Kongo-DRC yanukia mabadiliko kisiasa


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 02 November 2011

Printer-friendly version
Etienne Tshisekedi kuwa ‘Mokonzi?’
Abeba vigogo wakuu katika siasa
Kabila: Kufa na kupona kubakia ikulu

NI mtafutano. Ni piga nikupige katika siasa za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo – DRC.

Yote ni katika mbio za kwenda uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi huu. Swali ambalo wengi wanajiuliza ni: Je, Joseph Kabila atapenya tena?

Ni swali zito. Mpinzani wake mkuu ni Etienne Tshisekedi. Tayari amebabua nchi nzima kwa kauli za kutaka mabadiliko na kuondokana na utawala anaobeza na kuuita kuwa si wa kidemokrasia.

Kampeni rasmi za uchaguzi zilianza nchini kote DRC, Alhamisi iliyopita huku Tshisekedi akiwa ziarani Afrika Kusini. Wachunguzi wanasema “anatafuta kuungwa mkono katika hali yoyote ile itakayojitokeza.”

Mara hii upinzani umevaa khaki. Unataka kumwondoa Rais Kabila ambaye wanamtuhumu kutokuwa raia wa DRC; lakini pia kwa kushindwa kuleta “maelewano” katika nchi kubwa yenye madini mengi kuliko zote barani Afrika.

Tayari vyama 26 vimeahidi kusimama pamoja na Tshisekedi, mpigania demokrasi mkubwa tangu enzi za dikiteta Mobutu Sese Seko.

Wanasiasa wanaompinga Kabila aliyeingia madarakani mwaka 2003 na baadaye kushinda uchaguzi 2006, wanasema wao na wananchi wa Kongo, wanatafuta “Mokonzi wa Republíki;” au Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kongo.

Baadhi ya wanaomuunga mkono Tshisekedi ni watu mashuhuri na wenye hadhi katika Kongo. Wanasema sharti DRC iongozwe na watu wanaofikiria kuijenga kiuchumi kwa kutumia hazina kubwa ya raslimali zake.

Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 79 na mwanasheria kitaaluma, ndiye anaongoza chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) – Umoja kwa ajili ya Demokrasi na Maendeleo ya Jamii.

Ana wafuasi wengi katika jiji la Kinshasa, makao makuu ya nchi. Anapendwa Katanga ambako ni ngome yake; Kasai, Mbujimai (Magharibi), Bandundu na mkoa wote wa Ikweta (Equator); majimbo yote ya Kivu Kaskazini na Kusini, na eneo kubwa la Mbandaka, Kaskazini mwa nchi.

Mshirika mwingine wa Tshisekedi ni Antipas Mbusa Nyamwisi, aliyezaliwa 15 Novemba 1959 katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Nyamwisi, mwanasiasa shujaa na kiongozi wa zamani wa kundi la waasi dhidi ya Serikali, ana wafuasi wengi katika jimbo hilo la nyumbani kwao, Mashariki mwa Kongo.

Alikuwa mmoja wa wanasiasa walioazimia kugombea urais katika uchaguzi wa 2006, lakini baadaye akajitoa na kumuunga mkono Rais Kabila.

Baada ya uchaguzi huo, Nyamwisi anayetoka Chama cha RCD-K-ML, aliteuliwa waziri wa mambo ya nje mpaka 2008. Tena aliteuliwa waziri wa serikali za mitaa, miji na mipango ya mikoa.

Mpaka sasa, taarifa za ndani ya DRC, zinadai kuwa Nyamwisi angali na askari wanaomtii. MwanaHALISI imeshindwa kuthibitisha madai hayo.

Kulingana na taarifa zilizopo, hata Jean-Pierre Bemba Gombo, mwanasiasa anayekabiliana na mashitaka ya “uhalifu wa kivita” katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), iliyoko The Hague, nchini Uholanzi, anamuunga mkono Tshisekedi.

Hata hivyo, nyumbani kwao Bemba angali keki. Anategemewa kama sehemu ya nguvu za kumtoa madarakani Rais Kabila.

Bemba, mzaliwa wa 4 Novemba 1962, anajivunia wafuasi jijini Kinshasa, Bandundu (Equator) na Gbadolite, mji wa nyumbani kwa dikteta Mobutu, ambaye alipoona upinzani umezidi, alikimbia nchi.

Mobutu alikimbilia Mei 1997 na kwenda kuishi nchini Morocco ambako alifia miezi minne baadaye. Alizikwa hukohuko kimyakimya.

Bemba alikuwa mmoja wa wanasiasa wanne walioteuliwa kushika umakamu wa rais katika serikali ya mpito iliyoundwa mwaka 2003 kwa makubaliano ya mkataba wa amani wa kumaliza vita. Alishika nafasi hiyo hadi Desemba 2006.

Anaongoza Movement for the Liberation of Congo (MLC), chama kilichotangulia kuwa kundi la waasi wakati wa vita.

Umaarufu wa Bemba unazidi kupaa na kivuli chake kinatosha kuwapa upinzani maelfu ya kura.

Kuna Dk. Albert Onawelho, mwenye umri wa miaka 72 na kiongozi wa Chama cha MNC-Lumumba (MNC-L), kilichoanzishwa na rais wa kwanza wa iliyokuwa Zaire huru, Patrice Lumumba.

Dk. Onawelho ambaye anaishi London, Uingereza, naye anamuunga mkono Tshisekedi. Ana wafuasi wengi jimbo la Kasai (Mashariki na Magharibi mwa Kongo); Wembo-Nyama ambako ni nyumbani kwa Lumumba, Kisangani na Kivu Kusini.

Mshirika mwingine wa Tshisekedi ni Roger Lumbala, mwanasiasa ambaye Julai mwaka huu, televisheni yake iliteketezwa kwa moto. Inadaiwa waliohusika na hujuma hiyo ni wafuasi wa chama cha Kabila cha PPRD – Parti de Peuple Pour la Reconstruction et la Democratie.

Lumbala ana ngome jijini Kinshasa, majimbo yote mawili ya Kasai anakotoka, Bandundu, Gbadolite, Katanga na Mbujimayi.

Mwanasiasa mwingine anayepingana na Rais Kabila na kujiunga na kambi ya Tshisekedi, ni Joseph Olenghankoy Mukundji.

Huyu anaongoza kundi la FONUS ambalo kupitia kwake, Mukundji aliwahi kumwambia dikteta Mobutu kuwa, “…wewe ni betri iliyokwisha nguvu na kamwe haitawaka tena.”

Mshirika mwingine anayetia nguvu kwa Tshisekedi ni Songoro Nuru, kanali mkufunzi wa Jeshi la DRC, ambaye pia amekuwa mwelekezaji mkuu kwa majeshi ya Umoja wa Mataifa (MONUC).

Songoro aliacha kazi jeshini mapema mwaka huu. Tarehe 7 Juni alimwandikia Rais Kabila akisema, “kwa heshima na taadhima, naacha kazi yangu kwa kuwa nimeitwa na wananchi wa jimbo langu la Katanga ili nikawatumikie.”

Kanali Songoro hujivunia umaarufu katika jimbo la Katanga ambako taarifa zinasema, kama kuna mahali ambako Rais Kabila hajisikii kwenda mara kwa mara nchini DRC, basi ni katika jimbo la Katanga.

Askari huyu ana mvuto wa pekee pia kwa wananchi wa Kongo. Wakati mwingi hujadili suala la uhuru wa Katanga na kuondoa RDC katika makucha ya kibeberu.

Katika mazingira haya, Rais Kabila ana kibarua kigumu. Muungano wa vyama na watu mashuhuri lazima utikise mizizi ya chama chake cha PRP.

Utajiri wa Kongo, wapinzani wanadai, umekuwa ukinufaisha mataifa na kampuni za nje na kuwaacha wananchi katika dhiki.

Kuna kejeli isemayo “mungu” alikuwa anagawa madini duniani kote baada ya kuiumba. Kila nchi ilipewa. Lakini alipofika Kongo kapu lake likazibuka kiunoni na madini yote kumwagika Kongo.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema karibu wapinzani wote katika vyama 26 vinavyomuunga mkono Tshisekedi, wana mwelekeo wa kupigania demokrasi, utawala wa sheria na uhuru wa maoni.

Tshisekedi ana nafasi kubwa ya kumpiku Kabila na kwa kuzingatia nguvu hizo haitakuwa ajabu iwapo ataibuka mshindi.

“Kongo imevuja damu kwa muda mrefu,” anasema Venance Muliki, Katibu Mkuu wa MNC-Lumumba.

Aliiambia MwanaHALISI kwa njia ya simu akiwa mjini Ujiji, mkoani Kigoma hivi karibuni: “…tunataka kiongozi anayeamini kuwa Kongo ni mama, Kongo ni baba na yuko tayari hata kuifia. Siyo wapitanjia au watawala maslahi.”

Ajenda kuu za uchaguzi DRC zimeelekezwa kwenye kukataa kutawaliwa kisiasa na kiuchumi na watu kutoka nje; kuondoa majeshi yote ya kigeni na kuwa na kujenga uchumi.

Jingine ni kujenga umoja kitaifa ili wananchi waweze kuishi kwa amani na utulivu, jambo ambalo limewashinda Mobutu, Laurent Kabila na sasa, Hypolite Kanambe Joseph “Kabila.”

0
No votes yet