Kimbunga CHADEMA chagusa mfupa wa CCM


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

MOJA ya agenda kubwa katika vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma ilikuwa kuhusu ughali wa bei za vyakula na ugumu wa maisha unaowakabili Watanzania.

Agenda nyingine katika vikao hivyo vilivyomalizika juzi ni hali ya kisiasa na mchakato wa katiba mpya.

Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema, "…kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakilalamika hali ngumu ya maisha na kupanda kwa bei ya vyakula.”

Ameongeza, “…NEC itapata taarifa ya serikali kuona hali ikoje na kuangalia nini kifanyike kupunguza au kuondokana kabisa na hali hiyo.”

Suala la ughali wa bei za vyakula na ugumu wa maisha kwa wananchi limekuwa kubwa na sugu. Hatimaye limeilazimisha CCM kulijadili na kulitolea kauli tofauti na siku za nyuma.

CCM imelipa kisogo kwa muda mrefu. Imekuwa ikichaguliwa tangu mwaka 1995 ulipofanyika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, lakini wanaoichagua hawajapata unafuu wa maisha.

Katika uchaguzi mkuu wa 2005 CCM iliweka ahadi rasmi ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania” ambayo ilivuta wananchi na kuichagua kwa kishindo. Hadi sasa miaka saba baadaye, hawajaona “asali wala maziwa” waliyoahidiwa.

Kwa mfano, bei ya sukari imepanda kutoka Sh. 600 mwaka 2005 hadi Sh. 3,000 sasa. Unga uliokuwa unauzwa Sh. 300 sasa ni Sh. 1,200. Mchele uliokuwa unauzwa kati ya Sh. 800 na 1,000 sasa huupati hadi utioa Sh. 2,800 hadi 3,000.

Badala ya kushughulikia matatizo haya, chama hicho kikongwe, kimekuwa kikibadili tu kauli, mara nguvu mpya, baadaye nguvu zaidi ili kufuta ahadi ya maisha bora, na kuifanya isomeke “maisha bora yataletwa na  Watanzania wenyewe, si kuisubiri serikali.”

Pamoja na kaulimbiu tamu tamu zisizoleta unafuu, hali ya wananchi imezidi kuwa ngumu. Mfumo wa bei umefikia hatua ya kutisha na hakuna dalili zozote za mabadiliko ndani ya muda mfupi.

Hii ndiyo fimbo pekee ambayo vyama vya upinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), vimetumia kuichapa CCM hadi ikalainika.

Kwa kutumia fimbo hii, CHADEMA kimefanikiwa kuwafafanuliwa wananchi, ni jinsi gani ugumu wa maisha wanaopambana nao unavyohusiana na udhaifu wa chama kinachotawala, CCM.

Viongozi wa CHADEMA chini ya mwenyekiti Freeman Mbowe na katibu mkuu, Dk. Willibrod Slaa katika maandamano na mikutano ya uhamasishaji (Operesheni Sangara), wamefafanua jinsi CCM inavyolea mafisadi na kuukumbatia ufisadi.

Hata kwa uchache wao, wabunge wa CHADEMA na baadhi ya vyama vya upinzani wameonyesha uwezo wao bungeni katika kutetea wananchi dhidi ya umaskini na ugumu wa maisha unaowakabili; wenzao wa CCM wameonyesha umahiri wa kutetea maovu na matumizi mabaya ya serikali.

Wapinzani wamefafanua jinsi, CCM yenye kumiliki serikali, ilivyoshindwa kutekeleza utitiri wa ahadi zake kwa wananchi. Wameonyeshwa jinsi fedha za umma zinazopukutika kwa ufisadi badala ya kuwaletea maendeleo na maisha bora waliyoahidiwa.

Watanzania wamegundua kuwa mabilioni ya shilingi wanayokamuliwa katika kodi ili yawaletee maendeleo, yanaishia kwenye matumbo ya wachache kwa mtindo wa posho, wizi katika mikataba na ubadhirifu.

Wameona wabunge wa CHADEMA ndio wanapinga posho, wale wa CCM wanazishabikia. Wameanza kuwaamini na kujiunga nao mamia kwa maelfu. Ulianza kama upepo sasa ni kimbunga.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) imetia chumvi kwenye kidonda. Imeonyesha kuwa kuna “mchwa” wa kutisha serikali unaoguguna fedha za umma. Imejadiliwa kwa kina bungeni na kueleweka.

Wananchi wameshuhudia jinsi wabunge wa upinzani isipokuwa John Cheyo wa UDP walivyotia saini kumwondoa waziri mkuu au la, rais awatimue mawaziri wanaotuhumiwa kwa ufisadi;  wameona wabunge watano tu wa CCM wakijitokeza kutia saini kati ya 258 walioko katika bunge.

Wabunge 253 wa CCM walikataa kumshinikiza waziri mkuu kuwawajibisha mawaziri wanaotuhumiwa kufuja fedha za umma. Wamekataa kupambana na ufisadi. Wanataka wananchi waendelee kuwa maskini.

Kwa tafsiri hii, ndio kisa wabunge wa CCM waliokubali kutia saini azimio la Zitto Kabwe la kutaka waziri mkuu ang’oke wanapokewa majimboni kwao kwa bashasha na maandamano.

Ushujaa wa wabunge hao watano wa CCM – Deo Filikunjombe (Ludewa), Nimrod Mkono (Musoma Vijijini), Ester Bulaya (Viti Maalum), Kangi Alphaxard Lugola na Ally Mohamed Keisy (Nkasi) ndani ya chama kisichokuwa tayari kupinga ufisadi, ndio kisa cha kutishiwa na uongozi wa chama.

Vitisho hivi ni ishara kuwa viongozi wa CCM waliowatisha wabunge hao hawakufurahishwa na hatua yao ya kushinikiza watuhumiwa wa wizi, ufisadi na ubadhirifu kuwajibishwa.

Hata pale CCM ilipojitutumua na kutaka kuwatimua wanachama wake wenye tuhuma za ufisadi, imeshindwa. Badala  yake ikaanza kuwabembeleza watuhumiwa wajiondoe wenyewe. Wanaokataa hawaguswi na yeyote.

Hii pia ni ishara kuwa CCM haijawa tayari kuukataa ufisadi na mambo yake yote. Haijawa tayari kusimamia mali na fedha za umma ili zitumike kwa usahihi na kuwaondolea wananchi umasikini.

Hoja za wapinzani, zimewafumbua macho wananchi. wamebaini kuwa hata ile sera ya Kilimo Kwanza ni kiinimacho. Wamepata taarifa za uhakika kwamba yale matrekta ya power tiller yameshindwa kuhimili ardhi ya Tanzania, na mengi yameegeshwa kwa ajili ya maonyesho.

Wananchi kupitia wapinzani wamefahamu kuwa hata ardhi ambayo ilikuwa kimbilio lao la mwisho imetapanywa kwa walowezi kwa lugha ya uwekezaji. Umma umeelewa kuwa walowezi hawa wanalipia Sh. 200 kwa hekta moja.

Mtu anayekodi ardhi kwa miaka 33 au 66 au 99 na kulipia Sh. 200 kwa kila hekta kwa mwaka ni sawa na kumpatia bure ardhi ya Watanzania. Hivi baada ya muda huo kumalizika nani atakuwa akisubiri  kuhakiki kama ardhi hiyo imerejeshwa kwa  wananchi au la.

Wakati wa kampeni za urais, Rais Kikwete aliviita vyama vya upinzani, kikikwemo CHADEMA, kuwa ni vyama vya msimu. Sasa mambo yamebadilika, vimekuwa vyama vya kudumu vinavyotoa agenda na chama tawala kinatekeleza.

Wimbi la CHADEMA ambalo limeanza kama upepo sasa limegeuka kimbunga na kuitikisa CCM. CCM imeona haina tena mbadala, bali kuyarudia matatizo ya wananchi na kuanza kuyazungumza badala ya kuyapa kisogo.

CCM inadhani kuyazungumza tu kutakisaidia, hata kisipoyashughulikia. Kimesahau kuwa Watanzania wa zamani si wa leo, ambao wamekwishafunguka macho na masikio. Wanaona, wanasikia na wanachukua hatua.

Kuhusu agenda ya mabadiliko ya katiba imeripotiwa kwamba shinikizo la wananchi kutaka mgombea binafsi nalo limeilainisha CCM.

Habari za ndani ya vikao hivyo, zilieleza kwamba chama hicho hatimaye kimewataka wanachama wake kujiandaa kisaikolojia kukabaliana na wagombea hao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Suala hilo limekuwa linapingwa na CCM pekee, lakini kwa shinikizo la sasa haina tena namna ya kulikwepa wakati wa mabadiliko ya katiba.

Hata Mwalimu Julius Nyerere mnamo mwaka 1995, aliweka bayana msimamo wake ambao umebaki kama wosia:

Alisema, “…mimi nadhani sheria imekosea kuzuia wagombea binafsi. Hili jambo limekosewa ni la msingi. Ndiyo maana napenda kulisema ni la msingi, linahusu haki yangu na yako ya kupiga kura na kupigiwa kura. Hii ni haki ya uraia.”

Kamati iliyoundwa na chama hicho kuangalia jinsi inavyoweza kuwasilisha maoni yake katika Tume ya Katiba, imeweka bayana kwamba umefika muda wa kuondokana na hofu ya kupoteza wanachama watakaoshindwa katika kura za maoni.

Kamati hiyo, iliyoongozwa na Abdulrahman Kinana, pia imedokeza msimamo mpya wa CCM wa  kukubali agenda za wapinzani za kuwa na muungano wa Serikali tatu – Shirikisho, Tanganyika na Zanzibar au kubaki na Serikali mbili za sasa.

Muundo wa serikali tatu ni hoja ya vyama vya upinzani, vikiwamo CHADEMA na CUF. Hatua ya wazo hilo kuchukuliwa na kuwekwa mezani kwa CCM ni ishara nyingine kuwa kimbunga kimeitikisa. Imetikisika.

Mbali na agenda hizo, katika hoja ya hali ya kisiasa, suala la maelfu ya wanachama wa CCM wanaohamia CHADEMA lilichukua nafasi.

Awali, viongozi walionekana kubeza kimbunga cha wanachama wake kuhamia CHADEMA.

Nnauye amekaririwa mara kadhaa akisema wanaohama ni watuhumiwa wa ufisadi, mara ohoo, wanajivua gamba, lakini ukweli unabaki kuwa wanahama ni wengi, na wanatishia uhai wa chama. Na wahamiaji hawa si upepo tena. Ni kimbunga.

0756 346175
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: