Kutoka kuvuna dhahabu hadi ufukara wa milele

- Machimbo ya dhahabu Lusu
“Askari waliingia ndani. Walikuta nimelala. Wakaniambia nikikataa kutoka wataleta greda. Nililia lakini walinipuuza. Wakatishia kuniua kwa greda. Nikakimbia”
WANANCHI ambao kwa miaka mingi walikuwa na maisha ya uhakika, ghafla walitoswa kwenye ufukara na tangu hapo maisha yao hayajatengemaa.
Waliotibua maisha yao na “kuwaua kiuchumi,” ni kampuni ya Resolute Mining Limited (RML) yenye makao makuu nchini Australia.
Katika muda wa saa tatu tu, walijikuta wameshatawanywa kwa nguvu za polisi huku mali na makazi yao vikiwa vimeharibiwa.
Ni wananchi waliokuwa wakitegemea machimbo ya dhahabu ya Lusu, yaliyoko kiasi cha kilomita 20 Mashariki mwa mji wa Nzega, mkoani Tabora.
Kupitia kampuni yake tanzu ya Resolute (Tanzania) Limited (RTL), RML ilisaini mkataba na serikali ya Tanzania mwaka 1997 – mwaka mmoja baada ya operesheni ya polisi kukamilisha kuwaswaga nje ya machimbo na makazi yao.
Hakuna takwimu rasmi zinazotaja idadi hasa ya walioathirika, lakini wakili Tundu Lissu, ambaye amekuwa akifuatilia madai yao, anasema wanafikia 10,000.
RML, kupitia tovuti yake "http://www.resolute-ltd.com.au" www.resolute-ltd.com.au inasema inamiliki hisa asilimia 100 katika biashara inayofanyika kwenye machimbo hayo, chini ya mradi uitwao Golden Pride.
RML ni kampuni yenye utajiri mkubwa kwa uzalishaji wa dhahabu inaoufanya sehemu mbalimbali duniani. Ina migodi Queensland (Australia), Ghana na Mali.
Kufikia 30 Juni, mwaka jana, ilikuwa imepata wakia 303,722 za dhahabu ambazo kwa bei ya dola 1,186 kwa wakia moja iliyokuwepo 20 Mei mwaka huu, ingepata dola 360,214,292 sawa na Sh. 468.28 bilioni.
Tovuti hiyohiyo, pamoja na nyaraka za serikali ya Tanzania, inaonyesha mgodi wa Lusu una akiba ya wakia 180,000 za dhahabu na imewekeza Lusu mtaji wa dola 370 milioni (Sh. 500 bilioni).
Taarifa zinaonyesha mpaka 2005, imelipa serikalini dola 28.09 milioni, sawa na Sh. 30 bilioni, za kodi mbalimbali na mrabaha.
Kwa mapato yake na kwa kiasi ambacho kimelipwa serikalini, laiti kungekuwepo nia njema kwa wakazi wa Lusu, hata Sh. 10 bilioni zisingemalizika kuwalipa. Lakini hakuna aliyejali hilo.
Ingawa taarifa yake ya karibuni inaonyesha RML imeuza mali zinazotokana na mgodi ulioko Ghana kwa kampuni ya Viking Ashanti kwa thamani ya dola 8 milioni (Sh. 10 bilioni), nimekuta vilio na simanzi tupu Lusu.
Mbali na kijiji cha Lusu, mgodi unapakana na vijiji vya Isunga, Mwaluzwilo, Ifumba, Iyuki, Isanga, Bujulu, Mwakabasa na Mkwajuni vilivyoko ndani ya Kata za Lusu, Nzega Ndogo na Nata.
Hata baada ya kuwa wachimbaji wachache ndio waliogundua dhahabu Lusu mwaka 1987, na kuanza kuchimba mwaka 1988, waliondolewa kwa nguvu na kila kilicho chao kikateketezwa.
Siku isiyosahaulika
Tarehe 30 Septemba 1996 magreda ya serikali yaliingia Lusu na kuvunja nyumba za wakazi na biashara zao; yakavuruga mashamba yaliyokuwa na mazao ya chakula.
Yalivuruga kwa kuchimbachimba njia zote za asili zilizokuwa zikitumiwa kuingia na kutoka machimboni. Hazipo sasa. Kilichopo ni njia za kubahatisha na kuzunguka sana.
Zana na mashine za uchimbaji na uchekechaji mawe hadi kupata dhahabu, ziliharibiwa. Machimbo yenyewe ya asili yalivurugwa na kufukiwa.
Alfajiri ile ya saa 11, hakuna aliyesalimika. Si wamiliki mashimo (wanaita maduara) ya uchimbaji, wachimbaji, wala akinamama waliokuwa wakiuza chakula.
Kili Stephano, mmoja wao, anasema alishtuka aliposikia kishindo wakati akiandaa vitafunio vya biashara.
“Nilisita kufanya kazi. Baada ya muda kidogo, nikatoka kuangalia. Kumbe ilikuwa zahma kwetu. Sikutarajia kushuhudia unyama kama ule maishani mwangu,” anasema akiwa nje ya nyumba yake iliyopo Mkwajuni, kitongoji kilichoko karibu na mgodi.
“Hakuna kilichobaki; hadi nyumba niliyokuwa natumia kama hoteli ilivunjwa. Huo ukawa mwanzo wa safari ngumu ya maisha nisiyoweza kuisahau maana sina nilichookoa,” anasema.
Mwenyekiti wa kitongoji kimojawapo aliyetaka asitajwe jina gazetini, anasema alisikia sauti ya magreda akiwa msalani.
“Nilitolewa mkuku na askari. Nikaburutwa na kutakiwa kuondoka bila ya kuchukua chochote. Nilikuwa na maduara mawili na nyumba ya kuishi pale. Hakuna kilichobaki.
“Kuyaeleza haya yananikumbusha unyama waliokuwa wakifanyiwa Waafrika wenzetu weusi kule Afrika Kusini na serikali ya makaburu,” anasema.
Maisha yake yanajieleza. Nyumba yake ya sasa ni ya miti na tope iliyoezekwa nyasi. Ana kitanda cha miti kilichotandikwa nyasi chakavu. Si godoro. Awekako kichwa ndiko ameweka mbao ili kuinua kichwa. Yeye anasema huo ndio “mto wangu.”
Simulizi za Kabula Makalwe, mwenyeji wa Maswa, mkoani Shinyanga, zinahuzunisha. “Askari waliingia ndani wakakuta nimelala. Wakaniambia nikikataa kutoka wataleta greda. Nililia lakini walinipuuza. Wakatishia kuniua kwa greda. Nikakimbia ili kujiokoa na kifo cha kikatili.”
Aliona magreda yakipondaponda kila kitu na kufukia migodi yao midogo.
Anasema, “Wavunjaji hawakuumizwa na vilio vyetu – wanawake, watoto na wazee. Tulilia sana lakini wao ni kuita greda tu kuvunjavunja mali zetu. Walifukia kila kitu. Ukweli ni kwamba tulihama Lusu bila kupenda.”
Samwel Mwatonoka, aliyezaliwa 1946 kijijini Ibungila, Rungwe mkoani Mbeya, anasema “operesheni ile imenifilisi na sijaunga hadi leo.”
“Walinitoa kinyama. Hakuna tathmini yoyote ya mali zetu iliyofanywa kabla ya kufukuzwa na sijalipwa hata senti tano. Lakini najua wakubwa serikalini walilipwa kutumaliza.”
Mwatonoka alikuwa akimiliki shimo la uchimbaji pamoja na Tito Msengesi na Rehema Mdonge. Leo hataki kusema wakati huo alikuwa na shilingi ngapi.
“Nihurumie. Niache tu nisikueleze hilo. Nielewe tu nikisema walichofanya kimenitia umasikini na sitasahau... siwezi kwenda nyumbani mikono mitupu hivi, sitaeleweka. Ni aibu,” anasema.
Fatuma Mhina, mzaliwa wa mkoani Tanga aliyetokea Dar es Salaam na mumewe, Hashim, na kufikia Isunga kabla ya kuhamia Lusu kutafuta dhahabu, alikuwa anamiliki mashimo matatu ya uchimbaji.
“Mnapokuja hivi kutuuliza historia, inatuumiza sana. Walipokuja kutufukuza, nilikuwa najiandaa kwenda kusimamia miradi yangu… nilikuwa na maduara (mashimo) matatu, nyumba mbili na shamba,” anasema kwa sauti ya uchungu.
“Walivunjavunja kila kitu na sina chochote nilicholipwa hadi leo zaidi ya kuhangaika kwenye ofisi za serikali Nzega na Dar es Salaam,” anasema.
“(Lusu) kule wananchi tulikuwa na mali nyingi: mashamba, nyumba za biashara na makazi; mashine za kusaga nafaka, hata makaburi yalikuwepo. Hatukupata chochote na hatujalipwa chochote,” anasema.
Simulizi zinaonyesha “operesheni ondoa wachimbaji Lusu” ilisimamiwa na Stephen Mashishanga, mkuu wa mkoa wa Tabora wakati huo, Julius Manyambo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega na wakuu wa Polisi mkoani na wilayani.
Waliitwa Lusu baada ya wananchi kufanikiwa kuwafurusha mawakala wa wazungu waliofuatana na wazungu wenyewe kwenda kuwaondoa kwa magreda.
“Mzungu alichupa kutoka kwenye greda tukajua amekimbia na kujificha. Kumbe alikwenda kuita serikali. Ukaja msafara mrefu wa magari ya wakubwa. Wakatuamuru tuondoke au watatuangamiza na kila kilicho chetu. Walipoona tumetulia, wakaamrisha kazi ianze. Hakuna kilichosalimika,” anasema Robert Mshama Kigawilo.
Kigawilo, maarufu kwa jina la Mzee Bosi, anayeishi Mkwajuni tangu alipofukuzwa Lusu, anasema alihamishwa kwa nguvu na kwa “ukatili mbaya.”
“Nilikataa kutoka. Nikabaki getini pangu na baadhi ya mali pembeni. Wakangurumisha greda na kulileta hadi karibu yangu, sikutoka. Nikafumba macho ili nisiwaone wanavyoniua.”
“Ah, wale makatili kweli lakini,” anasema kwa mgegemo wa mchanganyiko wa kicheko na huzuni kubwa pale anapokumbuka mkasa wa 30 Septemba.
“Walikuja kuniinua na vitu vyangu. Wakanitoa pale. Nilikuwa nalia kama anavyolia mjukuu wangu; lakini hawakujali watoto. Wale, wabaya kweli…” anasema na kukatisha maelezo. Anafuta machozi.
Mzee Bosi, mzaliwa wa mwaka 1925 katika kijiji cha Ng’ongo, wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora, anasema akiyatafakari yaliyotokea 1996, anasema tu “Nigowalanguluka.”
Kwa Kinyamwezi, hilo lina maana ya “hata kesho kutakucha tu.” Ni masikitiko. Ni kukata tamaa.
Viongozi wa serikali Lusu
Siku chache kabla ya operesheni hiyo, wachimbaji wadogo na watu waliokuwepo machimboni Lusu, walimpokea Dk. William Shija, wakati huo mbunge wa Sengerema, Mwanza na waziri wa nishati na madini.
Alichokifanya ni kuwataka watulie, wajipange na kuimba. Nyimbo gani? Aliwaimbisha mara kadhaa, “Aliselema alija, aliselema alija.” Wanyamwezi wanatafsiri maneno hayo kuwa ni “kutembea huku ukiondoka.”
Ilikuwa ni amri kwa wachimbaji kuondoka Lusu, vinginevyo wataondoshwa kwa mabavu.
Mashishanga, anayeishi mjini Morogoro baada ya kustaafu serikalini mwaka jana, anatajwa ni mtu aliyeonyesha huruma kuliko viongozi wengine waliofika Lusu kabla ya wawekezaji kupishwa mgodini.
Alituliza watu na kuwasihi kutoa wasiwasi. Kwamba wataondolewa kwa utaratibu na atahakikisha wanafidiwa kwani walikuwa wakitegemea migodi kwa maisha yao.
Hebu tafakari yanayoelezwa kuhusu Omar Chambo, sasa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu ambaye wakati huo alikuwa Kamishna wa Madini, Kanda ya Magharibi, aliyekwenda kufanya ukaguzi wa mali zilizokuwa eneo la machimbo Lusu.
Godfrey Ntibakula (35), mwenyeji wa Kigoma aliyefika Lusu mwaka 1992, anasema Chambo alidhalilisha watu kwa kuita mali zao “si lolote bali vyoo.”
Anasema, “Omari Chambo alithubutu kuyaita maduara (machimbo) yetu ni vyoo visivyostahili kutathminiwa na kulipwa chochote.”
Ntibakula anaeleza, “Ofisa wa serikali mwenye dhamana muhimu ya kulinda maslahi ya serikali na wananchi, anapodharau watu ambao wamekuwa wakichimba dhahabu na kuita machimbo yao kuwa ni vyoo, ujue ni hatari.”
“Lakini ile ilikuwa ni jeuri ya pesa. Yeye na wenzake walishakamata chao ili kusaidia wawekezaji kuingia Lusu,” anasema Ntibakula.
“Angalia sasa tuliokuwa tunaishi kwa kutegemea machimbo yale, hatuna cha kujivunia isipokuwa huzuni na ufukara. Mimi hapa, sina kitu tofauti na nilivyokuwa,” anaeleza kwa sauti ya kunyong’onyea.
Ntibakula alikuwa akiendesha mashimo mawili ya uchimbaji dhahabu pamoja na mjomba wake aitwaye Elias Bichuro.
Mkuu wa Wilaya Manyambo, ambaye alihamishiwa wilayani Kahama na kukumbwa na tukio la kuuawa kikatili mwaka jana, alikuwa kiongozi maarufu Lusu lakini ni kwa sifa mbaya ya kutoa ahadi nyingi ambazo wana Lusu wanasema, “hata mwenyewe hakuwa anaziamini,” tena ndani ya kejeli.
Hata baada ya kuondoka Nzega, bado alishindwa kujibu maswali ya wachimbaji.
Ofisa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Nzega, anasema serikali inajua madai ya watu wa Lusu lakini hakuna aliyetayari kuyafuatilia.
“Kila kitu kinajulikana lakini nani wa kusema. Kusema kweli, wengine wanachota pale. Mimi usinitaje maana nitagombana bure na wakubwa zangu,” anaelekeza ofisa huyo.
Madai ya fidia ya wachimbaji wadogo wa Lusu yamefika serikali kuu kupitia iliyokuwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nayo mwaka 2003 ilimtuma Jaji Robert Makaramba kufuatilia.
Sasa akiwa Jaji wa Mahakama Kuu (Biashara), Makaramba hajarudi Lusu kusoma uamuzi baada ya kusikiliza, kwa siku tatu mfululizo, malalamiko yao kwenye ukumbi wa Mgurunde (wa Kanisa Katoliki Nzega mjini).
Tundu Lissu aliyewakilisha walalamikaji, anasema, “Haki haijapatikana. Sasa tunataka kupeleka kilio cha watu wa Lusu kwa wananchi wa Australia.”
Kwa nini wachimbaji wadogo wa Lusu waligoma kuondoka ili kupisha wawekezaji wenye mitaji mikubwa na zana za kisasa kwa ajili ya uchimbaji mkubwa?
Wanasema waligoma kwa vile walikuwa na haki juu ya mali zao. Walitaka zitathminiwe na kulipwa fidia. Huo ndio ubinadamu na ustawishaji haki sawa kwa wote. Walifukuzwa bila hayo kufanywa.
Kulingana na maelezo ya wachimbaji, Meneja Utumishi wa RTL, Ladislaus Machele, alikiri mbele ya Tume kuwa hawajalipa fidia wachimbaji wadogo ambao “walikuwa na mali.”
Hadi sasa si menejimenti ya RML wala RTL iliyojibu maswali yaliyotaka majibu kuhusu hatima ya madai ya wananchi.