MARCIO Barthelio Maximo, kocha wa timu ya taifa ya Tanzania – "Taifa Stars," hakustahili kupewa jukumu la kuinoa timu ya Bara, "The Kilimanjaro Stars."
Kwa nafasi yake ya kunoa timu inayojumuisha wachezaji kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani (Zanzibar), Maximo ana jukumu kubwa mno na wala hastahili kuongezewa mzigo zaidi, labda kama ni kwa nia ya “kumtafuta ubaya.”
Naomba nieleweke vizuri kabla sijaendelea. Mimi si miongoni mwa kundi la Watanzania wanaotaka kocha Maximo afungashiwe virago kutokana na msimamo wake wa kuwatema wachezaji wanaojiona mastaa na wanaodaiwa kukosa nidhamu.
Namuunga mkono Maximo kwa asilimia mia moja kwa kusimamia nidhamu na kuwakataa “wachezaji wa mashabiki.” Lakini hili la Shirikisho la Soka nchini (TFF) kumkabidhi jukumu jingine la kukinoa kikosi cha Tanzania Bara, halikubaliki.
Michuano ya Chalenji inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 28 nchini Kenya na Maximo ameteuliwa kunoa Kilimanjaro Stars. Hapa naona TFF imepotoka.
Kwa mtazamo wangu, timu ya Tanzania Bara angepewa kocha mwingine mzalendo na Maximo angebaki kuwa mshauri tu wa timu zote za Tanzania Bara na Visiwani. Au angekuwa mtazamaji kama watazamaji wengine.
Kuna mengi ambayo wapenzi wa soka wangejifunza kwa Maximo kuwekwa pembeni katika kuinoa Kilimanjaro Stars. Si wapenzi wa soka tu bali hata TFF na Maximo mwenyewe.
Kuna baadhi ya makocha wazalendo wanapingana na mtazamo wa Maximo kuhusu wachezaji “wasiokuwa na nidhamu.” Naamini kwa kocha mwingine angewachagua wale wachezaji wanaopigiwa kelele na baadhi ya mashabiki na hivyo tungepata kitu kingine kipya katika timu yetu.
Kufanya vizuri au vibaya kwa Kilimanjaro Stars, yenye kocha mwingine, kungeisaidia sana TFF, Maximo na wapenzi wa soka pia. Ukikaa kwenye vijiwe wanapopatikana viongozi wa TFF, utawasikia baadhi yao wakimponda Maximo.
Bali ajabu ya watu hawa ni kwamba wakiwa mbele ya vinasa sauti, wanampongeza na kuwabeza wale wanaompinga. Hakuna shaka wanapalilia nafasi na mafao yao.
Nasema TFF ingenufaika kwa mambo yote mawili. Hii ingekuwa bahati nzuri kwake. Kufanya vizuri au vibaya kwa timu hiyo ingekuwa faida kubwa kwa shirikisho hilo lenye jukumu la kusimamia soka hapa nchini.
Kwa mfano, Kilimanjaro Stars isingekuwa na Maximo, kisha ikafanya vibaya katika michuano ya Chalenji, basi ungekuwa mtaji mkubwa kwa TFF na Maximo mbele ya mashabiki na wapenzi wa soka la Tanzania. Ni wazi kwamba, “mdomo” wa wanaomchimba kocha huyu raia wa Brazil ungefungwa rasmi.
Na kama timu hiyo ingefanya vizuri, basi kibao kingegeukia kwa Maximo tu, lakini kwa TFF kingesomeka vilevile – faida kwao. Hapa namaanisha ungekuwa mtaji kwa mashabiki wa soka wanaoshinikiza hadharani kocha huyu atimuliwe na hata kwa TFF wanaosemea “vichochoroni.”
Lakini Maximo angepata faida nyingine. Angekuwa jukwaani akiangalia vipaji vipya kutoka kwa wachezaji wapya walioitwa na makocha wapya kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
Hapa, Mbrazil angekuwa na fursa kubwa zaidi ya kuona uwezo wa wachezaji wengine, hasa kutoka Zanzibar ambao pengine hajawaona.
Hakika nashindwa kuielewa nia na shabaha ya TFF kumkabidhi jukumu jingine Maximo wakati wanayo fursa na mamlaka ya kutoa jukumu hilo kwa kocha mwingine.
Tunaweza kuuliza maswali mengi: Je, TFF wanaogopa gharama za kuajiri kocha mwingine? Je, hawaoni faida ambayo wao na kocha mkuu wangepata? Je, wana shinikizo kutoka kwa “wakubwa” kwamba lazima watumie Maximo katika kila eneo la soka kwa kuwa analipwa na serikali?
Narudia: Mimi si miongoni mwa wanaomchimba Maximo kutokana na msimamo wake kwa wachezaji “waliokosa nidhamu.” Bali sikubaliani hata kidogo na mtazamo wa TFF kumuona kocha huyu kama ndiye “Mungu” wa soka la Tanzania.
TFF wamemkabidhi majukumu mengi ya kiufundi, kama si yote, kwa Maximo. Hata kazi ya anayeitwa mkurugenzi wa ufundi, Sandy Kayuni haijulikani pale Karume, Dar es Salaam – makao makuu ya TFF.
Kuanzia kutafuta kocha wa timu ya taifa ya vijana mpaka mtaalamu wa viungo; majukumu hayo amepewa Maximo kana kwamba ndani ya TFF hakuna mwenye uwezo wa kuwatambua wataalamu hao.
Hebu tuambizane ukweli jamani. Hivi nchi hii hakuna kocha mwenye uwezo wa kuiongoza Kilimanjaro Stars kwenye michuano ya Chalenji mpaka ang’ang’aniwe Maximo?
Ukweli ni kwamba makocha wapo; tena wengi. Pamoja na matatizo niliyoorodhesha hapo juu; tatizo jingine linaweza kuwa kutojiamini na kutojithamini. Matokeo yake ni kuua nia ya makocha wetu na kuwa tegemezi daima.
