Kwa maandalizi haya, siku zote tutaishia kuwa watalii

KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam, mwakilishi pekee nchini aliyebaki katika michuano ya vilabu barani Afrika, ilipata kipigo cha mabao 3-0 mbele ya Al Ahly ya Misri zilipokutana 15 Machi mjini Cairo.
Hicho kilikuwa ni kipigo kilichotarajiwa na wengi kwani timu hizo kiuwezo ni tofauti kubwa kama usiku na mchana. Isitoshe, Al Ahly ndio mabingwa watetezi wa Afrika.
Kwa vyovyote itakavyokuwa, Yanga nayo imefuata nyayo za timu nyingine za Tanzania kuondolewa kwenye michuano ya kimataifa hatua za mwanzoni.
Pengine utashangaa na kujiuliza kwa nini tuichukulie Yanga kuwa imeshaaga michuano ya mwaka huu wakati ina mchezo wa marudiano utakaofanyika nyumbani mbele watazamaji wanaoiunga mkono.
Wakati nakiri Yanga itakuwa uwanja wa nyumbani na kutaraji kushangiliwa na maelfu ya wanachama na wapenzi wake, sina pumzi ya kuipandisha Yanga iwe na uwezo wa kupata ushindi utakaoiwezesha kuipiku Al Ahly.
Kabla yake, wawakilishi wa Tanzania waliotolewa michuanoni ni Mundu FC ya Zanzibar iliyoshindwa kwa jumla ya mabao 7-0 na Red Arrows ya Zambia katika Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), Prisons ya Mbeya (CAF) nayo ilitolewa na Walibya, Khalij Setr, kwa jumla ya magoli 6-0 na Miembeni ya Zanzibar ilitolewa katika klabu bingwa na
Timu nyingine ya Tanzania iliyotolewa ni Miembeni ya Zanzibar ilitolewa katika klabu bingwa na Monomotapa FC ya Zimbabwe. Baada ya kulala 3-1 ugenini, Miembeni ilishinda 1-0.
Mwaka ambao Tanzania ilifika mbali katika michuano ya klabu barani Afrika, ilikuwa 2003 pale Simba ilipoitoa Zamalek ya Misri hatua ya makundi na kufikia robo fainali.
Kutoka hapo, timu za Tanzania zimekuwa zikiishia raundi ya kwanza au ya pili.
Hapa tujiulize sababu ya matokeo hayo licha ya baadhi ya timu kusajili wachezaji mahiri na kuajiri makocha wenye uwezo?
Jibu rahisi hapa ni kwamba maandalizi mabovu ndio tatizo kubwa kwa timu zetu. Bado timu za Tanzania hazijafanikiwa kuendesha soka kisayansi.
Wahenga wana misemo yao, ukiwamo wa “Starehe gharama’ na soka ni miongoni mwa michezo ya starehe inayohitaji mipango mizuri na uwekezaji wa kutosha.
Wakati tunasubiri mchezo wa marudiano wa Yanga utakaokuwa tarehe 4 Aprili, ukiangalia mwenendo wa maandalizi kwa wawakilishi wetu, utaumia bure.
Fikiria mazingira yanayoikumba Yanga ambayo mara baada ya kupoteza ugenini, kocha wake, Dusan Kondic alitamka wazi kwamba timu hiyo ijihesabu kuwa imeshatoka kwenye michuano kwani haina uwezo wa kuifunga Al Ahly Dar es Salaam. Alisema Wamisri hao ni timu iliyojengeka vizuri.
Kama kweli, viongozi wa Yanga wanaamini katika sayansi ya soka, wangekuwa wameshatangaza kuwa wataileta timu kama Asec Mimosas ya Ivory Coast, Enyimba FC ya Nigeria, Canon Younde ya Cameroon au Asante Kotoko ya Ghana.
Tuache timu za magharibi mwa Afrika. Uongozi wa Mwenyekiti Iman Madega ungekwishaeleza mipango ya kuileta Orlando Pirates au Moroca Swallows za Afrika Kusini au Atletico Aviacao ya Angola kuja kupimana nguvu na Yanga.
Kwa kucheza timu kama hizo, hapa wachezaji wangepata uzoefu unaofanana na kupambana na Al Ahly.
Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema kwamba unapotaka kujilinganisha basi ujilinganishe na mtu mzima na siyo mgonjwa au aliyedhoofu kama ulivyo wewe.
Kwa kiwango cha Yanga na kwa kuzingatia timu inayokabiliana nayo, inatakiwa kujipima na wenye uwezo badala ya kucheza na Azam FC au Mtibwa Sugar. Hatuwezi kufika.
Kwa hiyo, hata kama ingesajili nyota zaidi, kwa kutegemea maandalizi ya zimamoto tutabakia kuwa watalii.
Kwa hali inayokwenda timu zetu, zinawania kushiriki michuano hiyo kwa ajili ya kwenda kutembea.
Hapa lazima tukubali kuwa tumefuna tulichopanda na hakuna haja ya kumshika uchawi kwa timu zetu kuboronga.
Sikushangaa Kocha Mkuu wa Yanga, aliponukuliwa na vyombo vya habari kwa kusema: “Yanga imechelewa”.
Hapa nampongeza, kwani amesema ukweli wake na msema kweli ni mpenzi wa Mungu.
Kwa maandalizi haya ya kimzahamzaha, labda zile nchi zinazotisha zijitoe mashindanoni ndiyo tutaweza kufanya vizuri.
Kwa mfano zipo nchi sugu barani Afrika hazikushiriki kwenye nane bora katika michuano ya CHAN, kutokana na kutoyapa uzito mashindano hayo. Mifano ya nchi hizi ni Tunisia na Misri. Haya sasa na ile michuano ya CECAFA, na tumekuwa wasindikizaji hata kama tutaiandaa sisi wenyewe.
Ukiangalia tangu Simba ichukue Kombe hilo mwaka 2002, kuanzia mwaka uliofuata 2003, tumekuwa washiriki tu. Ukiangalia hata nchi za Afrika zinazopata nafasi kwenye fainali za kombe la Dunia hufanya maandalizi ya kutisha.
Huwezi kusikia zikijiandaa kwa kucheza na Msumbiji, Tanzania au Comoro. Mara nyingi hujipima kwa kupambana na England, Ujerumani na Argentina. Kwa hiyo hata sisi inabidi tufuate nyayo vinginevyo tutabaki kuwa watalii milele.