Kwa nini wapiga kura wanapungua?


Jonathan Liech's picture

Na Jonathan Liech - Imechapwa 02 June 2009

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

KUMALIZIKA kwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Busanda mkoani Mwanza hivi karibuni, kunaleta nafasi ya mjadala kwa yale yaliyotokea.

Ni mjadala wa iwapo taifa masikini lina uwezo wa kufanya uchaguzi mdogo kila kiti cha ubunge kinapokuwa wazi. Hili ni zoezi linalotumia fedha nyingi za walipakodi, ambazo zingetumika kuimarisha huduma za jamii.

Hivyo, kuna wanaosema yaletwe mabadiliko ili uchaguzi uwe sawa na ule wa nchi kama Afrika Kusini, ambako inapotokea mbunge amefariki dunia, chama chake hutakiwa kujaza nafasi hiyo bila ya kufanyika uchaguzi mdogo.

Nchi hii haiwezi kuendelea kupoteza raslimali zake kwa mambo yasiyo ya msingi sana.

Hata hivyo, mjadala huu, si muhimu zaidi kuliko hili ambalo tumekuwa tukilisikia na kulidharau bila ya kujua madhara yake huko tuendako.

Ninachozungumzia hapa ni ile hali iliyojitokeza tangu kuanzishwa kwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kwamba idadi ya wanaopiga kura ni ndogo mno kuliko ile iliyoandikishwa.

Tatizo hili limejitokeza katika karibu chaguzi zote ndogo zilizofanyika tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Kilele chake kilikuwa ni katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini uliofanyika mwaka huu ambapo kati ya wapiga kura 127,000 walioandikishwa, ni 44,855 sawa na asilimia 35 tu waliojitokeza kupiga kura.

Mbeya Vijijini ilikuwa ni kilele, lakini haya yalijitokeza pia katika chaguzi nyingine ndogo zilizofanyika. Kwa mfano, Tarime kulikuwapo na wapiga kura 64,795 wakati ilitarajiwa watu zaidi ya 140,000 kupiga kura.

Na hata Busanda hadithi imekuwa ile ile. Kati ya watu 130,000 waliotarajiwa kupiga kura, ni watu 55,460 sawa na asilimia 41 tu waliopiga kura.

Kama ningekuwa naishi Sweden au nchi nyingine yoyote iliyoendelea, takwimu hizi zisingenitia hofu hata kidogo. Kwa wenzetu haya ni mambo ya kawaida.

Katika nchi zilizoendelea, kwa kawaida wapiga kura ni wachache, labda atokee mgombea wa kipekee wa aina ya Barrack Obama.

Katika nchi hizo, watu tayari wana maji ya uhakika, barabara zinazopitika muda wote, umeme ni kwa kila mtu, shule zina walimu. Kwa kifupi, wagombea au vyama vinashindania mambo mapya, tofauti na hapa.

Ndiyo sababu siku hizi utasikia chama hiki ni cha kutetea mazingira, kile cha kutetea haki za mashoga, utoaji mimba na mambo mengine. Haya yote hayawezi kuwa hoja ya uchaguzi katika nchi masikini.

Nchini na Afrika kwa ujumla, watu wanataka maji na barabara; hawana kila kitu na ndiyo maana uchaguzi huwa ni jambo kubwa.

Hivyo, ni jambo la kushangaza kuona kwamba, katika mazingira kama ya Busanda hakuna maji, umeme, shule za maana na miundombinu mingine, eti asilimia 41 tu ya watu ndio wanakwenda kupiga kura.

Bila shaka kuna tatizo kubwa limejificha hapa. Katika mazingira ya kawaida kabisa, mtu angetarajia walau nusu ya walioandikishwa wangejitokeza kupiga kura na sababu zipo wazi.

Kwanza, kuna mambo ya kukera au kufurahisha, ambayo yanaweza kuwafanya wananchi kukipigia kura chama tawala au wapinzani.

Lakini kubwa ni kwamba kulikuwapo na hamasa ya kutosha kabla ya siku ya kupiga kura. CCM ilipiga kambi Busanda, na vivyo hivyo kwa Chadema na CUF.

Purukushani za wafuasi wa vyama hivyo vya siasa, helikopta ya Chadema na mambo mengine mengi, vingetosha kuwafanya wananchi wasubiri kwa hamu siku ya kupiga kura.

Sasa inakuwaje katika kila watu kumi waliojiandikisha ni wanne tu ndiyo walienda kupiga kura? Hamasa zote za kampeni zilikwenda wapi? Matatizo na raha zote za Busanda zilipotelea wapi? Kwa maoni yangu, hapa kuna kilichofichika.

Demokrasia inajengwa na dhana nzima ya wengi wape. Katika chaguzi ndogo zote zilizofuata uchaguzi mkuu wa 2005, dhana ya wengi wape haikushinda.

Ni kweli kwamba asilimia kubwa ya waliopiga kura Mbeya Vijijini, Tarime, Busanda, Kiteto na Tunduru, ndio walioamua mshindi, lakini itakuwa utani tukisema hiyo ndiyo iliyokuwa sauti ya wengi.

Kama wananchi hawaendi kupiga kura kwa wingi katika nchi masikini kama Tanzania, maana yake ni kwamba kuna tatizo kubwa, ambalo halionekani haraka.

Yaweza kuwa wamekosa imani na mfumo wa uchaguzi wa nchi yao. Na kama hilo ni kweli, maana yake ni kwamba ni hatari kwa taifa. Kama watu hawaamini katika demokrasia, wanaamini katika nini?

Kuna wanaosema kwamba kuna wananchi wanaamini CCM imekuwa ikicheza rafu mno nyakati za uchaguzi, kiasi kwamba hawaoni tena umuhimu wa kwenda kupiga kura.

Kuna wanaoamini kwamba baadhi ya vyama vimekuwa vikinunua shahada za kupigia kura kwa wingi na hivyo kusababisha kupungua kwa idadi ya wapiga kura.

Lakini kuna wale wanaosema kwamba inawezekana Daftari la Kudumu la Wapiga Kura “limechezewa” na kwamba idadi ya wapiga kura tunayotangaziwa ni hewa tu.

Kwamba, wakati ule wa uandikishaji, kuna watu walijiandikisha zaidi ya mara moja katika maeneo tofauti. Kwamba, kuna watu waliongeza tu idadi ya wapiga kura kwa sababu ambazo wenyewe wanazifahamu zaidi kuliko sisi.

Kama lolote kati ya haya linafanyika, basi taifa letu lipo katika hali ya hatari. Ubakaji wowote unaofanywa dhidi ya demokrasia huwa na madhara makubwa, ama wakati uleule, au baadaye.

Panahitajika mjadala kuhusu nini hasa kimelipata taifa hadi kufikia hatua hii. Hivi kutakuwa na faida gani ya kuchagua rais wakati pengine ni watu watatu tu katika kila kumi ndio wanapiga kura?

Mfumo bora kama wa Afrika Kusini utafaa na utakuwa na maana iwapo tu watu watapiga kura kwa kiwango cha kuridhisha bila ya kuwapo na mushkeli wowote.

Tatizo hili lisipotafutiwa ufumbuzi hivi sasa, taifa litakuja kulipa gharama kubwa huko tuendako na tusijue wa kumkimbilia.

Sitarajii kuna siku watu wote walioandikishwa watapiga kura. Haijawahi kutokea duniani na pengine haitatokea milele.

Lakini tatizo nchini limekuja ghafla na kwa kasi sana. Panahitajika kufahamu chanzo na sababu zake. Tujadili.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: