushindwa kusaidia utatuzi wa mgogoro wa ardhi uliotokana na askari wa Jeshi la wananchi kituo cha Nyandoto kuwapiga wananchi na kunyan’ganya maeneo yao huko Bugosi kata ya Nyamesangura.

Nne, analalamikiwa kuzuia uongozi wa Barrick katika mgodi wa North Mara kutoa fungu la fedha kwa ajili ya kusomeshea wanafunzi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo. Henjewele alizuia utaratibu wa vijiji kupewa fedha (asilimia moja) moja kwa moja badala yake akataka ziingie kwanza wilayani kupitia halmashauri sawa na mrabaha wa Sh. 250 milioni.

Inadaiwa katika moja ya mikutano na wananchi wa Nyamongo, mkuu huyo wa wilaya alisema kwa dhihaka, “Hivi walitegemea wao wazae na mgodi uwasomeshee watoto?”

Tano, analalamikiwa kuipendelea kampuni ya Barrick katika suala la fidia ya ardhi inayotakiwa kuchukuliwa na kampuni hiyo akidai wananchi wanalima na kujenga nyumba kwa “kutegesha”.

Kutegesha ni kuejenga nyumba au kuwekeza mali katika  eneo ambalo halijapimwa ili litakapopimwa na wataalamu fidia iwe kubwa.

Sita, mkuu wa wilaya analalamikiwa kwa kitendo chake cha kumwondoa madarakani mwenyekiti wa kijiji cha Nyakunguru, Abeil Maginga kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za kijiji.

Hata hivyo, ni kweli wajumbe wengi wa serikali ya kijiji hicho walimkataa kutokana na tuhuma zilizomhusu, lakini maamuzi hayo yalipaswa yapitiwe na kuamuliwa na mkutano mkuu wa kijiji na kisha muhtasari wake kuwasilishwa ofisi ya mkurugenzi kwa uchunguzi.

Alipopigiwa simu na kueleza tuhuma za madiwani dhidi yake, Henjewele alikanusha madai yote na akasisitiza haitawezekana kuondoa kizuizi cha magari eneo la Magena akisema kipo kiusalama zaidi. Pia alikanusha polisi kukitumia kwa maslahi binafsi.

Na kuhusu madai ya kutegesha mali na nyumba, DC huyo alidai yeye ndiye aliwatetea wananchi waliotegesha kabla ya kutathiminiwa walipwe na mgodi kwa awamu hii kwani mgodi ulikuwa umekataa.

0
No votes yet