Kinana anatekea maji kwenye pakacha, halijai


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version
Gumzo
Abdulrahman Kinana

KAULI ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana kwamba chama chake hakihusiki na ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi uliofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeibua mengi.

Kwanza, kwa mara ya kwanza viongozi wa CCM wamejitokeza hadharani kukana kuhusika na wizi ndani ya BoT. Katika hili, Kinana anasema, “CHADEMA wametengeneza uzushi na kebehi badala ya kutoa sera.”

Pili, Kinana anasema, viongozi wa upinzani, walioshusha tuhuma hizo wamekiuka maadili ya vyama vya siasa yanayokataza matusi.

Katika hili, Kinana alisema, “Ni vema kutumia lugha isiyo ya matusi ili hata baada ya uchaguzi viongozi waendelee kuongea pamoja badala ya kukwepana.”

Kinana ametoa kauli hiyo Jumapili iliyopita katika mkutano wake na waandishi wa habari, ofisi ndogo ya CCM, Lumumba Dar es Salaam. Alikuwa akijibu kile kinachoitwa, “kombora” lililoshushwa na mwasisi wa mageuzi nchini, Mabere Marando.

Akihutubia maelfu ya wanachama na wapenzi wa chama chake katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, Marando alisema CCM imeshindwa kupambana na rushwa kuwa baadhi ya viongozi wakuu wa serikali walihusika kwenye kashfa ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

Alisema wengi walioshiriki katika wizi huo hawajafikishwa mahakamani. Ni kwa sababu ya kulindwa na vyombo vya dola.

Kimsingi kauli ya Kinana imelenga mambo mawili makubwa: Kwanza, kutaka kuaminisha wananchi kuwa CCM inasingiziwa, inapakaziwa na inatuhumiwa uwongo na bila sababu za msingi.

Lakini pili, Kinana na chama chake wanataka kuudanganya ulimwengu kuwa CCM kinafanya kampeni za kistaarabu.

Tuanze na hili la kwanza; kwamba Kinana anasema, CCM haihusiki na wizi wa fedha za EPA.

Kila mwenye akili timamu anajua kuwa chama hiki na viongozi wake, hawawezi kukwepa tuhuma, shutuma na lawama kwamba walihusika na ukwapuaji uliofanyika. Hata Kinana analijua vema hili.

Anajua kuwa kwa zaidi ya miaka minne wabunge wa upinzani na wale wa chama chake, wamekuwa wakiwatuhumu viongozi wao kuhusika na wizi ndani ya BoT; hakuna mahali popote ambapo viongozi wa CCM na serikali yake walijitokeza hadharani kukana tuhuma hizo.

Hata ndani ya Kamati ya Rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi, iliyoundwa na chama chake kutafuta suluhu ya migogoro ndani ya Bunge na katika chama, suala la CCM kujinufaisha na fedha za EPA liliibuka.

Mjadala ulipopamba moto, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba alijitokeza na kukaripia wanaotuhumu. Akiongea kwa sauti iliyojaa mipasho, waziri Simba alimtuhumu Anne Kilango Malecela, kuwa ni miongoni mwa walionufaika na fedha za EPA.

Alisema Kilango alinufaika na fedha hizo kupitia kwa mfanyabiashara Jeetu Patel aliyekuwa anafadhili kampeni za mume wake, John Samwel Malecela.

Kauli ya Simba ilitokana na hoja kadhaa zilizokuwa zinajengwa na baadhi ya wabunge akiwamo Kilango, kwamba serikali imeshindwa kushughulikia ufisadi wa EPA kwa sababu baadhi ya fedha zilizoibwa zilinufisha chama chao.

Wabunge hao waliokuwa wamepachikwa jina la “Makamanda wa ufisadi,” walilenga mabilioni ya fedha yaliokwapuliwa na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited. Kampuni ya Kagoda ilichota zaidi ya Sh. 40 bilioni kupitia BoT.

Alisema, “Mimi ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri. Hata TAKUKURU – Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - iko chini yangu. Idara ya usalama wa taifa iko pale kwangu. Mlango wangu uko karibu na lango la rais. Nafahamu kilichotendeka.”

Aliongeza, “Nafahamu kwamba baadhi ya fedha za EPA ambazo leo Kilango anatuhumu zimetunufaisha baadhi yetu, zilinufaisha hata kampeni ya mumewe.”

Hakuna mahali popote ambapo CCM ilikana madai ya Simba.

Pamoja na kwamba Kinana alikuwa mjumbe katika Kamati ya Mwinyi, na kwamba yeye na katibu mkuu wake, Yusuph Makamba walihudhuria mkutano uliotuhumu Kilango, lakini hawakujitokeza kukana kauli ya Simba.

Hii ni kwa sababu, Kinana alijua kuwa yeye na Simba katika kujua siri za serikali, wako tofauti. Mwenzake ni waziri anayehitajika kila wakati katika kazi za kuendesha serikali, yeye huwa anatafutwa wakati wa kampeni tu.

Aidha, Kinana anajua kuwa tofauti na waziri Simba anayehudhuria vikao vya baraza la mawaziri, anayeshiriki mipango ya uendeshaji wa serikali, yeye hulazimika kusubiri ripoti ifikishwe kwenye vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashari Kuu (NEC). Isipoletwa basi!

Pili, tofauti na Sophia Simba, Kinana hana ubavu wa kusoma mafaili ya watuhumiwa wa ufisadi wanaochunguzwa na Takukuru. Hivyo basi, hawezi kujua nani ameiba nini, wapi na kwa kushirikiana na nani?

Hawezi kujua kwa ufasaha kwamba Jeetu alisema nini katika kiapo chake mbele ya Kamati ya Rais ambayo mtendaji mkuu wa Takukuru, Edward Hoseah alikuwa mjumbe.

Hafahamu kwa undani kwa nini Jeetu amegoma kurejesha baadhi ya fedha zilizokwapuliwa na nini ameegemea.

Wala Kinana hakuwa miongoni mwa wajumbe waliohudhuria kikao kati ya Rais Benjamin Mkapa wakati huo, Rostam Aziz na Gavana wa BoT, Daud Ballali kama ambavyo Rostam alinukuliwa na wakili wa mahakama kuu, Bhyidinka Sanze katika hati yake ya kiapo alichowasilisha mbele ya Kamati ya Rais.

Tatu, mwaka 2005, tofauti na Sophia Simba aliyekuwa mjumbe wa Kamati ya ushindi ya Kikwete, chini ya kile kinachoitwa, “wana-mtandao,” Kinana alikuwa nje ya kundi hilo. Yeye alikuwa kambi ya Malecela.

Ni mtandao huu unaotuhumiwa kuchota fedha BoT na baadhi kuzitumia kufanikisha kampeni za uchaguzi.

Lakini hata pale alipoteuliwa kuwa Meneja wa Kampeni za Kikwete, mtandao uliokuwa unaongozwa na Edward Lowassa ulihamishia shughuli zote za kampeni nje ya ofisi za chama.

Kuna taarifa kwamba ni Kinana huyuhuyu anayedaiwa kujiondoa katika kazi hiyo kimyakimya, baada ya kutofurahishwa na jinsi fedha za kampeni zilivyokuwa zikitafutwa.

Katika mazingira haya, Kinana hawezi kueleweka wala kauli zake kukubalika. Anatekea maji kwenye pakacha. Halitajaa. Anapaswa kujilaumu binafsi na kulaumu makada wenzake katika chama.

0
Your rating: None Average: 2.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: