Kutoka Richmond hadi Symbion Power


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 01 June 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

KAMPUNI ya Marekani ya Symbion Power, imezuia chombo chochote kuchokonoa, kuchunguza na kutoa habari kuhusu mkataba wake wa ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya Dowans Costa Rica.

Symbion Power inasema imepewa nguvu za kisheria ya kuzuia mtu kupewa siri za ndani za mipango hiyo bila idhini yake. Kwa hiyo, Symbion Power hawataki waandishi wa habari wadadisi ukweli wa mkataba huo ambao ama utawanufaisha au utawanyonga. Pia inataka wote waridhike kufungiwa mbuzi kwenye gunia na kukubali matakwa yao.

Wanaogopa nini? Kama wamepewa nguvu za kisheria, aliyewapa ni nani? Kwa nini wanaanza kwa kujihami? Kama Symbion Power ni halali kama ilivyo kwenye tovuti, vizingiti vya nini?

Mambo kadhaa yanasababisha watu kutilia shaka. Mathalani wakati inatangaza kuwa imenunua mitambo hiyo hawakuwepo wawakilishi wa kampuni ya Dowans iliyokuwa inamiliki.

Mmiliki wa mitambo hiyo ilielezwa kuwa ni Brigedia Jenerali Mstaafu wa Oman Suleiman Mohammed Yahya Al Adawi, lakini aliyepewa mamlaka ya kisheria kusimamia mitambo hiyo duniani kote isipokuwa Costa Rica ilikoandikishwa ni Rostam Aziz, mfanyabiashara na Mbunge wa Igunga.

Katika hili, waandishi na Watanzania wanataka kujua Symbion Power imezungumza na nani na wamekamilisha ‘dili’ kwa kiasi gani. Kampuni imewaficha habari waandishi wa Tanzania lakini, mtandao wa www.garp.org umefichua mitambo hiyo yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa mg 120 imeuzwa kwa dola 120milioni sawa na Sh. 180 bilioni.

Wakati kampuni haitaki watu wajue undani wake imekimbilia kufanya mazungumzo na Shirika la Ugavi Umeme Tanzania (TANESCO) ili liingie mkataba wa kuuza umeme.

Uharaka huu wa nini? Kwa nini TANESCO inajitia kitanzi cha mazungumzo bila kufuata utaratibu wa awali wa kuitisha zabuni? TANESCO haioni kuwa uwazi unahitajika zaidi kwa sasa hasa kwa mitambo hiyo yenye historia chafu iliyosababisha serikali kuvunjika Februari, 2008?

Jumamosi ya Mei 21, 2011 Symbion Power wanatangaza kununua mitambo ya Dowans na wanadai kuwa wameanza mazungumzo na TANESCO.

Jumatatu ya Mei 23, 2011 Meneja Mawasiliano wa TANESCO, Badra Masoud anatangaza kuwa wameanza mazungumzo na Symbion Power.

Siku inayofuata kamati ya Nishati na Madini inaikaanga serikali na TANESCO kwa kuchukua hatua za kinyonga katika kulipatia ufumbuzi tatizo sugu la umeme.

Vyombo vya habari vinamnukuu Katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo akisema serikali itaipa Symbion Power ushirikiano kuhakikisha inawasha mitambo hiyo kwa maelezo “tunataka umeme, tunataka maendeleo kwa watu wetu”.

Watanzania wameumwa na nyoka hivyo lazima washtukie kila unyasi ukiwagusa. Richmond Development LLC ni kampuni ya Marekani tena ilishinda zabuni, lakini baadaye ilionekana kuwa feki na kwa hiyo hata mkataba iliopewa ulikuwa batili.

Baadaye Watanzania wakaelezwa Dowans imepewa mkataba wa kufua umeme uliokuwa wa Richmond lakini ukafutwa na kusababisha Dowans kukimbilia Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC). Tatizo si ubora wa kampuni bali usiri katika kuingia mikataba.

Usiri umewaumiza Watanzania kuanzia wakati serikali ilipotia saini kuingiza IPTL huku ikijua athari zake. Baadaye viongozi walewale waliingiza kitapeli na kuipa mkataba kampuni ya Richmond.

Bila aibu viongozi haohao wakaingiza kitapeli Dowans na sasa inakubali wananchi wazuiwe kupata habari juu ya Symbion Power kuhusu dili la mitambo ya Dowans na inavyohaha kuhuisha mkataba wa kuzalisha umeme ambao utauzwa kwa Watanzania.

Power Symbion wanaweza kujitetea kuwa wao wamenunua mitambo na siyo kampuni. Ni kweli, lakini ieleweke kuwa hata Dowans haikununua kampuni ya Richmond. Tatizo ni namna kampuni husika inavyoingia mkataba. Mifano ipo.

Mwaka 1994; Luteni Kanali Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri wa Nishati na Madini aliingiza IPTL, mkataba huo unaitesa TANESCO hadi leo.

Mwaka 2006; Waziri mkuu, Edward Lowassa, alipanda pipa hadi Thailand kuomba mvua. Serikali ikaacha mradi huo ikabariki Richmond/ Dowans iliyosumbua nchi.

Mwaka 2007; Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi aliruka na mafaili ya mgodi wa Buzwagi hadi Uingereza kutia saini hotelini, tena usiku.

Kila likitokea tatizo la umeme nchini, serikali kwa kushirikiana na TANESCO huandaa mazingira kushinikiza jamii iridhike hatua za kutumia mitambo ya Dowans. Halafu akaletwa Al Adawi kujitambulisha kwamba yeye ndiye ‘Mr Dowans’.

Huyo ndiye alitumiwa kuwaambia waandishi wa habari kuwa yuko tayari kupunguza au kufuta deni lote isipokuwa gharama fulani muradi tu kampuni yake ikubaliwe kuingia mkataba mpya wa kufua umeme.

Al Adawi alitembelea mitambo ile iyoko Ubungo, akakutana na uongozi wa TANESCO na alikwenda ikulu ambako alikutana na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Katika siku ya pili ya ziara yake, TANESCO ikawasha mitambo ile kumpa matumaini Al Adawi kwamba wataunganisha umeme kwenye gridi ya taifa. Suala hilo liliibua mgogoro mwingine.

Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba alivalia njuga mitambo hiyo iwashwe. Mitambo hiyo imo kwenye mapendekezo ya kamati yake kwa serikali.

Baada ya mpango huo kugonga mwamba, wakatumia jumuiya ya wafanyabiashara kupiga kelele juu ya uhaba wa umeme na kushinikiza mitambo ya Dowans iwashwe. Kelele hizo hazikuzaa matunda.

Hapo ndipo Chama cha Wafanyabiashara (TCIA) kikatangaza kununua mitambo hiyo ili wafanye biashara na TANESCO. Mpango huo ukakwama pia kwa maelezo wamiliki wa Dowans walikuwa wanajigeuza sura.

TANESCO wakabuni tatizo la umeme kwamba katika muda wa siku 10 hivi kuanzia Mei 19, 2011 mgawo utakuwa mkali kwa vile mitambo ya umeme inayotumia gesi Ubungo itafungwa kwa matengenezo.

Siku tatu baadaye, Watanzania walioambiwa na Mahakama Kuu kwamba yasifanyike mazungumzo yoyote kuhusu mitambo ya Dowans bila kujulishwa, kampuni ya Symbion Power ikajitokeza kusema imenunua mitambo hiyo na haraka, serikali inatangaza kuisaidia iwashe mitambo izalishe umeme.

0658 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: