Kimbisa: Sikutumia fedha kushinda ubunge


mashinda's picture

Na mashinda - Imechapwa 01 August 2012

Printer-friendly version
Alhaj Adam Omari Kimbisa

“SIKUTUMIA fedha kushinda ubunge wa Afrika Mashariki. Nitumie fedha za nini…utampa nani? Pale ukitoa pesa huchaguliwi, wabunge wataona unataka kuwanunua, nani anataka kununuliwa?” anahoji Adam Kimbisa katika mahojiano na MwanaHALISI.

Ameongeza: “Kama ni pesa labda nilizotumia kujaza mafuta kwenye gari langu kwenda Dodoma na kurudi. Pia, labda gharama za simu nilizotumia kuwapigia wabunge kuomba kura.”

Kimbisa, mmoja wa wabunge tisa wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) waliochaguliwa hivi karibuni, alikuwa anajibu tuhuma kuwa rushwa ilikithiri uchaguzi huo.

Tuhuma zilitolewa na baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri, kuwa wagombea hao, akiwamo Kimbisa, walitembeza “rushwa ya kutisha” kwa viwango tofauti kuanzia Sh. 100,000 hadi Sh. 1,000,000 kwa kila mmoja kutegemeana na hadhi ya mbunge anayehongwa.

Lakini Kimbisa anasema tuhuma hizo si za kweli bali “ni mbwembwe tu za uchaguzi”.

“Kila uchaguzi una mbwembwe zake, hata wewe hapo (mwandishi) ukiamua kugombea wataibuka watu wataanza mbwembwe zao. Utasikia mara udini, mara rushwa, ukanda au ukabila…hizo tuhuma za rushwa mimi sikuona kama tatizo kubwa, bali ni mbwembwe tu za uchaguzi,” amesema.

Amesema jambo la muhimu ni kuangalia iwapo aliyeshinda ana vigezo vinavyotakiwa kwa maana ya elimu, uzoefu, umri na hadhi yake mbele ya jamii.

Kimbisa ambaye pia amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania katika bunge hilo, amesema ameshinda uchaguzi kutokana na sifa, uwezo, elimu na uzoefu wake katika nyanja za kimataifa.

Miongoni mwa sifa hizo, Kimbisa ana shahada ya pili ya uchumi akibobea katika uchumi mkubwa na mdogo, diplomasia, ujuzi wa lugha, kikiwemo Kifaransa kinachotumiwa na nchi za Rwanda na Burundi; na uzoefu katika masuala mbalimbali ya kimataifa.

Hata hivyo, amesema uchaguzi huo haukuwa rahisi kwake kwa kuwa “jimbo la lake uchaguzi” kwa maana ya bunge, ni gumu, limejaa watu waelewa na wanaotumia vigezo stahili kumchagua mtu wa kuliwakilisha taifa.

Ametaja vipaumbele vyake katika nafasi hiyo kuwa ni kusimamia maslahi ya Tanzania katika EAC, hasa ajira ambayo inalalamikiwa sana; na ardhi ambayo ameitaja kama rasilimali pekee waliyobaki nayo Watanzania.

“Ninajua wananchi wengi ni maskini hasa huko vijijini, wakija wageni na pesa kidogo wengi wataachia ardhi yote. Hili la ardhi hadi sasa halimo kwenye makubaliano, hivyo tutazidi kulisimamia lisiingie milele,” amesema.

Kuhusu ajira, Kimbisa amesema wananchi wana wasiwasi sana na wageni kuchukua nafasi zote muhimu, lakini yeye anaahidi kulinda zile nafasi ambazo Watanzania wana ujuzi nazo.

Kazi ambazo wengi hawana uwezo nazo, hasa kutokana na tatizo la lugha, amesema “itabidi ziende kwa wageni lakini kwa idadi maalum.”

“Kinachoweza kutuangusha ni endapo uhamiaji hawatakuwa wakali mipakani, au ukaingia ushawishi wa rushwa…mgeni  anaweza kuingia na kupata vibali kwa thumni,” amesema.

Pia mbunge huyo ana wasiwasi na jiografia ya nchi, kwa kuwa Tanzania ndiyo pekee inayopakana na nchi zote nne za Afrika Mashariki – Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya, hivyo wageni wanaweza kuingia kirahisi kupitia kila kona.

Kimbisa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini, kabla ya kuwania ubunge huo aliwahi kuwa meya wa jiji la Dar es Salaam kati ya 2005 na 2010.

Pamoja na changamoto za nafasi hiyo, anajivunia mambo kadhaa, hasa kwa “kuliweka jiji hilo katika ramani ya dunia”.

“Niliwezesha Jiji la Dar es Salaam kuwa na mahusiano na kutiliana saini mkataba wa ushirikiano na jiji la Hamburg la Ujerumani.

Mkataba huo umewezesha taasisi kama Bandari ya Dar es Salaam, Kikosi cha Zimamoto, Chuo Kikuu cha Ardhi na Mamlaka ya Maji Dawasco na Dawasa kushirikiana na mamlaka kama hizo huko Hamburg,” amesema.

Pia, ametamba kufanikisha ushirikiano kati ya Dar na jiji la Chan Zoo nchini China. Ushirikiano huu ulizaa msaada wa pikipiki zaidi ya 100 kwa madiwani wa Dar es Salaam ili kurahisisha usafiri katika kata zao.

Kimbisa pia anajivunia jengo la wamachinga maarufu kama Machinga Complex, ambalo licha ya kukamilika miaka kadhaa iliyopita hadi leo halijaanza kutumika.

“Mimi nilibuni na kujenga jengo, kuhusu uendeshaji, hilo usiniulize. Hiyo ni kazi ya watu wengine. Nilijenga jengo hilo kusaidia watu maskini, sababu yoyote inayotolewa ya kuwapa matajiri inanisononesha. Na ikitokea hivyo nitaumia sana,” amesema.

Ameongeza, “Hawa wafanyabiashara wakubwa wanaweza kwenda Kariakoo, pale kukodi chumba kimoja ni zaidi ya Sh. 1 milioni, hawa wadogo nani anaweza kulipa milioni moja? Kushindwa kulitawala tu jengo iwe sababu ya kuwapa watu wakubwa! Inaumiza.”

Kuhusu nini kifanyike ili jengo hilo liwasaidie walengwa, Kimbisa amesema: “Kinachotakiwa ni kazi ya menejimenti, pale hatukuweka kituo cha daladala, hatukuweka vivutio wala miundombinu mingine, haya yakirekebishwa jengo litaweza kufanya kazi.”

Anasemaje kuhusu mradi wa mabasi yaendayo kasi? “Tulipoingia madarakani tayari mradi ulikuwepo na baadaye uliundiwa mamlaka yake inayojitegemea, hivyo Halmashauri ya Jiji haikuendelea nao tena.

Je, machinjio ya kisasa yalishindikana na pesa kupotea? “Huu mradi sisi tulipoingia madarakani pia tuliukuta. Ulianzishwa kipindi cha mwenzangu Sykes (Meya mstaafu, Kleist). Uliundiwa bodi yake inayojitegemea chini ya Idd Simba, sisi tulichofanya ni kushtuka kuona pamoja na halmashauri kuingiza fedha hakukuwa na kitu kinachoendelea.”

“Kwa hiyo tuliposhtuka, manispaa zote tatu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tukaacha kuingiza fedha, hicho ndicho tulichofanya,” alisema bila kufafanua.

Katika maisha ya siasa, Kimbisa anakanusha taarifa zilizozagaa kuwa alikosa ubunge wa Dodoma Mjini kwa kile kinachoelezwa kuwa “nabii hakubaliki nyumbani kwao.”

“Hili si kweli. Mimi Dodoma nakubalika sana, na nilichaguliwa kwa kura nyingi, lakini kuna mtendaji mmoja wa CCM mkoa wa Dodoma hakutaka niwe mbunge akachakachua kura za maoni,” amesema.

Amesema kigogo huyo kabla ya “kuiba” kura zake, alimfuata na kumhoji kwa nini hakugombea nyumbani kwao Kondoa badala yake akaomba kugombea Dodoma Mjini.

“Hili mimi lilinishangaza, nyumbani kwangu mimi ni Tanzania, iweje kiongozi wa chama ananiuliza kwa nini sikugombea ‘nyumbani Kondoa?’ Nilikata rufaa, haikusikilizwa lakini hayo yamepita tugange yajayo…”

Kimbisa amesema, “Sijutii kuukosa ubunge wa Dodoma, lakini naamini mambo yote hutolewa na Mungu, nilinyimwa kuwania ubunge wa Dodoma sasa nimepata wa Afrika Mashariki, namshukuru Mungu.”

Kuhusu hali ya kisiasa ndani ya CCM na serikali yake, amesema “bado ni shwari, lakini kuna moshi unafuka…na popote moshi ukifuka, inabidi kuuzima mapema kabla haujageuka kuwa moto.”

Kimbisa ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, aliwahi kufanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje, diwani wa Kivukoni na Mwenyekiti wa Food Security Afrika.

0
No votes yet