Kukemea ufisadi ni ujasiri tosha


Fred Mpendazoe's picture

Na Fred Mpendazoe - Imechapwa 26 May 2009

Printer-friendly versionSend to friend
Waraka wa Wiki
Fred Mpendazoe

Tatizo kubwa la utawala wa nchi yetu na la muda mrefu na ambalo limekuja kujulikana hivi karibuni ni ufisadi usio kifani.

Mwalimu Julius K Nyerere katika kitabu chake cha uongozi na hatima ya Tanzania anasema, “utajiri unaweza kupatikana  kutokana na rushwa kwa watumishi wa umma au kutokana na wafanya biashara ambao wanawania nafasi za kisiasa ili wawe wadeni wa rais aliyeko madarakani.”

Haya aliyasema  Baba wa Taifa mwaka 1995 na kwa chaguzi zilizofuata za mwaka 2000 na 2005 mambo haya yalionekana dhahiri.

Aprili 2000 Jaji Sinde Warioba aliyewahi kuwa waziri mkuu na makamu wa kwanza wa rais alieleza, “Kuna mwenendo usiopendeza wa kuongezeka kwa kasi kwa pengo kati ya matajiri na masikini. Siasa inatekwa na matajiri. Ufisadi na rushwa ni vitu muhimu katika uchaguzi. Ufisadi unaigawa vipande nchi.”

Warioba alisema hakuna tajiri hata mmoja hapa nchini kwa hivi sasa anayeipenda CCM kwa dhati kiasi cha kutoa mwenyewe pesa zake mfukoni, tena nyingi, kwa chama hicho…(watoaji) wengi au wote wanajiingiza ili kulinda biashara zao tu.”

Maelezo ya Mwalimu  Nyerere mwaka 1995 na ya Jaji Sinde Warioba mwaka 2000 yanaonyesha kiini cha ufisadi katika nchi yetu. Ufisadi uliopo sasa katika siasa na serikalini ni zao la ufadhili.

Tarehe 30 Desemba 2005, alipokuwa akilizindua Bunge, Rais Jakaya Kikwete alisema, “Yameanza mawazo kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Tusipokuwa waangalifu nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo…”

Nchi kuwekwa rehani na matajiri ni jambo la hatari sana kwani maana yake ni kwamba serikali itaongozwa na matajiri na hivyo haitawajibika kwa wananchi na demokrasia itakoma. Huu ndiyo ulikuwa mtazamo wa rais siku chache baada ya kuapishwa.

Tanzania inayo nafasi kubwa ya kuondokana na umasikini kutokana na rasilimali nyingi zilizopo. Lakini kutokana na ufisadi unaofanywa na Watanzania wachache, bado Tanzania ni moja ya nchi 14 masikini sana duniani.

Katika mwaka 2007 kutokana na ufisadi mbalimbali uliofanyika, serikali ilipoteza karibu Sh. 1.25 trioni au asilimia 10 ya pato la taifa. Fedha hizi zingeweza kujenga barabara za lami zenye kilometa 500 au madarasa 7,500 na vifaa vyake vyote muhimu na wananchi wasingechangishwa.

Watanzania wanajua kwamba fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ziatazo Sh. 133 bilioni zingejenga zahanati 2,600 kwa kila kila zahanati kugharimu Sh. 50 milioni.

Fedha inayopoteza serikali kila mwezi kulipia gharama zinazotokana na mikataba mibovu ya Richmond, Downs, IPTL, Songas, Agreko na mingine mingi, ingetosha kuwalipia karo wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu nchini na kuwalipa ipasavyo wastaafu waliokuwa wafanyakazi wa shirika la Reli la Afrika Mashariki.

Ufisadi uliofanyika katika uuzaji wa mashirika ya umma, mfano shirika la Reli Tanzania, mgodi wa Kiwira, nyumba za serikali, ununuzi wa ndege ya rais na ununuzi wa rada, serikali imepoteza mabilioni ya shilingi ambayo yangetosha kuboresha huduma za maji na afya nchini, kuwapatia wakulima ruzuku waweze kupata pembejeo kwa bei nafuu na hatimaye maisha bora kwa kila Mtanzania yangepatikana.

Watanzania wote wanatakiwa kuwa na ujasiri w akupambana na ufisadi bila kujali itikadi ya vyama vya siasa. Ipo haja ya kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete kwa ujasiri aliouonyesha pamoja na Watanzania wengine.

Watanzania wazalendo wanaoitakia mema nchi yetu tumuunge mkono Reginald Mengi kwa ujasiri aliouonyesha hivi karibuni kwa kuuhabarisha umma kwa maoni aliyoyatoa juu ya chanzo cha ufisadi nchini.

Sir Churchill, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza (1940-45) na (1951-55) aliwahi kusema, “Ujasiri ni sifa ya kwanza kwa binadamu kwa sababu ujasiri ndiyo unaohakikisha kuwepo kwa sifa nyingine.”

Naye mwanafalsafa a Barry Goldwater aliwahi kusema, “Kuvuka mpaka katika kutetea haki na kutetea wananchi maskini siyo uovu, wala kudai haki kwa kadri si uugwana.” Mengi ameonyesha sifa ya ujasiri na upendo kwa Watanzania. Tumuunge mkono.

Watanzannia wenzetu wanaolalamika juu ya hatua alizochukua Mengi wanathibitishia kwamba mawe yalio chini ya bahari ni vigumu sana kusikia kilio cha kiu ya maji ya mtende ulioko jangwani. Ni bayana kwamba wao kwa namna mbalimbali wananufaika na fedha za ufisadi. Hawawezi kamwe kuwatetea wananchi wanaoathirika na matokeo ya ufisadi.

Kwa taswira hii Watanzania tumegawanywa katika matabaka. Tabaka la Oligaki: matajiri walio na nia na harakati za kupora uchumi wa nchi yetu, hawawezi kufurahishwa na juhudi za kuwasemea Watanzania maskini.

Tabaka la Aristikrasi: Wale wateule  marafiki wa mafisadi, hawawezi kusikia kilio cha wanafunzi waliokosa mikopo, wananchi wanaoshindwa kupata fedha za matibabu kwani watoto wao wanasoma shule za kimataifa za karo za mamilioni ya shilingi; wakipata mafua wanaenda kutibiwa  nchi za nje.

Tabaka la Timokrasi: Wale wenye tamaa ya madaraka na waliopata uongozi kwa hila na siyo kwa kura, wakati wowote wanaweza kuwasaliti wananchi na kuwa vibaraka wa mafisadi. Timokrasi ni wenye tamaa na wanafiki. Mnafiki humtukuza yeyote, kwa lolote kwa matumaini ya chochote.

Haya ndiyo mawe yaliyo chini ya bahari, mtende ulioko jangwani ukilalamika juu ya kiu, mawe haya yanakejeli kama baadhi ya Watanzania wanaodai kuwa “ajenda moja ya ufisadi imewachosha na haina tija.”

Tabaka la mtende jangwani: Hawa ni Watanzania wanyonge ambao kwa umaskini wao uliokithiri wameendelea kubebeshwa mizigo ya kulipia elimu, matibabu, uhaba wa maji, ubovu wa miundombinu ya barabara na reli. Wanakabiliwa pia na ugumu wa maisha kutokana na mfumuko wa bei.

Katika hali hii, kila anayepingana na ufisadi anastahili kuungwa mkono. Tunahitaji ukombozi mpya. Na miongoni mwa watu binafsi, Mengi amejidhihirisha.

Mwandishi wa makala hii ni Mbunge wa Kishapu (CCM)
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: