Kufunika Kagoda ni kuandaa janga


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 07 September 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

WAZIRI wa Fedha na Uchumi wa zamani, Zakia Meghji, alipoahidi kwamba serikali ilikuwa imeridhia kufanywa kwa ukaguzi wa Akaunti ya Fedha za Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hakusema hivyo kwa tabasamu na bashasha, bali alilazimika kwa kuwa hakuwa na namna wala jinsi.

Hakuwa na jinsi kwa sababu serikali yetu ni ombaomba ambayo aghalab hupewa masharti kabla ya kurushiwa visenti kwenye bakuli lake. Ndivyo ilivyokuwa, wahisani ambao wamekuwa wanasaidia bajeti ya serikali waliitaka serikali kufanya ukaguzi wa EPA kwa sababu kwao ilikuwa ni matusi kuendelea kuisaidia Tanzania wakati ikilinda ‘wezi’ ambao walikwapua kiasi cha Sh. 133 bilioni kwa sababu wanazozijua wao.

EPA ulikuwa wizi wa kushirikisha vyombo vya dola; kuanzia uandikishaji wa kampuni, ufunguaji wa akaunti, uwasilishaji wa nyaraka BoT, na kwa kweli hata usimamizi wa BoT wenyewe chini ya Gavana anayedaiwa alifia ughaibuni, Daudi Ballali.

Meghji ama kwa kujua au kutokujua uzito na upana wa EPA, aliandika barua ya kutetea ukwapuaji huo, kwa kusikia tu ushauri wa kilaghai wa Ballali hadi aliposhituliwa na Katibu Mkuu wa Hazina, kwamba sehemu ya uporaji wa EPA ambazo zilikuwa zimechukuliwa na Kampuni ya Kagoda Agriculture kiasi cha Sh. 40 bilioni (dola za Marekani milioni 30) hazikuwa na uhusiano wowote na usalama wa nchi, hivyo alifuta barua ambayo alikuwa amewasilisha kwa kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya Deloitte & Touche kuhalalisha wizi huo.

Ingawa haijawahi kuelezwa rasmi, kisa cha Meghji kuachwa kwenye baraza la mawaziri lilioundwa baada ya kuvunjwa mwaka 2008 kufuatia sakata la Richmond , hisia zinasema kuwa kwa jinsi alivyoshughulikia suala la EPA alijiweka pabaya.

Tangu mwaka 2007 suala la EPA limepigiwa kelele nyingi mno, kuanzia ndani ya Bunge hadi nje; kuna sauti za wanaharaki, zipo za wanasiasa, lakini katika vyombo vya habari nako imekuwa habari ya kudumu. Kila kitambo kidogo inaibuka na vionjo vipya.

Kuna baadhi ya washirika wa wizi wa EPA wamefikishwa mahakamani, wengine kesi zao zimefikia ukomo na kuhukumiwa kifungo, kesi nyingine nyingi ziko katika hatua mbalimbali za kusikilizwa, lakini katika hizo hakuna inayohusu Kagoda.

Serikali na hata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wamesema kwa nyakati tofauti kuwa hawawajui wamiliki wa Kagoda, hivyo ni vigumu kuwashitaki.

Ingawa serikali inasema haiwajui wamiliki, fedha za Kagoda zilipitishwa benki, zilisambazwa kwa watu mbalimbali na wanajulikana, lakini bado serikali inasema haijui kitu kuhusu Kagoda.

Ni katika mazingira hayo, wiki iliyopita akaibuka mwanaharakati Msemakweli Kainerugaba akisema ana ushahidi wa Kagoda; akaandaa na kuwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) akitaka watuhumiwa wafikishwe mahakamani. Sakata hili bado linaendelea.

Walioko serikalini leo wanasahau kitu kimoja kwamba wizi wa EPA ulikuwa na utaendelea kuwa kosa la jinai. Kwa wanaojua sheria vizuri wanaelewa kuwa jinai haina ukomo, hata baada ya miaka mingapi kesi inaweza tu kufunguliwa ingawa muda ukipita sana inakuwa na ugumu wake.

Wiki iliyopita dunia ilishuhudia maamuzi magumu yaliyofanywa na watawala wa Chile kuamua kuufukua mwili wa Rais Salvador Allende aliyekufa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1973. Nia ya kufukua mwili wake ni kujibu swali moja ambalo limekuwa linawasumbua kwa takribani miaka 40 kwamba Rais huyo alijiua au aliuawa na majeshi ya Jenerali Agustino Pinochet.

Ingawa kulikuwa na taarifa ya daktari kwamba Allende alikuwa amejiua kwa kujipiga risasi kidevuni kwa kutumia bunduki aina ya AK 47 aliyokuwa amepewa na Rais wa Cuba, Fidel Castro, bado uchunguzi huru ulikuwa haujafanywa.

Wachile walikuwa wanataka suala hilo lifike mwisho kwa kufanya uchunguzi huru. Kwa hiyo mwili huo ulifukuliwa na kufikisha suala hilo mwisho.

Uchunguzi wa Allende ni mfano tu, ipo mifano mingi juu ya kesi zinazofufuliwa baada ya kupita kitambo kirefu; hii ya Chile ni baada ya takribani miaka 40.

Hata hivyo, imethibitika kwamba Rais huyo alijiua baada ya kuona mashambulizi ya waasi waliokuwa wanaongozwa na Pinochet yakizidi kuteka nchi na kusababisha mauaji makubwa ya raia.

Nimesema kwamba wiki iliyopita Msemakweli aliamua kuchukua jukumu ya kuandaa nyaraka mbalimbali kuhusu uchukuaji wa fedha hizo, zikiwamo za usajili wa kampuni, benki na nyingine ambazo ziliwasilishwa BoT, amewasilisha kwa DPP na zimepokewa na ameanza kushirikiana na vyombo vya dola, likiwamo Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa nia ya kutafuta kama kesi inaweza kufikishwa mahakamani dhidi ya wanaotajwa.

Kinachonisukuma kuzungumzia suala hili ni kitu kimoja tu, kwamba ni kujidanganya kufikiri kwamba kujaribu kutafuta njia za panya kuzuia suala la EPA lisimalizeke kisheria ni kuahirisha tatizo. Ni hatari. Hatari hii ni kubwa miaka ijayo kuliko leo.

Kwa nini nasema haya? Leo inawezekana kuna nguvu fulani za kuzuia kesi hii isifikishwe kwenye vyombo vya sheria. Ni kweli tupu leo hii wanaweza kuwa na nguvu ya kuzuia kesi hii, lakini swali la kujiuliza hizi nguvu watakuwa nazo hadi lini?

Mbili, serikali leo inaweza kuwa na mahusiano ‘mazuri’ nao ambayo yanaisukuma kuzuia kesi hii isifikishwe mahakamani; lakini ni vema waliokalia nafasi mbalimbali wakatambua kwamba nafasi hizo ni dhamana, kuna kesho, kuna keshokutwa, kuna kustaafu, lakini pia kuna uwezekano wa kubadilika kabisa kwa serikali na watawala kwa ujumla wao.

Jingine ambalo ni la umuhimu mkubwa katika sakata lote hili la Kagoda ni aibu ya utamaduni wa serikali yetu kuchukua hatua ya mambo pale tu inapopata shinikizo, ama za ndani au hata za nje. Kwangu huu ni udhaifu ambao si tu kuwa ni hatari kwa watawala waliopo bali hata kwa maswahiba wao pia.

Ningelikuwa na nafasi ya kushauri wahusika wa kadhia hii ningewashauri jambo moja tu, kwamba wajitokeze wapambane kwenye vyombo vya kisheria kwa kusikiliza kesi hii ili wakifanikiwa kushinda wasonge mbele, wakishindwa watumikie adhabu zao. Kwa njia hiyo suala lao litakuwa limefungwa, na watakuwa na uhakika na amani ndani ya nafasi zao sasa na daima.

Sitaki kuamini kwamba kuna njia yoyote ya kukimbia mkondo wa sheria itakayomhakikishia mtu usalama wake kama kuna jambo la kisheria ambalo halijashughulikiwa kisheria.

Kama Msemakweli leo amethubutu kuibuka na suala hili na kulipeleka alipolifikisha, hata kama vyombo vya serikali vitalikwepa jambo hili kwa hila au mbinu yoyote leo, hakika haiwasaidii watuhumiwa, ila wanawaandalia tu uzee mbaya; wanawajengea kesi mbaya na mahangaiko wakati wa umri mkubwa watakapokuwa wanastahili kupumzika ndipo wahangaike na kesi ambazo wangeweza kushughulika nazo sasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: