Kofi Annan anaogopa ya Dk. Salim


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 21 July 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Waraka wa Wiki
Kofi Atta Annan

KAMA wewe ni mwanamume na unatoka katika kabila la Fanti nchini Ghana na ikatokea kwamba umezaliwa siku ya Ijumaa, utaitwa Kofi.

Na kama wewe ni mtoto wa nne wa kiume kuzaliwa kwenye familia yako (kama umetanguliwa na kaka zako watatu), basi wewe ujue utaitwa Annan. Iwapo umezaliwa pacha, utaitwa Atta. Na hapo ndipo linapokuja jina la Kofi Atta Annan.

Lakini kama ulizaliwa Jumamosi, jina lako litakuwa Kwame. Na kama wewe ni mtoto wa tisa kuzaliwa kwenye familia yenu, jina lako la pili litakuwa Nkrumah. Kwa hiyo utaitwa Kwame Nkrumah.

Na kwa kawaida, wafalme na machifu wa kabila hili huwa hawaruhusiwi kutahiriwa. Hii ni kwa sababu kama watatahiriwa, watatokwa damu na kiimani tukio hilo (kutokwa damu) ni uchuro kwao.

Katibu Mkuu aliyepita wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Atta Annan, ni mtoto wa chifu wa kabila la Fanti. Mara baada ya kumaliza kipindi chake cha ukatibu mkuu mwaka 2006, wengi walitarajia kwamba angewania urais wa Ghana katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo mwaka juzi.

Kinyume cha matarajio ya wengi, Annan amekaa kimya kabisa tangu aliporejea Ghana mwaka 2007. Annan hachangii katika mijadala ya kisiasa na hili limezua maswali mengi hapa.

Akiandika katika gazeti la Mail &Guardian la Afrika Kusini hivi karibuni, mwandishi wa habari mkongwe wa Ghana, Cameron Duodu, alisema yafuatayo kuhusu Annan; “Kofi Annan, pengine ndiye rais bora kabisa ambaye Ghana haijawahi kuwa naye.”

Katibu Mkuu wa nne wa UN, Kurt Waldheim (1972-1981), alikuja kuwa rais wa nchi yake, Austria kati ya mwaka 1986 hadi mwaka 1992 baada ya kuwa amemaliza muda wake.

Kwa hiyo kama Annan angeamua kuwania nafasi hiyo, hakuna ambaye angemshangaa. Kati ya wanasiasa wote wa Ghana hivi sasa, hakuna ambaye anafikia kariba ya Annan. Kimsingi, raia wote wa hapa wanasema ni Nkrumah pekee ndiye anayeweza kuwekwa kwenye daraja moja na katibu mkuu mstaafu huyu.

Inaeleweka Annan, raia wa Ghana, ndiye mtu anayejulikana zaidi kuliko mwingine yeyote duniani. Ana marafiki ambao wanaweza kumchangia fedha zozote ili awanie urais.

Pamoja na sifa hizo zote, Annan amekataa kutia mguu katika siasa za ndani ya Ghana. Swali la kujiuliza hapa ni kwa nini?

Jarida la Newsweek la hapa, lilimkariri mmojawapo wa rafiki zake tangu ujanani, Berihun Asfaw, raia wa Ethiopia, akisema kwamba mwanadiplomasia huyo alipanga kurejea nchini kwake na kuwa mwanasiasa mnamo mwaka 1972.

Wakati huo, Kofi tayari alikuwa mfanyakazi wa UN. Serikali iliyokuwapo madarakani ilikuwa chini ya Waziri Mkuu, Dk. Kofi Busia, ambaye alikuwa mjomba wa Annan.

Hata hivyo, mara baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Kanali Ignatius Acheampong yaliyofanyika mkesha wa mwaka mpya wa 1972, ndoto zote za Annan kurejea nchini kwake na kufanya siasa zikatoweka.

Tangu wakati huo, Annan amejitenga kabisa na siasa za Ghana. Yapo pia maswali kuhusu Annan ni mtu anayependa siasa za namna gani. Zile za Nkrumah za kijamaa au za kibepari.

Kwa mujibu wa Asfaw, ni vigumu kufahamu ni mrengo upi wa kisiasa ambao Annan anaufuata. Siku zote amekuwa akifahamika kuwa kipenzi cha Wamarekani, lakini Meles Zenawi, Waziri Mkuu wa Ethiopia anayedaiwa kupenda usoshalisti, ni miongoni mwa marafiki zake wa karibu.

Hata hivyo, Annan anadaiwa kutokumpenda Nkrumah. Kuna dhana mbili zinazotumika kuonyesha hili. Kwanza kuna mazungumzo rasmi ambayo aliwahi kunukuliwa katika miaka ya sabini akisema siasa za kipenzi huyo wa Afrika ziliharibu uchumi wa Ghana.

Pia, utawala huo wa mjomba wake ulikuja mara baada ya kupinduliwa kwa Nkrumah. Ingawa wote wawili walitoka katika jamii ya Asante, Nkrumah anatoka katika kabila la Nzima wakati Annan ni Mfanti.

Makabila haya mawili yana upinzani wa jadi ambao umehamia hadi katika siasa. Wengi wa wafuasi wa chama cha Nkrumah cha CPP wanatoka katika eneo la kabila lake lakini huwa hawashindi kwenye maeneo ambako watu wa kabila la Fanti wako kwa wingi.

Sababu hizi mbili zinaelezwa kuwa msingi wa maelezo ya kwa nini Kofi hakuwa mfuasi wa Kwame. Lakini hapa pia ndipo linappokuja tatizo lingine kubwa kwa Annan.

Kwamba wengi wa Waghana bado wanamwona Nkrumah kama shujaa wao. Mtu kama Annan anaonekana kuwa kama kibaraka wa Marekani na ni rahisi kwa wapinzani wake kusema yeye ndiye aliyechonga ‘dili’ la kumuua Nkrumah.

Kwa vyovyote vile hili litakuwa tusi kubwa sana kwake. Heshima yake yote aliyoijenga kwenye utumishi wa kutukuka duniani itakwisha kwa sababu ya madai kama haya.

Itakuwa sawa na namna Dk. Waldheim ambaye aliporejea Austria alihusishwa na Vita Kuu ya II ya Dunia. Vile vile itakuwa sawa na namna Dk. Salim Ahmed Salim, alipohusishwa na mambo ya kuudhi wakati alipojitokeza kuwania urais mwaka 2005 nchini. Alikuwa muathirika wa siasa za majitaka kama hizi.

Kwa upande mwingine kuna wanaodhani kwamba tatizo la Annan ni mahali pa kujiunga ili awanie urais. Yeye ni rafiki binafsi wa rais aliyepita, John Agyekum Kuffour, na wa sasa, John Atta Mills.

Kama ataamua kwenda kokote, ni wazi atakuwa ameharibu uhusiano wake mzuri alioujenga kwa muda mrefu na wanasiasa na wafuasi wa pande zote za kisiasa nchini kwake.

Hili nalo linamtisha. Kwamba kutoka kuwa mtu anayeheshimiwa na watu wote na kubaki kuwa mwanasiasa wa chama kimoja. Hapa napo Kofi anaona ugumu.

Ili aweze kuwa rais wa Ghana, ni lazima Kofi Annan akubali kujeruhiwa. Ni lazima akubali kutokwa damu. Lakini, ni chifu gani wa kabila la Fanti atakubali kutokwa damu?

Labda historia ya Annan itakuja kuwa kama ya Dk. Salim huko tuendako; Rais Bora Ambaye Nchi Husika Haikupata Kuwa Naye”

0
0
Your rating: None