Kwa mwenendo huu hatutafika


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version

HIVI karibuni serikali ilitangaza majina ya walioteuliwa kuwa wakuu wa wilaya. Ukimaliza kuyapitia majina yote unajiwa na maswali mengi, moja gumu ni, ‘Hivi kuwatangaza tu watu hawa, ndiyo kumeichukua serikali  miaka miwili?’ Ugumu ulikuwa wapi?

Hawa watafanyakazi kwa miaka mitatu tu, halafu watalipwa mafao na marupurupu kibao! Serikali hii inachezea hovyo fedha za walipa.

Siku chache baada ya kutangaza wakuu hao wa wilaya, Tarime wakatangaza mgogoro dhidi ya mteule wa Rais Jakaya Kikwete. Madiwani wote 39 waliweka kando tofauti zao za kiitikadi, wakaungana pamoja kumkataa mkuu wa wilaya, John Henjewele.

Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ester Matiku amesikika akisema kumbakisha Henjewele, Rais Kikwete hakuwatendea haki wananchi wa Tarime. Siyo Tarime tu madiwani wa Geita nao kwa kauli moja wamemkataa mkuu wa wilaya mteule wa Rais.

Lakini kwanini mtu akae Magogoni halafu achague watu kwa faida yake na awatume watu hao kwenda kuwatawala watu wa Tarime au Mbozi au Geita au wilaya nyingine? Hivi ndivyo walivyokuwa wanafanya wakoloni. Je, sisi tuna sababu ya kuendeleza ukoloni huo?

Mkuu wa wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario ameangua kilio; anadai kuwa wananchi wanataka kumtoa roho. Kimario atuambie aliwafanya nini watu wa Igunga mpaka waazimie kumuua?

Hili liwe fundisho kwa wakuu wa wilaya wote na wenzao wakuu wa mikoa ambao wanatanguliza maslahi ya chama chao badala ya maslahi ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.

Wakuu wa wilaya, kama walivyo wakuu wa mikoa, ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wanawekwa kwenye wilaya au mikoa kumwakilisha Rais. Hawana lolote wanalolifanya kwa ajili ya wananchi wa  wilaya au mikoa yao katika ujumla wao.

Kule wilayani kuna madiwani waliochaguliwa na wananchi wenyewe, na kuna wabunge waliochaguliwa na wananchi.

Pia kuna meya na mwenyekiti wa halmashauri. Mkuu wa wilaya anawekwa huko kufanya kazi gani? Huku ni kuongeza mzigo usio wa lazima kwa walipa kodi.

Tazama kiasi kikubwa cha fedha kilichofujwa kwa kile kilichoitwa sherehe za miaka 50 ya uhuru. Na fedha zilizofujwa kwa wale mawaziri nane waliotuhumiwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinafikia karibu sawa na bajeti ya serikali ya mwaka mzima.

Sasa umaskini wa nchi yetu hapa uko wapi? Wananchi wanataka kuwaondoa watesi wao mkuu wa wilaya lakini mko unawakingia kifua.

Wakati mabilioi ya shilingi yanafujwa, wanafunzi wa darasa la tano na la sita wa shule ya msingi Kidugalo, wilayani Namtumbo katika mkoa wa Ruvuma wanasomea katika chumba kimoja kutokana na uchache wa vyumba vya madarasa.

Wenzao wa darasa la sita katika shule ya msingi Selous iliyopo wilayani humo humo Namtumbo, kusema ule ukweli, wanasomea nje. Darasa lao ni paa tu la nyasi lililoshikiliwa na miti na kulifanya darasa kuonekana kama turubai linavyowekwa msibani.

Baada ya habari hizo nikageuza macho kuitazama picha ambayo Rais wangu alipiga pamoja na mawaziri wake. Kundi kubwa kweli la watu mpaka mtu unatishika!

Nikajiuliza kwa nini kundi kubwa hivi? Au nchi yetu ni kubwa sana! Hapana. Mbona Marekani ni kubwa zaidi na haina kundi kubwa la mawaziri kama hili! Au Watanzania tuko wengi sana! Hapana mbona Wafaransa ni wengi zaidi yetu na hawana kundi kubwa la mawaziri kama hili!

Tena tunaambiwa bado kuna malalamiko, wengine wamekosa. Ala kumbe tatizo ni kula! Kila aliyeshiriki kufika hapa lazima amegewe kipande chake ale! Ole wao wanamtandao.

Laiti kama Mwenyezi Mungu angenijalia uwezo wa kumlaani mtu ningewalaani wote “waliowaficha” waja wake ukweli ambao ungewaondolea mateso haya.

Halafu nilipokea ujumbe uliosema, “Ndugu Mayega, waliobadilishwa ni baadhi tu ya wanamuziki. Bendi ni ileile, mtindo wa muziki ni uleule, vyombo vya muziki ni vilevile. Usisahau kuwa kiongozi wa bendi ni yuleyule. Hata unenguaji pia utakuwa ni uleule”

Haya maneno yanaonyesha Watanzania walivyokosa imani na serikali yao.

Sasa kuna mawaziri na naibu mawaziri hawaruhusiwi kuhudhuria vikao vya kamati za Bunge kwa vile kuteuliwa kwao kuwa wabunge na halafu kuwa mawaziri na kuapishwa kumekiuka katiba.

Bunge linasema hao hawajawa wabunge, kwa sababu hiyo, hawawezi kuteuliwa uwaziri. Kutokana na kosa hilo, hawawezi kushiriki katika vikao vya bunge hadi watakapoapa kiapo cha uaminifu wa Bunge.

Lakini mwanasheria mkuu wa serikali anayepaswa kuwa mjuzi wa sheria na katiba, Frederick Werema anasema hao ni wabunge.

Rais wa wanasheria wa Tanganyika anasema katiba iko kimya. Kama katiba iko kimya si tutumie akili zetu? Kipi kianze? Kwa precedence (msingi wa matumizi ya utaratibu uliozoelekea) si kiapo cha ubunge kinaanza kabla ya uwaziri ?

Kwa nini tunaendesha nchi kama tairi lililochomoka kwenye gari? Mabadiliko ya watu peke yake hayana maana yoyote. Bila kwanza kuweka msimamizi madhubuti kinachofanyika ni kubadilisha walaji tu.

Kama lengo ni kumshirikisha kila mkuu wa wilaya, mkoa, au mawaziri na wengine nchi itabaki mifupa mitupu katika hii miaka mitatu ya mashaka iliyobaki. Kwa hakika walitenda dhambi kubwa waliowaficha Watanzania ukweli.

Hivi wanaposema wajinga ndio waliwao ni kwa milele yote? Siamini kwa sababu wengine wanasema siku bubu mambo yatakapomzidia atasema! Naihofia siku hiyo! Wache wale kuku maskini wanalalia pumba.

Naungana na wanaosema muundo na imani ya CCM ni mzuri. Tatizo ni uongozi, utendaji hakuna. Ni dhaifu mno katika kufanya maamuzi. Mara nyingine yamefanyika maamuzi yasiyo sahihi na wakati mwingine maamuzi yakifanyika yakiwa yamechelewa mno kiasi cha kupoteza maana. Chama kinahitaji uongozi mpya ulio imara. Hii si kwa faida ya chama tu bali kwa afya ya Taifa hili vinginevyo kwa mwendo huu hatufiki!

0713334239
0
No votes yet