Kwa CCM, ubora na uoza ni sawa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 June 2010

Printer-friendly versionSend to friend
Tafakuri

RAIS Jakaya Kikwete ameibuka na kauli mpya, lakini iliyosheheni matundu.

Anasema, “Watu hawakifahamu vizuri chama changu – Chama Cha Mapinduzi (CCM).” Kwamba, kama wangekifamu, wasingekilaumu kutokana na hatua yake ya kumruhusu yeye kugombea tena urais katika ngwe hii ya pili.

“Inaonekana watu hawaifahamu vizuri CCM. Kama ningekuwa nimeboronga, tayari ningekuwa nimefukuzwa,” alisema Kikwete kwa sauti ya ukali.

Alisema kuruhusiwa kwake kugombea tena nafasi hiyo, kumetokana na kusimamia na kutekeleza vizuri ilani ya chama chake.

Kikwete alitoa kauli hiyo alipozungumza na wanachama wa CCM, mkoani Dar es Salaam. Ni wale waliokusanyika kumdhamini kwa ajili ya urais katika uchaguzi ujao.

Lakini kila mwenye kufuatilia anajua jinsi Kikwete alivyoboronga. Jinsi alivyoshindwa kutimiza ahadi zake na kibaya zaidi, jinsi asivyoweza kusimamia hata kauli zake mwenyewe.

Mara kadhaa Kikwete ameahidi kuboresha hali za wananchi. Ameahidi kuinua kipato cha wakulima; kutoa soko la uhakika la mazao yao; kuboresha kilimo chao kutoka kile cha kale hadi kile anachoita, “kilimo cha kisasa.”

Ameahidi kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuipa uwezo na vitendea kazi taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU).

Lakini ni Kikwete aliyeshindwa kumuondoa katika kiti chake, mkurugenzi wa taasisi hiyo, Edward Hoseah, aliyetuhumiwa na Bunge kubeba kampuni ya kitapeli ya Richmond kwa maslahi binafsi.

Ndani ya chama hakuna mshikamano. Wengi wa wanachama na viongozi wake, wameacha misingi ya asili ya chama isemayo “…nitasema kweli daima, fitina kwangu ni mwiko.”

Hakuna tena anayetanguliza maslahi ya chama mbele. Wengi wao wanaangalia maslahi ya tumbo lao kwanza. Hakuna kiongozi wala mwanachama mwenye mikono misafi, na hivyo, hakuna anayeweza kusimama na kumkemea mwenzake kwa matendo yake machafu.

Hata Kikwete mwenyewe hawezi kufanya hivyo. Ni kwa sababu, Kikwete ni sehemu ya yale ambayo yanalalamikiwa.

Hivyo basi, hapa Kikwete hajasema ukweli hata kidogo. Hatua ya kuruhusiwa kugombea tena imetokana na kutokuwa makini; na huenda hata unafiki wa viongozi wake na siyo kwa sababu ametekeleza ilani ya uchaguzi ya chama chake.

Kikwete anafahamu kuwa madai ya wazee katika chama na serikali hayajakauka. Kwamba ameshindwa kuchukua hatua katika mambo ya msingi, na hivyo wakapendekeza azuiwe kugombea muhula wa pili.

Kuruhusiwa kwake kugombea ngwe ya pili kumetokana na kukwepa aibu kutoka kwa wananchi na jumuiya za kimataifa; siyo kwa sababu ametekeleza kile alichoahidi.

Kumtosa Kikwete, kungekilazimu chama kuomba radhi Watanzania kwa kuwateulia na hatimaye kumnadi mtu ambaye kilimjua tangu mwanzo kuwa ni dhaifu.

Kingine kilichomsaidia ndani chama hiki, ni madaraka makubwa ya umungu mtu kwa vile ndiye mwenye kila mamlaka. Katika hali hiyo, hakuna awezaye kuzuia mwenyekiti wa CCM kuumba amtakaye na kuumbua asiyemtaka.

Lakini kama kuboronga ameboronga mara nyingi. Miaka mitano yote haikuwa neema kwake; chama chake wala wananchi wengine wa kawaida. Uhusiano wake na wapambe wake wa msingi umedorora. Chama kimejaa makundi yasiyoaminiana, yanayofitiniana.

Lakini kuna mifano mingine mingi inayoonyesha kuborongo kwa Kikwete katika miaka yake mitano hii.

Kwa mfano, wakati akiomba chama chake kimteue kuwa mgombea urais mwaka 2005, Kikwete alikuja na kaulimbiu ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya.

Leo, hakuna asiyefahamu kwamba hakuna chochote katika miaka mitano ya utawala wake kilichofanyika kwa kutumia falsa hiyo.

Wakati wananchi wakiwa bado wanajiuliza juu ya falsafa hiyo, juzi ameibuka na kaulimbiu nyingine (wala siyo falsafa) ya: Ari Mpya Zaidi, Nguvu Mpya zaidi na Kasi Mpya Zaidi.

Inawezekana kuwa ari, nguvu na kasi mpya zilizoibuliwa na Kikwete, zimelenga kuwadidimiza zaidi wananchi badala ya kuwasaidia. Ari, nguvu na kasi, vimelenga kuingiza wananchi katika utumwa wa kimapato.

Hii ni kwa sababu, tangu kaulimbiu yake, bei ya kila bidhaa – kuanzia za viwandani hadi zile za kilimo – imepanda maradufu.

Wakati Kikwete hajaingia madarakani na kaulimbiu yake hiyo, bei ya kilo moja ya sukari ilikuwa Sh.500 hadi 600, lakini leo, sukari inauzwa kati ya Sh. 1,500 na Sh. 1,800.

Ni Kikwete aliyeshindwa kutimiza ahadi ya kurejeshwa kwa mahakama ya kadhi nchini. Badala yake, waislamu wamekuja na hoja: Wanasema Kikwete na chama chake wamewatapeli kwani sasa wanadai kuwa “…suala la Mahakama ya Kadhi limeshashughulikiwa.”

Wanajiuliza: Nani anaweza kusema suala la mahakama ya kadhi limeshughulikiwa? Limeshughulikiwaje? Kwa kiwango gani? Nini kimekubaliwa? Inaanza lini? Kwa utaratibu upi?

Wanafika mbali zaidi. Wanalituhumu hata Kanisa wakisema, “limechangia kufanya mahakama hiyo kutorejeshwa, ingawa wengine wanasema kushindwa kurejeshwa kwa mahakama hiyo kumetokana na udhaifu wa Kikwete mwenyewe.

Huo ndio msingi wa tishio lao la kumyima kura katika uchaguzi ujao. Wanajua fika kuwa suala la mahakama ya kadhi, bado halijashughulikiwa na liko mikononi mwa Kikwete. Amekuwa nalo tokea alipoingia madarakani na hadi sasa bado analo.

Lakini kuna jingine pia ambalo limemshinda. Katika historia ya uongozi wa nchi hii, tangu Tanganyika na baadaye Tanzania, huyu ndiye rais pekee ambaye hakuonyesha ujasiri wa kumwaibisha mteule wake aliyevurunda hata katika mambo ya msingi.

Ukimwacha aliyekuwa waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ambaye alilazimika mwenyewe kujiuzulu kutokana na kashfa ya Rada, wengine wote, walijiuzulu kutokana na shinikizo kutoka nje.

Hata Edward Lowassa, na mawaziri wenzake wawili – Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi – waliojiuzulu kutokana na kashfa ya mkataba tata wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond, walifanya hivyo kutokana na shinikizo la wabunge.

Vinginevyo Kikwete alikuwa hana ubavu wa kuwafukuza. Ndiyo maana, Karamagi, Lowassa na Chenge, wameendelea na ubunge wao, pamoja na kukabiliwa na lundo la shutuma na tuhuma za kuangamiza nchi.

Wamebaki huko kwa sababu, ndani ya chama hiki, hakuna utamaduni wa kuwajibishana. Ni bahati Lowassa aliwahi kujiuzulu kwa sababu ya kuogopa Msabaha kumwaibisha. Vinginevyo, Kikwete hakuwa na ubavu wa kukabiliana naye.

Hii ni tofauti na waliomtangulia – Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Benjamin Mkapa na Ali Hassani Mwinyi. Watatu hawa wana mifano ya dhahiri inayoonyesha rais aliwajibisha watendaji wake; na ikulu ilikuwa sehemu ya utumishi.

Sasa kama CCM hawawezi kutofautisha ubora na uoza, basi chama na viongozi wake wanahitaji “miwani.” Nani awapime? Nani aichonge?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: