Kuhusu Kaseja, Kondic asidanganye Yanga


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version

UMESHIKA gazeti hili ulipendalo la MwanaHALISI. Unasoma makala hii. Aya ya tano tu za kwanza, fumba macho. Tafakari na vuta hisia juu ya kipa bora nchini Tanzania.

Rudisha kumbukumbu za miaka ya nyuma; chukua ya 1970. Kumbuka majina ya Omari Mahadhi bin Jabir, Athumani Mambosasa (wote marehemu) walioidakia timu ya Simba kabla ya kugeukia Elias Michael (marehemu) na Juma Pondamali “Mensah.”

Hata kama hukuwahi kuwaona dimbani wakizuia mashuti na kukupa burudani ya nguvu, kalamu za waandishi zinarejea historia zao.

Acha hao, jongea miaka ya nchani 1980 na 1990. Kumbuka Sahau Kambi, Rifat Said (marehemu), Idd Pazi “Father,” Mackenzie Ramadhani kabla ya Mohammed Mwameja na Joseph Katuba.

Baada ya zama za Mwameja na Steven Nemes kwisha, takafari tangu kuingia karne ya 21 ambayo leo ina miaka tisa, nani anaweza kuwa mfano bora wa hao ndani ya miaka 10 kufikia leo?

Labda tu iwapo utakuwa mnazi ndio utahangaika kumtafuta, lakini muangalie Juma Kaseja.

Kipa mwenye kasoro mbili tu; moja ikiwa tayari ameimaliza mwenyewe kiungwana kwa kuwa ‘ilielezwa’ ni ya kibinadamu.

Ukiacha umbile lake fupi (kasoro ninayolazimishwa na wadau wa soka kuiamini maana ndio maumbile yake), Kaseja alimtibua nyongo Kocha Mkuu wa timu ya taifa Tanzania (Taifa Stars), Marcio Maximo kwa kudaiwa kuwa alishangilia.

Mabao ‘ya kizembe’ aliyofungwa Ivo Mapunda, usiku wa 24 Machi 2007 dhidi ya Senegal (Simba wa Teranga) mjini Dakar, yalitosha kumfanya Kaseja apae, sababu inayodaiwa na wadau kuwa ndiyo iliyomtibua Mbrazili Maximo, ambaye kwa bahati mbaya hajapata kuithibitisha.

Kaseja akatiwa hatiani ni mtovu wa nidhamu kwa kuwa alikosa uzalendo mwaka huo ambao Tanzania ilikuwa inatafuta nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2008 zilizofanyika nchini Ghana.

Hadi niandikapo hapa, Kaseja hajaitwa timu ya taifa ingawa alijitokeza mbele ya waandishi na kuomba radhi kwa Maximo. Kwa utamaduni wa watu wa Tanzania, tayari alionyesha uungwana. Angesamehewa.

Awapo golini, Kaseja amethibitisha umahiri. Anawaacha hoi wanazi wa soka kuona mabao ya kizembe wanayofungwa Ivo, Farouk Ramadhan, Ally Mustapha “Barthez,” Deo “Dida” Mushi na kwa sasa, Shaaban Dihile.

Ukiacha dhana ya unazi wa kisoka wa Simba (Msimbazi) na Yanga (Jangwani), Watanzania wengi wanaokwenda uwanjani, huuliza: “Kaseja yuko wapi.” Ishara ya imani kutokana na uwezo wake.

Wenye macho wanaona. Wanakiri Kaseja ana akili kubwa kama kipa. Hana maskhara golini ndio maana anajipanga.

Umahiri wake huo ni matokeo ya kujituma na kuijua kazi yake vilivyo. Iwapo wengine hamjui, Kaseja hutangulia mazoezini kusudi ajipime mwenyewe kabla ya kusubiri maelekezo ya kocha. Maana Kaseja ana jitihada binafsi katika mazoezi. Hizi ni sifa.

Pamoja na ufupi wake, ana uwezo wa ‘kupunguza goli’ kiasi cha kufanya washambuliaji wakune vichwa ili kutafuta njia nyingine ya kumfunga.

Kaseja ni kipa mwenye uwezo wa kucheza krosi ambazo kwa zama hizi, sijaona mfano wake nchini petu. Pondamali anasema Dihile anafanya hivyo mazoezini, lakini ikija mechi, loh.

Kaseja anapanga beki, anazungumza na mabeki.

Ni mwepesi asiyependa kufungwa. Kwa wanaomfahamu, Kaseja anachukia mno kufungwa, sembuse anapodaiwa amekula mlungula.

Hizo ndiyo sifa za kipa Kaseja. Na ni hizohizo zinazonisukuma na kuthubutu kuuliza ukiacha wale wa nyuma waliopita hadi alipostaafu Mwameja, nani kama yeye Tanzania?

Ajabu wakati juzi Jumatatu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilifungua msimu mpya wa michuano katika soka, ndani na nje ya nchi, Kocha Mkuu wa Yanga, Dusan Kondic, anaibuka na kusema anamtema Kaseja.

Nadhani Kondic angesema tu kwamba “mkataba wa Kaseja umekwisha na Yanga haina uwezo wa kumsajili kwa ajili ya msimu unaofuata.” Haikubaliki anaposema hamfai tena kiuwezo.

Kwa Kondic, raia wa Serbia, Kaseja ni mmoja wa wachezaji stadi aliotangaza kuwatema. Anasema hana uwezo.

Naona Kondic anachemka sasa ikiashiria Yanga inamshinda uwezo. Huenda akawa na msimu mbaya Jangwani tangu ajiunge mwaka 2007.

Anapomfananisha Kaseja na makipa wengine nchini, hakika Kondic anathibitisha amechoka kufikiri. Baadhi ya anaowataja wanafahamika mno walivyo mahiri katika kutema mipira. Fikiria kudondosha mpira alipo mshambuliaji hodari. Goli.

Ningemuelewa Kondic laiti angejenga hoja yake Julai mwaka jana alipobaini Mfadhili wa Yanga, Yussuf Manji, anateta na Kaseja ili kumsajili. Aliridhia na hatimaye Kaseja akasajiliwa kwa fedha nyingi kuliko mchezaji mwingine nchi nzima.

Lakini kutoa hoja dhaifu muda huu kwa sababu Yanga haina nguvu ya kumbakisha Kaseja, ni kudanganya wana Yanga na wapenda soka Tanzania.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: