Kupanda, kushuka kwa Saitoti


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version
George Saitoti

VILIO na majonzi nchini Kenya vilihanikiza. Simanzi na maombolezo kote. Nchi imepoteza mwanasiasa aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuwa mrithi wa rais wa sasa Mwai Kibaki.

Huyo si mwingine ila ni George Saitoti (66) aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani wa nchi hiyo, ambaye 10 Juni mwaka huu ajali ya helikopta iliyotokea katika eneo la Kibiku karibu na mji mkuu wa Nairobi, ilikatisha maisha yake.

Si yeye pekee aliyefariki dunia. Watu wengine watano waliokuwepo kwenye helikopta hiyo nao walifariki wakiwepo naibu wake Orwa Ojode, walinzi na marubani. Makamu wa rais wa Kenya.

Saitoti na naibu wake Orwa walikuwa wakielekea katika mkutano wa kiusalama katika eneo la Sotik magharibi mwa Kenya.

Mengi yamesemwa lakini taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa Saitoti alikuwa akionekana kuwa ni mmoja wa wanasiasa mashuhuri waliokuwa wakiwania nafasi za juu za uongozi wa nchi hasa nafasi ya urais unaotarajiwa kufanyika Machi 2013.

Saitoti, katika medani za kisiasa nchini Kenya, alitumia nafasi ya elimu yake katika kumpandisha katika ulingo wa kisiasa na hatimaye mwaka 1983 alichaguliwa kuwa mbunge nchini humo chini ya uongozi wa aliyekuwa rais wa Kenya, Daniel Arap Moi. Baada ya miaka mitano Saitoti alichaguliwa kuwa makamu wa rais.

Taarifa nyingine zinasema kuwa Saitoti alitokea kupata umaarufu kutokana na utendaji wake wa kazi, unyenyekevu na uaminifu kwa rais Moi, jambo ambalo lilimshawishi Moi kuendelea kumweka madarakani kwa miaka 13.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, wakati bado akiwa makamu wa rais na waziri wa fedha, Saitoti alihusishwa na kashfa ya rushwa iliyojulikana kama “Goldenberg Scandal” – udanganyifu uliofanywa katika serikali kiasi cha kuathiri uchumi wa Kenya kupungua kwa asilimia kumi katika mapato yake ya mwaka.

Hiyo ilikuwa kashfa iliyomchafua sana Saitoti kwa kipindi chote alichokuwa madarakani japokuwa kuhusika kwake katika kashfa hiyo hakukuweza kuthibitishwa moja kwa moja.

Saitoti alijiuzulu kuwa waziri wa elimu Februari 2006, lakini akachaguliwa tena kushika nafasi hiyo mwezi mmoja baada ya mahakama ya sheria nchini humo kuamua kuitupili mbali kashfa iliyokuwa ikimkabili ya kuhusihwa katika rushwa.

Baada ya maamuzi hayo ya mahakama, Saitoti alisema kuwa alihisi kuwa huru na kutua mzigo mkubwa, ambao alikuwa ameubeba kwa zaidi ya muongo mmoja. Hata hivyo, serikali ilisema itakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, lakini haikufanya hivyo.

Pamoja na kashfa hiyo kutikisa, Saitoti hakukata tamaa na hatimaye akateuliwa kuwa mmoja wa “makamanda” walioaminika katika serikali ya rais wa sasa wa Kenya, Mwai Kibaki.

Akiwa ndani ya serikali ya Kibaki, Saitoti alichaguliwa kuwa waziri wa elimu na hatimaye kuwa waziri wa usalama wa ndani wa Kenya, ambapo alikuwa msemaji mkuu wa serikali katika masuala ya usalama wa nchi hiyo.

Saitoti alichaguliwa na serikali yake katika kuongoza mapambano dhidi ya kikundi cha kigaidi cha Somalia cha al-Shabab, ambacho kinaaminika kuhusika katika mashambulizi mbalimbali yanayotokea ndani ya Kenya.

Saitoti alionekana mara kwa mara katika televisheni ya taifa akielezea uamuzi wa nchi yake katika kupambana na kikundi cha al-Shabab. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa alitimiza wajibu wake katika kufanya maamuzi hayo.

Katika kile kinachoonekana kukubalika katika ulingo wa siasa nchini Kenya, utendaji kazi wa Saitoti ulimweka katika nafasi ya kugombea kiti cha urais wa nchi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa kifo chake kinaweza kusababisha matatizo ndani ya serikali ya nchi hiyo. Ikumbukwe pia kuwa serikali ya Kenya ilikumbwa na machafuko ya kisiasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Ni serikali ambayo haijawa na urahisi na kutulia katika siasa za uadui ambayo kwa sasa inasemekana kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitafuta kura za kikabila wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.

Lakini si kwa Saitoti; akiwa na asili ya mchanganyiko wa damu ya Masai na Kikuyu, inasemekana hakuwa na kundi lolote la kikabila, na wala hakuwahi kujaribu kufanya hivyo, badala yake alifanya kazi ya kuunda kundi la wanachama walio na nguvu.

Siasa za Kenya sasa zimeingia katika mapungufu, na inaonekana kwamba haitakuwa rahisi kupata mtu mwingine wa kuziba nafasi iliyoachwa na Saitoti, na kuimarisha makundi aliyoyaita kuwa ni yake.

Taarifa nyingine toka nchini humo zinasema kuwa, ingawa bado muda wa kampeni haujafika rasmi, baadhi ya wanasiasa wameanza kupiga kampeni, jambo ambalo linaonekana litasababisha uchaguzi huo kuwa moja kati ya chaguzi za hatari na zenye vurugu ambazo Kenya haijawahi kushuhudia katika historia yake.

Wakati hayo yakitokea, serikali imetangaza siku tatu za maombolezo kutokana na msiba huo.

“Kifo cha Saitoti ni pigo kubwa sana na kimeiangusha serikali yetu katika kipindi hiki ambacho tupo katika maandalizi ya kufanya uchaguzi mkuu wa amani,” alisema Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga katika eneo la ajali Kibiku takriban kilomita 20 kutoka mji mkuu wa Nairobi.

Bado haijulikana chanzo cha ajali hiyo cha helikopta hiyo kuanguka. Polisi wapo katika uchunguzi wa ajali hiyo.

“Mpaka tunapoongea sasa, hakuna mtu anayejua chanzo cha ajali hii na uchunguzi bado unaendelea,” alisema Odinga.

Alisema kuwa Saitoti na naibu wake Orwa walikuwa wakielekea katika mkutano wa kiusalama katika eneo la Sotik magharibi mwa Kenya.

Naye Johnnie Carson, Katibu msaidizi wa Marekani katika masuala ya Afrika, wakati alipoitembelea Kenya Jumapili iliyopita alisema kuwa nchi hiyo imempoteza mtumishi aliyekuwa na msisimamo na mpiginaji mkuu na kwamba nchi yake imetuma salamu za rambirambi nchini Kenya.

Aidha, kiongozi ambaye anajulikana kuwa ni mpinga rushwa nchini Kenya, Mwalimu Mati alisema kuwa tukio hilo liifanye nchi hiyo kutilia mkazo katika kupinga historia ya serikali ya kipuuzi ambayo imekuwa ikinunua helikopita za kipolisi.

Alisema kuwa helikopta hizo zina gharama kubwa na pia gharama za matengezo zimekuwa kubwa na kuongeza kuwa vitu hivyo vimegharamu nchi hiyo mamilioni ya dola tangu mwaka 1999.

0
No votes yet