Kustaafu kwa Luhanjo ni salamu kwa Makinda


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 04 January 2012

Printer-friendly version

MWAKA jana katika moja ya makala zangu kwenye safu hii niliandika kwa kina sababu za Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuteua wajumbe wasiokuwa na majina makubwa wa kamati teule kuchunguza sakata la David Kitundu Jairo na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.

Nilisema miongoni mwa sababu, ni kujenga himaya yake. Anataka kujipambanua na siasa za spika mtangulizi wake, Samuel Sitta. Ni kama alitaka kuanza kutekeleza kile wahenga walichosema “kila zama na kitabu chake.”

Ni kweli Makinda angeweza kuteua wabunge mashuhuri kama wale waliochangia hoja ya kuundwa kamati hiyo – mfano wa Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini-CHADEMA), Beatrice Shellukindo (Kilindi- CCM) na Christopher ole Sendeka (Simanjiro-CCM). Aliteua wabunge wageni.

Hata hivyo, ripoti ya kamati hiyo iliibua mambo mengi mazito: Kwanza kuwatia hatiani Jairo kwa kuendesha uchangishaji wa fedha kinyume cha taratibu; pili, ilibaini Luhanjo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh walikuwa na njama za kutaka kumsafisha Jairo. Wawili hawa (Utouh na Lujanjo) wametakiwa kuwajibishwa.

Hatua ya Spika Makinda kuunda kamati teule ya wabunge wageni wasio makeke sana kama walivyoshuhudiwa kwa Bunge la Tisa aloliongoza Sitta na ikaleta matokeo mazuri, ilijenga taswira kwamba spika amevunja hisia kuwa ni wabunge “wakubwa” tu wanaoweza kutikisa kama ilivyokuwa kwa kamati teule iliyochunguza kashfa ya mkataba wa Richmond. Hii iliongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, sasa Naibu Waziri wa Miundombinu.

Makinda amefanikiwa haraka hivi katika hatua ya awali. Mtihani sasa ni katika hatua yake ya pili ya kuhakikisha maazio ya Bunge yanatekelezwa vizuri. Kwa sasa kuna kila dalili atakabiliwa na kile kile alichokumbana nacho mtangulizi wake, katika kuhakikisha kuwa walioguswa na ripoti ya Bunge wanaadhibiwa bila kusitasita.

Disemba 31, mwaka jana, umma ulishuhudia jambo kubwa. Rais Jakaya Kikwete alimwapisha Balozi Ombeni Sefue kushika wadhifa wa Luhanjo, aliyestaafu utumishi wa umma siku hiyohiyo, kwa mujibu wa sheria.

Luhanjo amestaafu wakati umma ukisubiri kusikia amewajibishwa na serikali kutokana na azimio la Bunge baada ya kubainika alimsafisha Jairo isivyopasa. Ina maana Luhanjo amestaafu bila doa na amepata maslahi yake kisheria.

Utouh bado yuko kazini. Wala naye haijulikani kama amechukuliwa hatua yoyote ya kinidhamu kwa kile alichobainika kutenda katika suala la Jairo. Wote wawili haielekei kama wamebanwa vyovyote vile kufuatia azimio la Bunge. Tunasubiri mvutano sawa na uliowahusu walioguswa katika suala la Richmond.

Itakumbukwa kuwa pamoja na watumishi wengine wa umma waliotakiwa kuwajibishwa kwa sakata la Richmond ni pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi. Walimaliza utumishi wao wa umma bila kuguswa. Sasa ni wastaafu!

Maazimo ya Bunge kuhusu kuwajibishwa kwao yalipigwa danadana hadi Sitta ambaye alikuwa ameyasimamia kwa mbwembwe nyingi, alipofunga kazi kwa kuagiza kuwa mjadala wa suala hilo “umefungwa.”

Uzito wa kuwajibisha watuhumiwa ulioikabili serikali kwa Hoseah, Mwanyika na Mwakapugi umejirudia kwa hili la Jairo. Nini kinaweza kutokea sasa? Ni msuguano uleule wa Bunge na Serikali juu ya utekelezaji wa maazimio yake. Kwamba kulikuwa na mvutano wa Bunge na serikali wakati wa sakata la Richmond, si jambo la kujiuliza. Kwamba ugomvi huo uligeuka na kuwa wa baadhi ya wabunge ndani ya Bunge na hata na baadhi ya watendaji serikalini, pia si jambo la kujiuliza.

Hata kile kilichokuja kubatizwa jina la uhasama wa kisiasa kati ya wabunge wa CCM halikuwa jambo jingine bali ni majeraha yaliyoendelea kuwaandama wabunge wa CCM yakiakisi sakata la Richmond katika picha iliyoonekana kama juhudi za makundi yaliyopingana kutaka kulipizana kisasi au kulenga kupinduana.

Ugomvi huo wa maazimio ya Bunge ndio ulisababisha hata baadaye kuundwa kwa kamati ya watu watatu CCM chini ya Mzee Ali Hassan Mwinyi kwa nia ya kupatanisha makundi yaliyokuwa yanahasimiana na kukamiana. Kazi hiyo haikuwezekana na hadi leo haijawezekana. Wajumbe wake walikuwa Pius Msekwa na Abdulrahaman Kinana.

Kwa maana hiyo, kustaafu kwa Luhanjo bila ya kuonekana kuchukuliwa kwa hatua zozote dhidi yake kunaweza kuwasilisha ujumbe mmoja muhimu kwa Spika Makinda: kwamba ingawa alionekana kuwa anaweza kusaidia kupoza makundi hasimu ndani ya Bunge na kwa mantiki hiyo katika CCM, ukweli wa hali halisi unaelekea kwenda kinyume chake.

Ni vigumu kusadiki kwa mfano kuwa Rais Kikwete anaweza kuridhia kuadhibiwa kwa Luhanjo. Amefanya kazi naye kwa muda mrefu; tangu akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambapo Luhanjo alikuwa Katibu Mkuu. Alihama naye kwenda Ikulu hadi alipostaafu. Bado haijulikani kama ndiyo mwisho wa utumishi wake au kuna uwezekano wa kuteuliwa na kusogezwa popote kwa madaraka ya rais.

Pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maazimo ya Bunge kuhusu Jairo na wenzake kusubiri kuwasilishwa bungeni katika mkutano unaokuja wiki chache zijazo, hilo haliondoi hulka na mwenendo wa serikali ya awamu ya nne – utamaduni wa serikali kuyumba katika maamuzi ya kusimamia sheria, taratibu na kanuni.

Ni serikali hii ilishindwa kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu Richmond kiasi cha kuibua mbinu chafu kupitia chama tawala ya kutaka kumpoka Sitta kadi ya uanachama kwa kile kilichoonekana kuwa kikwazo katika kuua hoja ya Richmond. Sitta aliposoma alama za nyakati, alikubali yaishe. Aliua hoja hiyo kinyemela kiasi kwamba mpaka sasa ana deni kubwa kwa Watanzania.

Pia ni serikali hii iliamua kushughulikia sakata la wizi wa fedha katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa njia za kifisadi sana. Kwamba wapo watuhumiwa walioshitakiwa, lakini wapo wengine walioachwa tu watese mitaani licha ya kukwapua mabilioni ya fedha za walipa kodi.

Sasa ninaposema serikali ina utamaduni wa kuruka vihunzi katika kusimamia sheria, kanuni na taratibu, sizui. Ni jambo la wazi.

Kustaafu kwa Luhanjo kutoshe tu kumpelekea Makinda salamu, kwamba pamoja na nia njema anayoweza kuwa nayo kutaka kuendesha Bunge kikakamavu zaidi, kuepuka njia ya Sitta na kutaka kurejesha umoja na mshikamano ndani ya Bunge na kwenye chama chake. Somo kuu: utamaduni wa serikali kulindana utaleta matokeo mabaya siku moja.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: