Kupishana kauli dalili ya ombwe serikalini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version

MWAKA 1995 Augustino Mrema alijiuzulu uwaziri wa Mambo ya Ndani na kujitoa katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kushindwa kutunza “siri za serikali”.

Mrema alichukua uamuzi huo kutokana na matamshi yake bungeni, kuhusu ufisadi uliogubika katika ubinafsishaji wa mashamba ya katani alipopewa mfanyabiashara V.G Chavda.

Kitendo chake cha kutoa “siri ya ufisadi” hadharani, kilisababisha asulubiwe na kusakamwa kwa kilichoelezwa kuwa alisaliti serikali ambayo yeye ni kiongozi.

Mrema alibanwa hadi kwenye kona na hatimaye kulazimika kuutema uwaziri. Mbali na uwaziri wa mambo ya ndani, Mrema alikuwa naibu waziri mkuu, wadhifa usiokuwepo kikatiba.

Kwa lugha nyingine, Mrema alistahili kukaa kimya kama mawaziri wenzake hata alipoona mambo hayaendi vizuri.

Mawaziri wote walikuwa wanajua V.G Chavda kafanya nini, alishirikiana na nani serikalini na walichopata hao walioshirikiana. Walifanya kile wanachoita uwajibikaji wa pamoja.

Uwajibikaji wa pamoja katika serikali zinazofuata mfumo wa Jumuiya ya Madola, unataka waziri awajibike kuyaunga mkono kwa uwazi maamuzi yote ya serikali yanayofanywa na Baraza la Mawaziri, hata kama yeye binafsi hakubaliani nayo. Uungaji mkono huo, unakwenda mbali hadi wakati wa upigaji kura katika bunge.

Yaliyotokea wakati wa Mrema yamekuwa yakijirudia katika serikali za awamu zote, na kwa sasa yako wazi zaidi. Tofauti ya wakati huo na sasa ni kwamba hatua hazichuliwi yanapojitokeza.

Si jambo la ajabu kusikia waziri anasema hili, mwenzake anampinga au anasema lile. Kinachoshangaza ni pale mkubwa wao, anapokuja na lake, tofauti kabisa na wasaidizi wake.

Wakati mwingine viongozi hao wa serikali wanatofautiana kwa maneno hadharani na hakuna hatua zinazochukuliwa.

Viongozi wengi kwa sasa wanaichanganya jamii. Kauli wanazozitoa zinapishana, kiasi kwamba haijulikani ipi ni ya serikali, ipi ni yao binafsi, lakini kibaya zaidi, husikii serikali ikitoa kauli ya kusawazisha mambo.

Aprili mwaka jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliduwaza wabunge wa CCM bungeni, alipopiga kura kukubaliana na kifungu cha 50 cha Muswada wa Sheria ya Utawala wa Mahakama wa mwaka 2011, kinyume na serikali yake ilivyokuwa inapendekeza.

Mapendekezo ya serikali yalitaka wakuu wa wilaya na mikoa wawe wajumbe katika kamati za maadili za mahakama katika maeneo yao. Kambi ya Upinzani ilipinga pendekezo hilo.

Wakati wa bunge kupigia kura kifungu hicho, Pinda alipiga kura ya “ndiyo” kuunga mkono kambi ya upinzani. Wabunge wenzake wa CCM, akiwamo Spika Anne Makinda, waliduwaa.

Wale wa upinzani walifurahi na kugonga meza. Hata baada ya Spika kumuuliza Waziri Mkuu mara tatu kwa kudhani amejisahau au akitaka kumshawishi abadili msimamo, yeye alisisitiza: “Nimesema ndiyo”.

Kwa kitendo hicho, Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, alisaliti serikali yake. Alipinga makubaliano waliyokuwa wamefikia kwenye Baraza la Mawaziri kuhusu kifungu hicho. Alistahili kufukuzwa au kujiuzulu. Hakufanya hivyo.

Pinda huyuhuyu Machi mwaka jana, alishangaza umma alipomzuia Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kutekeleza mpango wake wa kubomoa makazi ya watu ili kupisha hifadhi ya barabara.

Ingawa ana fursa ya kukutana na Magufuli kila anapotaka, Waziri Mkuu Pinda alisubiri hadi akiwa jimboni kwa waziri huyo na kutoa kauli hiyo.

Kana hiyo haikutosha kuonyesha udhaifu kiuongozi, Rais Jakaya Kikwete naye alipotembelea Wizara ya Ujenzi alimuagiza Waziri Magufuli kuzingatia kile alichokiita “utu” na “ubinadamu”.

Hatua hii ilishangaza wengi na kuhoji, hivi Rais na Pinda wameshindwa kumuita waziri na kumweleza hayo hadi wamseme hadharani? Waziri Magufuli aliwajibu mabosi wake akisema, yeye ataendelea kutekeleza anachokiona kwa mujibu wa sheria.

Mifano hii inaakisi mambo mengi yanayojitokeza serikalini sasa. Mathalan, suala la posho ya vikao na ugonjwa wa Dk. Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wa Ujenzi, nalo limesababisha mawaziri kupishana kauli.

Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amekuwa kila mara anainanga serikali ama kwa kushindwa kuchunguza na kutaja bayana matokeo ya uchunguzi wa ugonjwa huo.

Sitta ameeleza kushangazwa kwake na Waziri Mkuu Pinda kutozungumzia suala hilo kwa kuwa Dk. Mwakyembe alishatoa idhini kwa serikali kufanya hivyo.

Anasema hata kauli ya Pinda kuwa anayetakiwa kuzungumzia hilo ni Dk. Mwakyembe mwenyewe, si sahihi, kwani suala hilo linahusu jinai.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha anamtaka Sitta awapelekee Polisi ushahidi kuwa Dk. Mwakyembe alilishwa sumu. Baadaye anasema polisi tayari wanachunguza, lakini hawatatoa taarifa hadharani.

Wakati Pinda na Nahodha wanatoa majibu hayo, Sitta anakwenda mbali zaidi kwa kusema uchunguzi aliofanyiwa Dk. Mwakyembe nchini India kwa kuchukua kucha, ngozi na uboho, umeonyesha mbunge huyo wa Kyela, mkoani Mbeya, alilishwa sumu na ripoti iko serikalini.

Hivi haya anayoeleza kwa umma kupitia vyombo vya habari, mawaziri hao wanashindwaje kuyaeleza kwenye baraza la mawaziri ambako wote ni wajumbe?

Kama serikali ni moja kwa nini madai ya Sitta hayafanyiwi kazi? Hii ni ishara nyingine kuwa serikali imeparaganyika.

Mifano tuliyotazama hapo juu ni ya kushindwa kwa dhana ya uwajibikaji wa pamoja. Na hiyo ni matokeo ya serikali kushindwa kuheshimu misingi ya utawala bora.

Nguzo za utawala bora ni nidhamu ya utendaji wa kazi na mahusiano mazuri ya kazi kati ya watumishi, wakiwamo mawaziri. Haya yakikosekana ndiyo kuparaganyika kwa serikali. Hiki ndicho tunachoshuhudia katika serikali sasa.

Suala jingine ambalo linaashiria kuparaganyika kwa serikali kwa kukosa uwajibikaji wa pamoja ni ongezeko la posho za vikao za wabunge kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000 kwa siku.

Katika hoja hii ambayo ni moto kwa sasa, viongozi wa serikali wamepishana kauli kwa upande wao, na wale wa bunge, mhimili mwingine wa dola, kwa upande mwingine. Pia viongozi wa mihimili hiyo wametofautiana.

Pinda amesema tayari Rais Kikwete ameidhinisha ongezeko la posho za  vikao  (sitting allowance)  za wabunge kutoka Sh 70,000 hadi Sh 200,000 kwa siku, lakini Ikulu ikakana taarifa hiyo ikisema rais hakuwahi kusaini nyongeza hiyo bali alitaka Waziri Mkuu atumie busara katika kupatia suluhu suala hilo.

Kwa upande mwingine, Spika Makinda anazidi kusisitiza kuwa posho hizo zimekwishaanza kulipwa na Rais (Kikwete) ameshatoa kibali.

Kauli hiyo inamwingiza kwenye mvutano na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah, ambaye amesema jibu la ikulu ndilo sahihi, kwa kuwa Rais Kikwete hajaidhinisha posho hizo.

Kauli hizi tata zinatia shaka kuhusu umakini wa serikali na bunge, ikiwa viongozi wakuu wa mihimili hiyo wanatoa kauli tofauti juu ya jambo moja linalogusa maslahi ya nchi, na ambalo wana uwezo wa kushauriana kwenye vikao vyao vya ndani.

0756 346175
0
No votes yet